Serikali
ya India na Tanzania zimesaini mikataba ya miradi ya maendeleo katika
sekta za maji, kilimo, viwanda, teknolojia ya habari na mawasiliano na
afya katika kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili ili kusaidia
wananchi wake.
Mikataba
hiyo imesainiwa leo, wakati Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi
alipokuakifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mikataba wa kwanza uliosainiwa inahusisha mradi wa kusambaza maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Aidha,
mkataba wa pili unahusisha mradi wa kusambaza maji Zanzibar ambao
unatarajiwa kugharimu dola za kimarekani milioni 92 ambapo mradi huo
unatarajiwa kufikia miji 17 nchini na mkataba mwingine utahusisha
mafunzo ya ufundi yatakayosaidia kuzalisha wataalamu mbalimbali.
“Lengo
letu ni kusaidiana na kuimarisha mahusianao yetu katika kukuza uchumi
na kutengeneza fursa mpya za ajira kwa wananchi wetu” alisema Waziri
Modi.
Waziri
Modi aliongeza kuwa Serikali ya India itaendelea kushirikiana na
Serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni
pamoja na kuongeza wigo wa biashara na hatimaye kukuza uchumi wa nchi
hizo.
Kwa
upande wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli
alisema Serikali India imekua na ushirikiano mzuri na Tanzania hasa
katika masuala ya maendeleo ambapo imeweza kuwekeza nchini kiasi
shilingi za Kimarekani dola bilioni 2.4 na kuzalisha ajira 54,176.
Baadhi
ya misaada iliyotolewa na Serikali ya India ni pamoja na mashine ya
vipimo vya ugonjwa wa kansa katika hospitali ya Bugando, itakayosaidia
wakazi wa kanda ya ziwa na nchi nzima kwa ujumla pamoja na kuongeza na
kuimarisha ushirikiano kati ya Shirika la viwanda vidogo vigodo la India
kushirikiana na Tanzania katika kukuza viwanda vidogo na vya kati
nchini.
Katika
masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, Serikali hiyo imeahidi
kuleta wataalamu wao nchini Tanzania kwa lengo la kutengeneza program
mbalimbali ili kuisaidia Tanzania katika masuala ya ulinzi wa mitandao
pamoja na kutengeneza namna bora za ukusanyaji wa mapato ya nchi.
Katika
masuala ya viwanda, Serikali ya India imeahidi kuanzisha viwanda vya
kutengeneza dawa za binadamu zitakazotibu magonjwa mbalimbali ikiwemo
malaria, figo na kisukari, ikiwa ni pamoja na kutengeneza vifaa tiba
vitakavyotumika katika hospitali mbalimbali nchini kwa lengo la
kupunguza gharama ya kununua vifaa hivyo nje ya nchi.
Aidha,
Rais Magufuli alisema kuwa nchi ya India ina uhitaji mkubwa wa mazao ya
kilimo hasa jamii ya kunde hivyo akawataka wakulima kutumia fursa hiyo
kuzalisha mazao hayo kwa wingi.
“India
inauhitaji wa tani 200 za mazao jamii ya kunde, wakulima mnatakiwa
kuzalisha mazao hayo kwa wingi kwa vile tayari kuna soko la uhakika, na
tutahakikisha madalali hawatakuwepo ili mkulima asikandamizwe” alisema
Rais Magufuli.
Katika sekta ya uwekezaji nchini, India ni nchi ya tatu kwa uwekezaji Tanzania ikifuatiwa na Uingereza pamoja na China.
0 comments:
Post a Comment