WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema uamuzi wa Serikali
kumnyang’anya mali zake likiwamo shamba la Mabwepande, Dar es Salaam ni
njama na hila za CCM kumdhoofisha kisiasa baada ya kuhamia Chadema.
Amesema Oktoba mwaka jana, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, chini ya Waziri William Lukuvi ilimnyang’anya
shamba kwa madai ya kulimiliki muda mrefu bila kuliendeleza.
Akizungumza juzi kwenye kongamano lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa
Chadema (BAVICHA), mkoa wa Geita kujadili hali ya demokrasia nchini,
Sumaye alisema hata wakimnyang’anya mali wasitarajie kuwa atafilisika na
kamwe hatarudi CCM.
Sumaye aliyekuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo, alisema licha ya
kunyang’anywa shamba hilo, ataendelea kuishi na maisha yake
hayatabadilika na akaahidi kupambana usiku na mchana kuhakikisha CCM
inaondoka madarakani.
“Mimi walininyang’anya shamba langu, nikawaambia nyang’anyeni, mimi
ndiyo sasa naingia kwenye mapambano sawasawa,” alisema Sumaye na
kuongeza:
“Wako marafiki zangu kule CCM wakahoji kwa nini nisirudi CCM badala ya
kuteseka kiasi hicho. Na mimi jibu nililowaambia ni moja tu, nimetoka
CCM kazi yangu iliyobaki ni kuiondoa CCM madarakani na si kurudi CCM.”
Alifafanua kuwa mateso wanayopata wananchi ndiyo wanayopata viongozi wa
juu wa Chadema ambao baadhi yao wameanza kuteswa kwa kunyang’anywa mali
zao akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyenyang’anywa nyumba
anayoimiliki kwa asilimia 75.
Alisema licha ya Mbowe kunyang’anywa nyumba hiyo ambayo hakuitaja,
alisema Serikali ina mpango wa kumpora pia shamba analolima kilimo cha
kisasa.
Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, Sumaye ambaye ni mjumbe wa Mkutano
Mkuu wa Chadema Taifa, alisema uamuzi wa Rais John Magufuli kuzuia vyama
vya upinzani kufanya mikutano kwa wananchi, ni kinyume na Katiba ya
Tanzania na haijawahi kutokea hali hiyo tangu vyama vingi
vilipoanzishwa.
Alisema kwa katazo hilo, hakuna mtu atakayeanzisha chama cha siasa kwani
kuanzisha chama lazima ifanyike mikutano ya hadhara kutafuta wananchi,
lakini kwa hali hiyo hakutakuwa na usajili wa vyama.
“Hata Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mtungi anajua hilo kwamba
demokrasia imekandamizwa. Nasi hatuogopi kumwambia Rais ambayo si ya
kufanya kwani hana ruhusa ya kuvunja Katiba kwani aliapa kuilinda na
kuitetea,” alisema Sumaye.
Aidha, alisema kama hali itaendelea hivyo pamoja na hali ngumu ya maisha
ya Watanzania njia itakuwa nyeupe ya Chadema kuingia madarakani, na
hivyo aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele kuipinga Serikali na kutetea
demokrasia.
Baadhi ya wananchi walisema hali ya maisha ni ngumu na imefikia hatua ya
wanaume kutelekeza familia zao kwa kushindwa kuzihudumia.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) jimbo la Geita, Mary Paschal
alisema kuna familia zimetelekezwa na wanaume kwa sababu ya maisha
magumu.
“Akina mama wengi tumekuwa wahanga wa maisha magumu, wanawake
tunahangaika sana kwani akina mama tunapoomba matumizi wanaume
wanachukua suruali na kuondoka bila kuaga,” alisema Mary.
Awali Mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa wa Geita, Neema Chozaile alisema lengo
la kongamano hilo ni kujadili hali ya demokrasia nchini ambapo alisema
demokrasia inataka kupotezwa kwa kunyimwa uhuru wa habari, kujieleza na
kutoa maoni.
Alisema Serikali iliyopo ni ya kwanza kujitokeza kubinya demokrasia
nchini kwa kunyima uhuru hasa wa vyama vya siasa kujieleza kwa wananchi.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment