Siku
chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kutoa agizo la kupunguza
mishahara mikubwa ya watendaji wa mashirika ya umma, hatimaye Serikali
kupitia Bodi ya Mishahara imeanza kazi ya kufanya marekebisho hayo.
Hatua
hiyo imekuja baada ya Rais Magufuli, kuagiza kushushwa kwa viwango vya
mishahara ya viongozi wa mashirika ya umma ambapo wengine hulipwa Sh
milioni 36 hadi milioni 40 kwa mwezi.
Jana
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Angellah Kairuki, alisema katika kipindi cha miezi 15 kuanzia
sasa mishahara ya watumishi hao itapunguzwa na kuwa yenye uwiano.
“Katika
kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa tunayo Bodi ya Mishahara ambayo
ilianzishwa katika Serikali ya awamu ya nne na jukumu lake kubwa ni
kufanya mapitio ya mishahara mbalimbali na kuhakikisha mishahara ya
watumishi wa umma haipishani sana.
“Hatua
ambazo tumeanza kuzitekeleza, tayari mamlaka zetu zimeanza kukutana
kupitia Utumishi, Hazina na Msajili wa Hazina ili kuangalia namna ya
kulitekeleza agizo hilo,” alisema Waziri Kairuki.
Alisema
kutokana na hali hiyo mamlaka hizo hivi sasa zinaangalia mishahara ya
taasisi mbalimbali na watumishi ili kuweza kubaini wale wanaolipwa zaidi
ya Sh milioni 15 ni wangapi na itakatwa vipi.
Akizungumzia
taasisi zinazozalisha kwa kiwango kikubwa na kuwa na uwezo wa
kujiendesha, Waziri Kairuki, alisema Bodi ya Mishahara hivi sasa ina
jukumu la kuangalia uwiano baina ya mtumishi wa umma na mashirika ya
Serikali.
“Unakuta
mtumishi wa taasisi X kiwango chake cha elimu, uzoefu, ujuzi, muda wa
kuingia kazini pamoja na kazi anayoifanya ni sawa na ya mtumishi wa
taasisi Y lakini unakuta mtumishi X analipwa mshahara mkubwa zaidi ya
mara tano ya mtumishi Y jambo ambalo si haki katika utumishi,” alisema.
Kauli ya Rais Magufuli
Machi
30, mwaka huu akiwa wilayani Chato, Mkuu huyo wa nchi, alisema kuna
watu wanalipwa kiwango kikubwa cha mishahara na wamekuwa wakiishi kuliko
hata malaika na sasa ni lazima washushwe ili waishi kama shetani.
Hatua
ya Rais Magufuli, kupitisha panga na kuweka uwiano wa mishahara kwa
watendaji wa taasisi hizo unaelezwa kuwa utaisaidia uwajibikaji na usawa
kwa watendaji.
Katika
mkutano huo, Rais Magufuli, alishangazwa na baadhi ya bodi za
wakurugenzi kushindwa kufanyakazi zao kwa mujibu wa sheria na badala
yake wamekuwa na kazi ya kupandisha mishahara kwa watendaji.
Alisema
anashangazwa na bodi hizo, kwani kila kukicha zimekuwa zikifanya kazi
ya kupandisha mishahara pamoja na kufanya vikao nje ya nchi.
Alisema
hivi sasa ameunda timu ya wataalamu ambayo imeanza kufanya kazi ya
upunguzaji mishahara mikubwa kwa watendaji wakuu wa mashirika ya umma.
“Tena
hawa wakurugenzi ndio wanaongoza kwa kulipwa fedha nyingi na hata
kwenda kufanya vikao ulaya. Ninasema hapa kwamba suala hili litaanza
kushughulikiwa katika bajeti hivi karibuni,” alisema Rais Magufuli.
Alisema
tayari ameunda timu ya wataalamu ambayo inafanya kazi ya kupunguza
mishahara hiyo na kufikia Sh milioni 15 kwa mwezi ili asipatikane
Mtanzania anayelipwa zaidi ya kiwango hicho.
“Kuna watu wanaishi kuliko hata malaika lazima tuwashushe waishi kama shetani,” alisema Rais Magufuli.
0 comments:
Post a Comment