MVUA kubwa inayoendelea kunyesha mfululizo katika maeneo mbalimbali
nchini imeendelea kuleta madhara ikiwamo kufariki dunia askari wa Jeshi
la Polisi aliyekumbwa na mkasa wa kusombwa na maji yaendayo kasi wakati
akiwa na pikipiki visiwani Zanzibar.
Aidha, mvua hizo zilizosababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali,
yakiwamo ya Tanga na Zanzibar na kusababisha maafa makubwa kwenye baadhi
ya maeneo nchini, zimewashtua wabunge ambao jana walitaka kusitishwa
kwa shughuli za Bunge ili kupata taarifa kamili na kujadili hatua za
kuchukua.
KIFO CHA POLISI
Licha ya kuendelea kuharibu miundombinu kama ya barabara na kubomoa
nyumba, mafuriko yatokanayo na mvua yaliendelea kuleta vilio baada ya
jana kusababisha kifo cha askari wa Jeshi la Polisi, Sajenti Abbas Anas
Haji (55). Marehemu alikumbwa na umauti baada ya kusombwa na maji katika
barabara ya Fuoni Kibonde Mzungu, Mkoa wa mjini Unguja, Zanzibar.
Akizungumza eneo la tukio, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi,
Hassan Nassir Ali, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 5:30
asubuhi wakati askari huyo akiwa na usafiri wa pikipiki (Vespa),
akitokea kazini Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, kuelekea nyumbani kwake.
Alisema alipofika katika eneo hilo, aliteleza na kuanguka kabla ya kusombwa na maji hayo.
Mwandishi wa Nipashe alifika katika eneo la tukio na kukuta umati wa
watu waliokuwa wakiendelea na shughuli za uokozi wa mwili wa marehemu
ambao ulikuwa hauonekani kutokana na maji mengi yaliyokuwapo.
Hata hivyo, vikosi vya uokoaji vilifanikiwa kuupata mwili wa askari huyo majira ya saa 9:30 jioni.
Kamanda Ali alisema marehemu ni wa kitengo cha picha Makao Makuu ya Jeshi hilo, Zanzibar.
Alisema eneo hilo ni hatari kutokana na barabara kufunikwa na maji
ambapo pembezoni mwa barabara hiyo kuna bonde kubwa la mpunga na maji
huwa mengi, yakipita barabarani kwa kasi na mengine kutuwama pembezoni.
“Hivi sasa haturuhusu waenda kwa miguu wala vyombo vya moto kupita eneo
hilo kwa sababu maji yana kasi kubwa na yanaweza kusababisha maafa
mengine,”alisema.
Alisema mwili wa marehemu umeshakabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya
mazishi ambayo yanatarajiwa kufanyika kwao, Fuoni Kibondeni.
Alisema Jeshi la Polisi limepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha askari
huyo na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari, hasa katika kipindi hiki
cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’,Unguja, Silima Ali Haji, alisema hali ya
mafuriko ya mvua si nzuri na maeneo mengi yameathirika na mvua hizo,
ikiwamo nyumba kujaa maji na pia barabara kutopitika kwa kufunikwa na
maji.
Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni barabara ya Mwanakwerekwe Sokoni
ambayo hivi sasa haipitiki, barabara ya Fuoni Kibonde Mzungu na eneo la
Tomondo Ziwa Maboga ambako nyumba nyingi hivi sasa zimejaa maji na
wananchi waliokuwapo kukosa mahala pa kuishi.
“Bado hatujafanya tathmini katika wilaya yangu familia ngapi zimekosa
makazi. Lakini athari za mvua ni kubwa na niwasihi wananchi wachukue
tahadhari kwani bado mvua zinaendelea kunyesha”alisema.
Akizungumzia kuhusu tukio la Mafuriko Bwejuu Mkoa wa Kusini Unguja
ambalo limeenea katika mitandao ya kijamii ya kwamba watu wanatembea
mitaani kwa mitumbwi, mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa mafuriko yapo
katika baadhi ya maeneo lakini siyo makubwa ya aina hiyo na kwamba,
video inayosambazwa haiakisi uhalisia wa eneo husika.
Akizungumzia kuhusu maafa ya mvua zinazoendelea kunyesha, Rais wa
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema serikali yake imekuwa ikifanya
juhudi mbalimbali za kuimarisha miundombinu ili kuhimili maafa hayo kwa
kuzuia maji yasituwame pasipostahili.
“Nimeshuhudia eneo la Tomondo Ziwa Maboga pamejaa maji. Nyumba nyingi
zimefukiwa na maji lakini kila wananchi wakitakiwa waondoke hawataki,”
alisema Dk. Shein, akisisitiza wananchi kuzingatia tahadhari
zinazotolewa kipindi hiki.
Aidha, imeelezwa kuwa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo
mbalimbali ya visiwa vya Unguja na Pemba zimeathiri nyumba 325 katika
Mkoa Kusini Pemba, nyumba 667 kukimbiwa na wakazi wake ndani ya Mkoa wa
Mjini Magharibi Unguja pamoja na kubomoka kwa miundombinu ya barabara na
baadhi ya madaraja.
WABUNGE WASHITUSHWA
Katika mjadala wa jana bungeni, wabunge waliitaka serikali kueleza
athari za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini
na hatua inazozichukua kuwapa unafuu wa maisha wananchi waliokumbwa na
mafuriko hayo.
