Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO, Dodoma.
Serikali itaendelea
kusimamia haki ya mtoto wa kike ya kupata elimu na kuwachukulia hatua kali za
kisheria ikiwemo kuwapeleka mahakamani wale wote wanaowapata ujauzito wanafunzi
na kuwakosesha kupata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.
Kauli hiyo imetolewa
na Naibu Waziri Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Seriklali za Mitaa (TAMISEMI)
Seleman Jafo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Janeth Mbene wa Ileje baada
ya kujibu swali la msingi lililohoji kuhusu kushuka kwa kiwango cha elimu
nchini.
“Serikali haitamvumilia
mwanaume yeyote atakayempa ujauzito mwananfunzi na kukwamisha kupata elimu kwa
wakati na kumharibia malengo ya maisha yake” alisema Naibu Waziri Jafo.Hatua hiyo ya
Serikali itawahakikishia na kuwawezesha watoto wa kike nchini kusoma na
kumaliza masomo yao hatua ambayo itakuwa msaada kwa watoto hao wa kike, familia
zao na taifa kwa ujumla.
Akisistiza msimamo wa
Serikali kuhusu wanaume wanaowapa ujauzito wanafunzi, Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alisema kuwa Serikali haipo
tayari kuwavumilia wanaume wenye tabia ya kuwakwamisha watoto wa kike kupata elimu
kwa kuwapa ujauzito na itahakikisha sheria inachukua mkondo wake ili kukomesha
tabia hiyo.
Akizungumzia tatizo hilo
la wanafunzi kupata ujauzito wakiwa shuleni, Mbunge wa Jimbo la Igunga Seif
Khamis Gulamali alisema kuwa tatizo hilo lipo sehemu mbalimbali nchini ambapo
watoto hubebeshwa mimba wakiwa katika umri mdogo wa kuwa shuleni na tatizo hilo
linaendelea kuleta hasara kubwa kwa wanafunzi wenyewe, familia zao na taifa kwa
ujumla.
Gulamali alisema kuwa
hali hiyo inatokana na hulka ya makabila mengi nchini hasa ya wafugaji hali
inayosababishwa na tabia ya kuhama hama kutafuta malisho na maji kwa ajili ya
mifugo yao.“Wapo wazazi
wanaowapa maelekezo watoto wao wasifaulu mitihani yao ili waweze kuolewa na
wamegeuzwa kuwa sehemu ya kipato cha familia zao kwa kupata mahari” alisema
Gulamali.
Ili kukomesha tabia
hiyo ya kuwapa ujauzito watoto wenye umri mdogo hasa kwa wafugaji, Gulamali
alisema kuwa ipo haja ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
pamoja na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuweka mazingira mazuri ambayo yatawapa
wananchi wengi fursa ya kuwekeza kwenye
sekta ya kilimo na mifugo kwa kuwahakikishia upatikanaji wa maji kwa wingi ili
wananchi wazalishe na kuondokana na tabia ya kuhama hama kwa wazazi wao ambayo
imekuwa kikwazo kikubwa kwa watoto kupata elimu.
Kuhusu shilingi
milioni 50 zilizoahidiwa na Serikali kwa kila kijiji hapa nchini, Gulamali
alisema kuwa ni vema ufikiriwe mfumo wa kupeleka hizo fedha ambao utakuwa wa
tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla utakaohkikisha fedha hizo zitakuwa
endelevu na kuwarahisishia wananchi kazi na kuongeza uzalishaji wa mazao yatakayowaongezea
kipato.
Hatua hiyo itasaidia
taifa kuwa na matumizi bora ya rasilimali fedha zinazotolewa na Serikali kwa
kuwekeza kwenye sekta za viwanda, mifugo, uvuvi na kilimo ambapo Tanzania kuna
mvua ya kutosha, mabonde yenye rutuba, mito, maziwa, bahari pamoja na watu
ambao ndio msingi wa maendeleo kwa taifa kwa kuongozwa na Dira ya Maendeleo ya
Taifa ifikapo 2025 Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati.
0 comments:
Post a Comment