CHAMA
cha Wananchi (CUF) kimelitaka Jeshi la Polisi kuwapandisha mahakamani
viongozi wake wanaowashikilia kwa tuhuma za uchochezi kisiwani Pemba.
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa jana, Mkurugenzi wa
Habari na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Salim Bimani, alisema kama
polisi wana ushahidi wa viongozi wa CUF na wafuasi wao kujihusisha na
matukio ya uvunjifu wa amani basi wawapeleke mahakamani.
Bimani
alisema wanasikitishwa na hatua ya jeshi hilo kuwaweka ndani viongozi na
wafuasi wao kwa muda mrefu bila ya kuwafikisha mahakamani kinyume na
haki za binaadamu.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi kama wana ushahidi
juu ya viongozi wetu ambao wanawahusisha na matukio ya uvunjifu wa amani
kisiwani Pemba basi wawapeleke mahakamani,” alisema Bimani.
Bimani
alisema kuwa tokea kuanzishwa mfumo wa vyama vingi Tanzania kumekuwa na
unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya raia hasa wanachama wa CUF jambo
ambalo alisema kuwa linafanyika kwa nia ya kukikandamiza chama hicho.
“Ikiwa
sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo kila wakati Zanzibar imekuwa
ikishuhudia kuletwa askari wengi katika kipindi cha uchaguzi,” alisema
Bimani.
Hata hivyo, alisema kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi
wa Oktoba 25, 2015, kumekuwa na hatua kadhaa za unyanyasaji dhidi ya
wafuasi wa chama hicho unaofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Haya
yote yanayofanyika ili kuzima sauti za watu, lakini tunawaambia
viongozi wa CCM pamoja na vyombo vya dola, tutaendeleza msimamo wetu wa
haki sawa kwa wote,” alisema Bimani.
Alisema CUF inalaani vitendo
vya hujuma dhidi ya raia na mali zao unaofanywa kwa lengo la kuvipa
sababu vyombo vya ulinzi na hasa wafuasi wake, pamoja na kulaani kauli
za vitisho na lugha za kibabe zinazotolewa na Jeshi la Polisi Zanzibar,
kama vile iliyotolewa Juni 28 mwaka huu na Naibu Mkurugenzi wa Upepelezi
Salum Msangi kisiwani Pemba kwa lengo la kuwanyamazisha wananchi ili
kuisambaratisha CUF.
0 comments:
Post a Comment