Mjadala huo ulisababisha Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliyekuwa
anaongoza kikao cha Bunge, kuitaka serikali itoe tamko kuelezea jambo
hilo na hatua zilizochukuliwa.
Chenge alilazimika kuamua hivyo baada ya wabunge watatu kusimama kuomba
mwongozo wa Kiti cha Spika, huku baadhi yao wakitaka shughuli za Bunge
zisitishwe ili kujadili hoja hiyo waliyotaka ichukuliwe kuwa ni ya
dharura.
Wabunge walioomba mwongozo wa Kiti cha Spika ni Stephen Ngonyani 'Prof.
Majimarefu' (Korogwe Vijijini-CCM), James Mbatia (Vunjo-NCCR Mageuzi) na
Rashid Shangazi (Mlalo-CCM).
Akiwasilisha hoja yake, Prof. Majimarefu alitumia Kanuni ya 68(7)
akisema kuna athari kubwa nchini zilizosababishwa na mafuriko nchini.
“Kwenye mkoa wangu wa Tanga kumekuwa na maafa. Leo (jana) hii
tunavyoongea kuna watu 1,000 hawana chakula, mahali pa kuishi na hawana
msaada wowote," alisema.
"Serikali itawasaidiaje hawa watu wakati kamati za afya zikiendelea na utaratibu?" Alihoji.
Katika kujenga hoja yake, Shangazi aliyesimama kwa kuzingatia Kanuni ya
47(1), alitaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili wabunge wajadili kuhusu
mafuriko hayo.
“Sasa hivi katika Mkoa wa Tanga kuna mafuriko makubwa sana. Na jana
(juzi) yametokea maporomoko katika Milima ya Usambara, eneo la barabara
za Lushoto-Arusha-Mombo, Pangani-Tanga, Mombo kwenda Lushoto na
Kilindi-Morogoro zote zilifungwa,” alisema Shangazi.
Alisema Mkoa wa Tanga umegeuka kuwa kisiwa ghafla na umepata athari
kubwa na kuiomba serikali ilione jambo hilo ni la kimkakati na Wakala wa
Barabara (Tanroads) umezidiwa.
Mbatia alisema hali ni tete katika mikoa mingi nchini ikiwamo
Kilimanjaro, Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Zanzibar kufuatia mafuriko
yaliyojitokeza na kuomba utu kuzingatiwa miongoni mwa wabunge kwa kuamua
kutenga walau robo saa kujadili suala hilo na kupendekeza hatua za
kuchukua.
“Tutenge muda wa dakika 15 ama 20 ili tujadili suala hili ambalo ni la
maafa. Tunaweza tukatoa majibu sahihi kwa wapigakura wetu," alisema.
Akijibu maombi ya wabunge hao, Chenge, akirejea kanuni, alisema kwa hali
anayoiona, haoni kama suala hilo linahitaji kujadiliwa bungeni kwa
kipindi hicho.
“Ni kweli tukio hili limegusa maeneo mengi, nawapa pole walioguswa kwa
namna moja hata nyingine. Naamini Serikali iliyoko humu ndani, itaitolea
maelezo wakiangalia nchi nzima,”alisema Chenge.
Alisema anaamini serikali italizungumzia vizuri suala hilo kuliko kila mbunge kujisemea katika eneo lake.
Akijibu ombi la Prof. Majimarefu, Chenge alisema Kanuni ya 68(7) kuhusu
kuomba mwongozo wa Kiti cha Spika, ina sharti la lazima mwongozo huo
uombwe kwa tukio ambalo limetokea mapema bungeni na si nje ya chombo
hicho cha kutunga sheria.
HALI YA TANGA
Kutoka Tanga, inaelezwa kuwa mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo
zinaendelea kuleta athari na hivyo kukata mawasiliano kati ya mikoa ya
Kiliamanjaro na Arusha.
Zaidi ya magari yameharibika vibaya baada ya kupondwa na mawe makubwa yaliyoporomoka kutoka juu ya milima kwenda barabarani .
Mawe hayo yalifunika baadhi ya magari na kufunga kabisa barabara
zinazoelekea wilayani Lushoto lakini kwa mujibu wa serikali mpaka jana
hali imerudi shwari na magari yameanza kupita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, alisema jana kuwa
magari hayo yameharibika baada ya kuangukiwa na udongo ambao umetoka juu
ya milima katika barabara kuu ya kutokaka wilayani Korogwe kuelekea
Soni Wilaya ya Lushoto.
Alisema katika ajali hiyo watu nane walijeruhiwa vibaya na walipelekwa
katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kwa matibabu na wameruhusiwa
kurudi nyumbani baada ya kutibiwa.
Kamanda Wakulyamba alisema kuwa magari yaliyoharibika kwa kuangukiwa na
udongo wa mawe kutoka milimani kuwa ni Toyota Coaster mbili, Toyota
Carina, Noah na Toyota Hilux na kwamba barabara ya kutoka Mombo kwenda
Lushoto iliyokuwa imefungwa, sasa imefunguliwa na magari yameanza kupita
kwa tahadhari kubwa.
Hata hivyo, mawasiliano kati ya Pangani na Tanga mjini yamekatika baada ya daraja kubomoka eneo la Neema jijini Tanga.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment