Uamuzi wa Serikali wa kuwafukuza kazi watumishi wanaodaiwa kughushi
vyeti, umezidi kuchukua sura mpya, baada ya watumishi sita wa
Halmashauri ya Kilwa mkoani Lindi kufungwa jela mwaka mmoja kila mmoja
kwa kosa la kughushi vyeti vya kidato cha nne na kujipatia ajira.
Taarifa nyingine zinasema Katibu Tawala wa Wilaya ya Tandahimba (DAS),
Mohamed Azizi naye ameguswa na sakata la vyeti feki baada ya kutajwa
katika orodha ya watumishi wenye vyeti feki akiwa namba 5356.
Chanzo cha uhakika kutoka ofisi ya DAS kimesema kuwa, tayari kiongozi
huyo ameshaondoka Mtwara kuelekea Dar es Salaam kupeleka malalamiko yake
katika mamlaka za juu kwamba jina lake limeingizwa kimakosa katika
orodha hiyo.
Taarifa nyingine kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini zinasema
zahanati mbili zimefungwa baada ya watumishi wote waliokuwapo kukumbwa
na sakata la vyeti feki.
Madereva hao, walihukumiwa jana na Mahakama ya Wilaya ya Kilwa, baada
ya kupatikana na hatia ya makosa matatu ya kufoji vyeti vya kidato cha
nne.
Hukumu hiyo, imetolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Gabriel Ngaeje baada
ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Madereva waliohukumiwa ni Juma Sungura, Issa Juma Abdurahamani, Abdull Chubi, Dactuce, Ahamadi Selemani na Abdallah Kilolopera.
Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Hakimu Ngaeje aliwauliza washtakiwa kama
wana sababu zitakazoishawishi mahakama isiwape adhabu kali.
Kila mmoja kwa wakati wake, aliomba mahakama iwaonee huruma, kwani wana
familia zinazowategemea, hivyo iwapo watapewa adhabu kali kuna hatari ya
kukosa matunzo yao.
Naye mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Emmanuel Camilius aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho
kwa watuhumiwa na watu wengine wenye tabia ya aina hiyo ndani ya Mkoa wa
Lindi na Taifa kwa ujumla.
“Tabia ya aina hii si ya kuifumbia macho, kazi wanazozifanya zinahusu
usalama wa watu, kugushi vyeti kwa ajili ya kujipatia ajira ni
hatari,”alisema Camulius.
Hakimu Ngaeje, akitoa hukumu katika kesi hiyo namba 07/2014, alisema
amesikiliza maombi ya pande zote mbili, hivyo akawahukumu kila mmoja
kifungo cha nje cha miezi (12) kwa kila kosa na kufanya idadi ya miezi
(196).
“Kwa vile adhabu inakwenda pamoja, mtatumikia kifungo cha nje miezi 12,”alisema.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwanasheria Camilius, kuwa watumishi
hao wakijua wanachokifanya ni makosa, walifoji vyeti vya kidato cha nne
na kujipatia ajira kinyume na sheria ya nchi.
Naye Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), alisema zahanati mbili
katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini mkoani Lindi, zimefungwa
baada ya watumishi wake kutajwa katika orodha ya watumishi wa umma wenye
vyeti feki.
Bobali alitoa taarifa hiyo bungeni mjini Dodoma jana, alipokuwa
akichangia bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, kwa mwaka wa fedha 2017/18.
“Mheshimiwa mwenyekiti, hili suala la vyeti feki limeleta shida katika
Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini kwa sababu kuna zahanati mbili
zimefungwa, baada ya watumishi wake wote kubainika wana vyeti feki.
“Kwa hiyo, namwomba mheshimiwa waziri, achukue hatua haraka,” alisema Bobali wakati alipokuwa akihitimisha mchango wake.
Pamoja na kusema hayo bungeni, nje ya bunge Bobali alisema a zahanati
zilizofungwa ziko katika Jimbo la Mtama katika Halmashauri ya Wilaya ya
Lindi Vijijini.
“Zahanati zilizofungwa ni za Mkanga 2 na Sudi ambazo zote ziko pembezoni
kabisa ya mji, kiasi kwamba kitendo cha kuzifunga, kitaathiri mno
wananchi.
“Kwa hiyo, ndiyo maana nilimwomba mheshimiwa waziri afanye kila
analoweza kuhakikisha zinafunguliwa haraka ili kunusuru maisha ya
wananchi,”alisema Bobali.
Kwa mujibu wa Bobali, zahanati hizo zilikuwa na watumishi watatu watatu kila moja.
Taarifa zaidi kutoka Lindi, zinasema watumishi 236 wa Serikali wamegundulika kutumia vyeti feki.
Katika sakata hilo, halmashauri za wilaya za Nachingwea na Kilwa zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey
Zambi alizitaja wilaya na idaidi ya watumishi kwenye mabano, kuwa ni
Nachingwea (72), Kilwa (53), Ruangwa (45),Lindi Vijijini (25), Ofisi ya
Katibu Tawala (RAS) (23), Manispaa (11) na Liwale (7).
Alisema katika idadi hiyo, idara za afya na elimu zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watumishi wa vyeti feki.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment