MWILI wa aliyekuwa Kiongozi wa Jumuiya ya Freemason Tanzania na Afrika
Mashariki, Sir Jayantilal Keshavji Chande (89) ‘Andy’ Chande, umewasili
juzi kutoka jijini Nairobi nchini Kenya alipokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza na MTANZANIA mmoja wa wafanyakazi wa Sir Chande ambaye
hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema kiongozi huyo aliyefariki
juzi alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya tumbo.
“Mwili wake umeshawasili tangu jana (juzi) saa 2:30 usiku katika Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) na wamerudi wote
pamoja na familia yake yaani mkewe na watoto watatu waliokuwa
wakimuuguza,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alisema kwa sasa mwili huo umehifadhiwa katika Hospitali ya Aga Khan
jijini Dar es Salaam, ukisubiri maziko yatakayofanyika Jumanne ijayo.
Mbali na hilo pia alishangazwa na kusambaa kwa taarifa za kifo hicho kwa
haraka juzi kwa kuwa familia hadi jana mchana ilikuwa haijapata taarifa
rasmi.
“Mzee ni mtu mkubwa si Tanzania tu hata India, Marekani wote wameandika
habari zake baada ya kusikia katika mitandao, lakini bado watu
hawajaanza kuja kutoa pole, wengi wanapiga simu kuuliza tu kama ni kweli
sisi tumeshangaa taarifa hizi mmezitoa wapi wakati hakukuwa na mtu
aliyetoa habari kutoka katika familia jana,” alisema mfanyakazi huyo.
Alisema Sir Chande ambaye anatarajiwa kuchomwa Jumanne katika eneo la
Makumbusho, aliugua tumbo kwa kipindi cha wiki moja wakati ugonjwa wake
mkubwa uliokuwa ukimsumbua ulidaiwa kuwa ni shinikizo la damu.
Alisema vikao vya familia bado vinaendelea na kwamba wageni kutoka nchi
mbalimbali wanatarajiwa kuingia kuanzia Jumapili kuhudhuria mazishi
hayo.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jioni na msemaji wa
familia ya Sir Chande ambaye ni mtoto wake, maziko ya kiongozi huyo
yatafanyika Jumanne saa nne asubuhi katika makaburi ya Makumbusho jijini
Dar es Salaam.
“Taratibu za kuaga mwili wa Sir Chande zitafanya siku hiyo hiyo kuanzia saa 2.30 asubuhi nyumbani kwake,” ilieleza taarifa hiyo.
FAMILIA YAMWELEZEA
Katika taarifa, familia yake pia ilimwelezea Kiongozi huyo kama mtu
aliyekuwa na hekima ambapo mara nyingi alikuwa anaisaidia Serikali na
Watanzania na watu wengine duniani kote kwa kujihusisha na shughuli za
kijamii, uchumi na misaada ya kibinadamu.
“Katika kutambua hilo, Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza alimtunuku
medali ya heshima ya kuwa Commander of the Civil Division of the Most
Excellent Order of the British Empire (KBE),” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin
Mkapa, wakati akitoa maoni ya tuzo hiyo alisema anashangilia kushuhudia
Mtanzania aliyestahili kutunukiwa ‘Order of Knighthood in the British
Empire’.
Familia yake pia imesema Chande aliwahi kupewa tuzo ya heshima ya
Pravasi Bharatiya Samman kutoka kwa Rais wa India ambayo inatambulika
kwa kiasi kikubwa nchini India kama mwanachama wa Diaspora.
Mwaka 2004, Chande alichapisha hotuba zake pamoja na mafundisho na
habari kuhusu Freemason katika kitabu kinachoitwa Whither Directing Your
Course na mwaka 2011 alichapisha kitabu kingine cha Transitions of a
Life na kingine ‘A Knight in Africa: Journey From Bukene.
Vitabu vyake viligusa maeneo mbalimbali ikiwemo historia, biashara, mazingira, elimu na mambo ya kijamii.
Taarifa hiyo ya familia pia imeelezea namna Sir Chande alivyoshiriki katika harakati za ukombozi na uhuru nchini.
Inaelezwa uzalendo wa Sir Chande katika taifa kwa mara ya kwanza
ulijitokeza mwaka 1967 katika harakati za maazimio ya Arusha wakati wa
biashara ya familia yake, kiwanda cha Chande Industries Limited
kilitaifishwa kwa Serikali Februari 7, 1967.
Hayati Mwalimu Nyerere alimwalika Chande kusaidia kuanzishwa kwa
Shirikisho la viwanda vya kusaga na kuchakata (National Milling
companies).
Alikubali kwa uaminifu kuwa Mkurugenzi Mkuu wa National Milling
Corporation kwa miaka mitano, baada ya kustaafu alitumikia kama mshauri
wa Bodi ya Wakurugenzi.
Kati ya mwaka 1958 hadi 1961 kabla ya uhuru wa Tanzania, Sir Chande
inaelezwa alitumikia katika nafasi ya mwanachama wa Legislative Council
(LEGICO ).
Mwaka 1959, alipata nafasi ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na
Katibu Mkuu wa Serikali ya Uingereza, Ian McLeod, kuhusiana na
mapendekezo ya Uingereza kutoa uhuru wa kujitawala kwa Tanganyika.
Baada ya uhuru, Chande inaelezwa alishiriki katika shughuli mbalimbali nchini hasa za kijamii na kiuchumi.
Kwa nyakati tofauti aliwahi kuwa Mwenyekiti au kama mwanachama wa Bodi
ya Wakurugenzi wa makampuni kadhaa ya umma na binafsi ikiwa ni pamoja na
Benki ya Barclays Tanzania na Uganda na pia mashirika mbalimbali ya
Serikali ikiwa ni pamoja na Shirika la Reli la Afrika Mashariki na East
African Harbors Corporation.
Kufuatia kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, Sir
Chande, aliteuliwa kuwa mwanzilishi na Mwenyekiti wa Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL) na baadaye Mwenyekiti wa Mamlaka ya Bandari Tanzania na
wa Tanzania Railways Corporation.
Inaelezwa pia Chande alikuwa anajishughulisha na masuala ya kisiasa na
kidiplomasia, wakati mmoja aliwahi kuwa mshauri wa Wizara ya Kamati ya
Umoja wa Afrika ambayo inashughulikia masuala ya migogoro ya mafuta nchi
za Waarabu.
Nyumbani kwake Masaki
Mazingira ya nyumbani kwa Sir Chande, Masaki hayaonyeshi eneo hilo kama
kuna tukio lolote kubwa kutokana na ukimya uliokuwepo jana.
Mwandishi wa gazeti hili ambaye alifika nyumbani hapo mchana, alishuhudia wana ndugu wachache pamoja na watoto waliokuwa ndani.
Ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na waombolezaji wapatao watano waliokuwa
wakionekana sebuleni huku baadhi ya wana ndugu wakitajwa kuwa eneo la
juu la nyumba hiyo wakiendelea na kikao cha kupanga taratibu za mazishi.
Sir Chande alizaliwa Mei 7, mwaka 1928 nchini Mombasa, Kenya ameacha mjane Jayalaxmi na watoto watatu.
Hatua kwa hatua atakavyochomwa
Baada ya mwili wa marehemu kuingia ndani ya jengo lakuchomea maiti,
Wahindi huvunja nazi tatu katika kaburi lililo karibu kabisa na lango
kuu.
Baada ya hapo mwili huletwa katika tanuru lenyewe na hupangwa kuni juu
ya tanuru hilo ambalo limeundwa mithili ya kitanda cha chuma.
Kuni hupangwa kwa ustadi mkubwa na zile za ukubwa kiasi hupangwa katika
umbile la reli na magogo makubwa manne hupangwa kushoto, kulia Magharibi
na Mashariki ya tanuru hilo ambapo kuni zinakuwa nyingi.
Kabla ya kuchoma maiti
Kabla ya kuuweka mwili katika tanuru huuzungusha mara nne kulizunguka tanuru hilo.
Baada ya hapo, mwili wa marehemu ukiwa na sanda huwekwa katikati ya kuni hizo, kichwa kikielekezwa Magharibi.
Kabla ya uchomaji wenyewe kuanza, mila za Wahindu hutaka kuhakikisha iwapo kweli ndugu yao amefariki.
Ndugu mmoja wa marehemu hutakiwa kuhakiki kwa kuchukua kipande kidogo
cha kuni chembamba kilichoshika moto, kisha humchoma marehemu katika
unyayo mara nne huku akilizunguka tanuru.
Hatua inayofuata ni kuchukua moto kwa kutumia makoleo maalumu, kisha kuuchanganya moto huo na mafuta ya samli.
Mwili wa marehemu hupakwa mafuta ya samli kuanzia usoni mpaka miguuni
kabla ya kuwasha moto, baada ya hapo moto huwashwa na unakuwa moto mkali
zaidi ya gesi.
Mafuta ya samli pamoja na mafuta ya marehemu mwenyewe husaidia moto kuwa mkali kuliko kawaida.
Wakati moto unaendelea kuwaka kwa kasi, mbegu za ufuta hurushwa juu ya
mwili unaoendelea kuungua na ndugu za marehemu ambao wanakuwa
wamelizunguka tanuru.
Uchomaji mwili kawaida kuchukuwa saa mbili au mbili na nusu kumalizika au kuteketea kabisa.
Baada ya mwili kuungua na kwisha kabisa, kinachotakiwa kubaki ni vipande
vya mifupa, lakini wakati mwingine moto huweza kwisha kabisa na wakati
huo mwili bado haujamalizika.
Baada ya mwili kuchomwa na kwisha, ndugu mmoja wa marehemu huchukua
chungu maalumu kilichojazwa maji na kukiweka katikati ya miguu, kisha
anatakiwa kutazama Magharibi akiyapa kisogo mabaki ya mwili huo wakati
huo waombolezaji wote wanageuka pia.
Anachofanya ndugu huyo wa marehemu akiwa amesimama ni kuchukua jiwe na
kukipiga chungu hicho kwa nguvu hadi kivunjike na maji yamwagike
kuelekea lilipo tanuru.
Baada ya tukio hilo yeye pamoja na umati wote wa waombolezaji hutakiwa kuondoka bila kugeuka nyuma.
Kwa upande mwingine baada ya mwili kuchomwa na moto kumalizika kabisa,
mabaki ya mwili hutolewa kama vipande vya mifupa ya mwili na fuvu,
vilivyochanganyika na majivu na mkaa kutoka tanuruni.
Mifupa hiyo huwekwa katika mifuko maalumu na hatua ya mwisho ni ndugu kwenda kuyatupa baharini.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment