India
imeipatia Tanzania dola za Kimarekani milioni 500 kwa ajili ya miradi
ya maendeleo ili kukuza ushirikiano wa kiuchumi baina nchi hizi mbili.
Hayo
yamesemwa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Magufuli katika dhifa ya kitaifa aliyomwandalia mgeni
wake , Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi,Ikulu jijini Dar
es Salaam.
“Tunaishukuru
India ambayo imeonyesha utayari wa kushirikiana nasi kiuchumi katika
kilimo, TEHAMA, maji, Elimu, Afya na Ulinzi,” amesema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli pia amesema ushirikiano wetu na India utatoa fursa kwa
Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda kwani katika
ziara hii Waziri Mkuu ameambatana na wafanyabiashara takriban 50 ambao
wanaangalia fursa za kibiashara hapa nchini.
“India
ni mdau wetu mkubwa wa kibiashara na uhusiano huu umekuwa ukikua
kwani mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini India yameongezaka toka thamani
ya dola za kimarekani milioni 187 mwaka 2005 hadi dola bilioni 1.29
mwaka 2015,”alisema Rais Magufuli.
Aidha,
Rais Magufuli amesema kuwa India itatoa fedha kwa nchi ya Tanzania kwa
ajili ya kilimo cha Dengu ambayo ni fursa ya ajira kwa watanzania na
kuinua kipato cha wananchi.
Rais
Magufuli ameeleza kufurahishwa kwake na miradi ya India ikiwemo mradi
unaojulikana kama Making India, mradi ambao unatumia malighafi
zinazopatikana nchini na kutumia nguvu kazi ya nchini ambao utapunguza
tatizo la ajira katika Taifa la Tanzania.
Amebainisha
kuwa India iko tayari kushirikiana na Tanzania kwenye miradi ya gesi
ikizingatiwa kuwa aina mbali mbali za gesi zinazidi kugunduliwa hapa
nchini. Katika suala la gesi India iko tayari kutoa utaalamu na
wataalamu kwa ajili miradi ya gesi.
Kwa
upande wake Waziri Mkuu wa India , Mhe. Narendra Modi ameishukuru
Tanzania kwa ukarimu alioupata hapa nchini na akaahidi kuendeleza
ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili.
Amesema
India italeta watu wake, utaalaamu na teknolojia yake kwa Tanzania,
jambo ambalo litaongeza ushirikiano wa kiuchuni kati India na Tanzania.
Waziri
Mkuu huyo amemaliza ziara yake ya kiserikali ya siku mbili nchini na
kuondoka kuendelea na ziara katika nchi nyingine za Ukanda wa Afrika
Mashariki.
0 comments:
Post a Comment