WATU
watatu wamekufa baada ya kufukiwa na mizigo wakati lori walilokuwa
wamepanda kutoka Mnada wa Mgaga wilayani Bahi mkoani Dodoma, kupasuka
tairi na kupinduka.
Ajali
hiyo iliyotokea katika Kijiji cha Chifutuka saa 11 jioni juzi, pia
ilisababisha majeruhi 19 ambao wamekimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma
kwa matibabu.
Akithibitisha
kutokea kwa ajali hiyo, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani
hapa, Mayala Towo alilitaja lori lililohusika kuwa ni aina ya Mitsubishi
Fuso lenye namba za usajili T 689 BEG.
Alisema lori hilo lilipofika eneo la Chifutuka wilayani Bahi, tairi lake la mbele lilichomoka na kupinduka.
“Gari
hilo lilichomoka tairi ya mbele na kusababisha kupinduka kisha mizigo
kuwaangukiwa watu waliokuwepo katika lori hilo ambapo watu watatu
wamekufa na majeruhi 19 walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa,” alisema Towo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Dodoma, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Zainabu Chaula alisema
juzi saa mbili usiku walipokea majeruhi 19 na maiti watatu.
Dk
Chaula alitaja waliokufa kuwa ni Isdori Thomas Motto (38), Michael
Msongela (29) na Elias Masimo Petro (51) wote wakazi wa Dodoma.
Daktari
huyo alisema majeruhi 12 walitibiwa na kuruhusiwa huku wengine
wakilazwa wodi namba 10, 8 na 11 kwa ajili ya uangalizi zaidi.
Aliwataja
waliolazwa kuwa ni Muoni Magege (40) mkazi wa Dar es Salaam, Suzy,
Samweli (16), Frida Chipaga, Chausiku Mohammed (38), Josephine Sakiru
(43), Selemani Salum (35) na Elias Petro (51) wote wakazi wa Dodoma.
Akisimulia
ajali hiyo, mmoja wa majeruhi ambaye amelazwa katika Wodi Namba 8,
Chausiku Mohammed mkazi wa Chinangali mjini Dodoma, alisema walipanda
lori hilo lililokuwa likitoka mnadani na kwamba alichokiona ni kuchomoka
kwa tairi la lori hilo, hivyo gari kupinduka na wao kufunikwa na mizigo
iliyokuwepo katika lori hilo.
“Mimi
nilienda mnadani kwa ajili ya kununua mazao, kama unavyojua malori ya
minadani yanabeba kila kitu hadi mizigo sasa sisi kilichotuumiza ni
mizigo kwani ilitulalia na mimi kama unavyoona nimeumia huu upande wote
wa kulia na hapa katika mkono wangu,” alisema Chausiku.
Seleman
Salum aliyelazwa Wodi Namba 11 mkazi wa Uwanja wa Ndege, alisema ajali
hiyo ilisababishwa na kuchomoka kwa tairi la mbele na kupinduka. Alisema
ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11 jioni karibu na Kijiji cha
Chifutuka wilayani Bahi.
0 comments:
Post a Comment