Rais
Magufuli ameipongeza ofisi ya Bunge kwa kubana matumizi na kufanikiwa
kuokoa shilingi Bilioni 6, ambazo zitatumika kutengeneza madawati ya
wanafunzi wa shule na amezitaka ofisi na taasisi nyingine za serikali
kuiga mfano huo.
Ameagiza
fedha hizo zipelekwe Idara ya Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
ili vyombo hivyo vifanye kazi ya kutengeneza madawati yanayotarajiwa
kuwa zaidi ya 120,000 ambayo yatasambazwa katika shule ili kukabiliana
na tatizo la wanafunzi wanaokaa chini kwa kukosa madawati.
Hundi
Kifani ya fedha hizo imekabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais na Naibu Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Akson, ambaye
amesema Ofisi ya Bunge imetekeleza wito wa serikali wa kubana matumizi
ambapo kiasi hicho cha shilingi Bilioni 6 kimepatikana kwa kipindi
kifupi cha takribani nusu mwaka.
Katibu
wa Bunge Dkt. Thomas Kashilila ametaja maeneo ambayo Bunge limebana
matumizi kuwa ni Safari za nje ya nchi, Mafunzo nje ya nchi, Machapisho
na ununuzi wa majarida, Shajala, Chakula na Viburudisho, Mtandao, Malazi
hotelini, Matibabu ya wabunge na familia zao nje ya nchi, Umeme, Maji,
Simu na Uendeshaji wa Mitambo.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pia
ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Anne Kilango Malecela
na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Abdul Rashid Dachi, kufuatia mkoa huo
kutoa taarifa zisizo sahihi kuwa hauna watumishi hewa.
Rais
Magufuli ametangaza kutengua uteuzi wa Viongozi hao wa Mkoa wa
Shinyanga leo tarehe 11 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam, mara
baada ya kupokea Taarifa ya Mwaka 2014/2015 ya Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na kupokea hundi kifani ya shilingi
Bilioni 6 kutoka Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
zilizotokana na kubana matumizi.
Dkt.
Magufuli ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa kuwa Mkoa wa Shinyanga
hauna watumishi hewa, aliamua kutuma timu ya ukaguzi iliyokwenda kufanya
uchunguzi ambapo hadi kufikia jana tarehe 10 Aprili, 2016 imebaini
kuwepo watumishi hewa 45 huku zoezi likiwa linaendelea katika wilaya
mbili za Ushetu na Shinyanga Vijijini.
“Na
wale wote wa Shinyanga ambao walisemekana ni zero, hakuna mtumishi
hewa, walikuwa tayari wameshalipwa shilingi milioni 339.9, nimejiuliza
sana, na nikajiuliza sana na kwa kweli nimejiuliza sana na kwa
masikitiko makubwa, kwa nini Mkuu wa Mkoa alisema hakuna mtumishi hewa?” Amesisitiza Rais Magufuli
Rais Magufuli amesema baada ya kutengua uteuzi wake, Anne Kilango Malecela atapangiwa kazi nyingine.
Pamoja
na hatua hiyo, Dkt. Magufuli ametaka wakuu wa mikoa yote wawafichue
watumishi hewa wote ili waondolewe mara moja, na ameagiza timu
iliyofanya uchunguzi Mkoani Shinyanga itumike kufanya uchunguzi katika
mikoa mingine kwa lengo la kukomesha upotevu mkubwa wa fedha za umma.
Katikati
ya Mwezi Machi, 2016 Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa yote
nchini kusimamia zoezi la kuwaondoa watumishi hewa wote katika orodha ya
malipo ya mshahara, ambapo mpaka tarehe 31 Machi, 2016 Jumla watumishi
hewa 5,507 walibanika.
Kati
ya shilingi Bilioni 583 ambazo serikali imekuwa ikitumia kila mwezi kwa
ajili kulipa mishahara, kati ya shilingi Bilioni 53 na 54 zimekuwa
zikipotea kutokana na kulipa mishahara ya watumishi hewa.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam-11 Aprili, 2016
0 comments:
Post a Comment