MKUU wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu amefunguka kuhusu mambo juu ya utendaji wa jeshi hilo na kueleza kuwa wakati wowote litamburuza mahakamani Katibu Mkuu wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuhamasisha uchochezi visiwani Zanzibar.
Amebainisha kuwa jeshi hilo, kamwe halikandamizi wala kuonea chama chochote cha siasa, kwani limekuwa likitekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.
Akizungumza
katika mahojiano yaliyofanyika kwenye kipindi cha Funguka,
kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Azam jana, IGP Mangu alisema
hali ya siasa Zanzibar ilikuwa shwari katika chaguzi zote mbili na
kwamba machafuko na vurugu vilianza kutokea baada ya uchaguzi wa pili.
Alisema
vurugu hizo zilianza baada ya kubainika kuwa Maalim Seif, alikuwa
akifanya mikutano ya ndani na mingine ya chini kwa chini na wafuasi wake
katika maeneo ya Kaskazini na Kusini.
“Kwa
sababu ilikuwa ni mikutano ya ndani, Polisi hatukuona tatizo na wala
hatukumzuia, tuliona ni mwananchi anataka kuzungumza na wafuasi wake,
tukasema mwache aongee nao tu,” alisema IGP Mangu.
Alisema
baadaye jeshi hilo liligundua kuwa kiongozi huyo wa CUF, alikuwa
anawachochea wananchi waichukie serikali iliyopo madarakani na wapinzani
wao ambao ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwafanyia uhalifu.
Alisema
baada ya vikao hivyo vya Maalim Seif, visiwani humo kukaanza kuibuka
matukio ya vurugu kama vile mashamba kuchomwa moto na mazao kung’olewa.
“Haya mambo hayakutokea kabla ya vikao vya Seif, yalitokea baada ya vikao vyake,” alifafanua mkuu wa polisi.
Alisema
wafuasi hao walichochewa, kiasi cha kususa hadi shughuli za kijamii,
kama vile misiba na wakati mwingine ilifikia hatua ya kususa kuwauzia
bidhaa wafuasi wa CCM.
“Tukasema
kama wameona kugeuza biashara zao siasa, basi waendelee tu. Biashara
inadumu kwa sababu unatengeneza faida, sasa kama umeamua kuchagua wa
kumuuzia ni shauri yako. Hawa tuliwaacha kwa sababu tuliona hawana
makosa,” alisema.
Hata
hivyo, alisema jeshi hilo kamwe halikuwanyamazia wahalifu waliochoma na
kung’oa mazao kwenye mashamba ya wenzao, eti tu kwa kigezo cha ufuasi
wa chama au siasa.
“Hawa
tuliwakamata na wapo wengine tunaendelea kuwatafuta, watakapoacha ndio
hatutawatafuta. Wale wahalifu ndio tunaowatafuta. Pengine kwa sababu ya
siasa wanadhani Polisi tunawaonea wananchi tunawakamata bila sababu.
Sasa hawa watu tunawaoneaje wakati tunawapeleka mahakamani?” Alihoji.
Maalim Seif kuhojiwa
Alisema
kutokana na matukio hayo, tayari Maalim Seif amehojiwa na jalada lake
halijaamuliwa, lipo kwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) Zanzibar. “Lakini pia tunataka tumpeleke mahakamani kumshitaki kwa makosa aliyofanya ya kuchochea fujo,” alieleza.
Alisema
kazi kubwa ya Polisi kwa sasa si kujiingiza kwenye siasa au kupatanisha
pande mbili zinapokwaruzana, bali kazi yake ni kuhakikisha inadhibiti
na kuwakamata wahalifu.
Alisema
endapo vyama viwili vinavyolumbana visiwani Zanzibar, vitaamua kuchukua
hatua za kisheria kumaliza tofauti zao, polisi haina tatizo, lakini
endapo vyama hivyo vitachukua hatua za kijinai au kukomoana, jeshi hilo
halitokaa kimya.
“Kazi ya polisi iko wazi, tunakamata tunapeleleza na kupeleka mahakamani umma unatuona tunachofanya hatuna cha kuficha,” alisisitiza.
Maandamano na mikutano
Akizungumzia
madai ya jeshi hilo kukandamiza demokrasia na wapinzani kwa kudhibiti
shughuli za siasa nchini, IGP Mangu alisema hakuna mwanasiasa au chama
chochote, kilichozuiwa kufanya shughuli zake, ikiwemo mikutano.
Alisema
kinachotakiwa ni kwa mwanasiasa au chama hicho, kupeleka maombi yake
Polisi kwa mujibu wa sheria na baada ya jeshi hilo kufanyia tathmini
maombi hayo, endapo yataonekana hayana tatizo yataruhusiwa kuendelea.
Alisema
endapo jeshi hilo linazuia shughuli za kisiasa, hutokana na uchunguzi
au tathmini lililofanya na kujiridhisha kuwa shughuli husika si salama
na inatishia usalama wa raia.
“Unajua
unapozungumzia masuala hayo tuwe makini kidogo, kwa sababu hapa kuna
watu wa aina mbili kuna wanaofanya siasa na sisi watendaji tunaotekeleza
sheria. Ila sisi pia hatuko juu ya sheria, kama kuna mahali tunakiuka
upo utaratibu wa kutushughulikia,” alisisitiza.
Alisema
hata katika suala la kuzuia shughuli za kisiasa, kama vile mikutano na
maandamano endapo, kuna chama au mwanasiasa anahisi kuwa jeshi hilo,
halikutenda haki au limeenda nje ya mstari, taratibu zinamruhusu kukata
rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu,
Rais na Mahakama.
Hata hivyo, alisema jeshi hilo halifanyi jambo lolote nje utaratibu wa kisheria, akifafanua, “lakini
sisi hatuwezi kujiingiza kwenye siasa kwa sababu sisi sio wanasiasa,
pia hatuwezi kuzuia wanasiasa kulumbana kwa sababu ni uwanja wao wa
kulumbana. Sasa kama tulitoa maelekezo fulani basi ujue tulikuwa
tunatekeleza sheria na utaratibu uliopo.”
“Sidhani
kama sisi tunakandamiza upinzani, tunachofanya sisi ni kufuata sheria
na taratibu zilizowekwa na watu wako huru kama wanafikiri tumeenda nje
ya mipaka yetu wakatuchukulie hatua,” alisisitiza.
Alitoa
mfano wa matukio yaliyozuiwa na Polisi kwa sababu za kiusalama kuwa ni
pamoja na mkutano wa mahafali wa Dodoma, ambao ulifanyika siku moja na
mkutano wa mahafali uliofanyika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam ambao
wenyewe haukuzuiwa. Yote ilikuwa mikutano ya wanafunzi wafuasi wa
Chadema.
“Kama
sisi tuna sera ya kuzuia, mbona wa Karimjee hatukuuzuia? Dodoma
kulikuwa na sababu na imeelezwa na viongozi wa Dodoma. Hii si sera yetu,
usichukulie mkutano mmoja kuzuiwa basi ndio yote nchi nzima imezuiliwa.
Haiwezekani,” alifafanua.
Alisema
sheria inazungumzia wanaohitaji kufanya mkutano au kufanya maandamano,
wanatoa taarifa kwa mkuu wa polisi wa hilo eneo, na mkuu huyo ataangalia
kama mazingira yanaonesha hakuna tatizo, mkutano utaendelea, kama kuna
tatizo atauzuia.
“Sasa
ni wapi sisi tumefanya kitu ambacho ni kinyume na tunaonekana
tunakandamiza upinzani? Na ikumbukwe kuwa kuna mikutano baadhi iliombwa
tukaizuia kwa sababu kipindi hicho kulikuwa na kelele za mauaji Mwanza,
Sengerema, Tanga mpaka tunahojiwa Polisi mko wapi,” alisema.
Alisema wakati Polisi ikihojiwa kuhusu dawa ya mauaji, baadhi ya vyama viliwasilisha maombi ya maandamano.
“Hivi
kweli? Kwanza mauaji yenyewe mtindo wake ni mpya unajuaje kama
wanaoomba wangeenda nao kuvamiwa? Lazima tuchukue tahadhari,” alisema na kuongeza kuwa Polisi imepewa jukumu la kisheria kuhakikisha panakuwepo na amani.
“Sasa tunapochukua hatua kuhakikisha kuna amani, naomba tuvumiliane. Msione kuna amani, basi mkajua ipo tu na ni ya kudumu, mjue kuna wengine wameumia kuhakikisha hiyo amani inakuwepo. Lazima iwe hivyo ndio utaratibu wa kuongoza nchi, sisi hatubagui wala kukandamiza chama chochote,” alieleza IGP Mangu.
“Sasa tunapochukua hatua kuhakikisha kuna amani, naomba tuvumiliane. Msione kuna amani, basi mkajua ipo tu na ni ya kudumu, mjue kuna wengine wameumia kuhakikisha hiyo amani inakuwepo. Lazima iwe hivyo ndio utaratibu wa kuongoza nchi, sisi hatubagui wala kukandamiza chama chochote,” alieleza IGP Mangu.
Matumizi ya nguvu
IGP
Mangu alisema si kweli jeshi hilo limekuwa likitumia zaidi nguvu katika
kudhibiti vurugu na kubainisha kuwa nguvu hutumika, pale tu
inapobainika kuwa upande wa pili unaodhibitiwa nao unatumia nguvu.
Hata
hivyo, alisisitiza kuwa Polisi nchini imekuwa ikitekeleza wajibu wake
vyema bila kukandamiza wala kutumia nguvu, kwani hata taasisi ya
kimataifa iliyofanya tathmini juu ya utendaji wa jeshi hilo katika
uchaguzi mkuu nchini ilibainisha kuwa jeshi hilo lilifanya vyema.
Polisi na rushwa
Akizungumzia
tuhuma zinazorushiwa Jeshi la Polisi kwamba kuna baadhi ya askari wake,
wanatuhumiwa kwa rushwa, alisema askari hawana mamlaka ya kula rushwa
na kujilimbikizia mali halafu wasiguswe na mtu.
“Hili
haliwezekani. Kwa hiyo nasema bado wananchi wanaweza wakasaidia kama
kweli wanazo taarifa za Polisi na zitafanyiwa kazi. Kama hawaamini kama
sisi wenyewe hatuwezi kudhibitiana, vipo vyombo vingine vinaweza kufanya
hivyo,” alisema.
Hata
hivyo, alisema wapo askari Polisi wenye maisha mzuri kwa maana ya
nyumba na magari, ambao wamepata mali hizo kupitia taasisi mbalimbali za
mikopo ikiwemo Saccos ya Polisi, ambayo ndio kubwa nchini.
“Askari
polisi kumiliki gari nzuri si kosa, la msingi amepataje hilo gari, kama
kuna polisi ana mali au gari isiyo na maelezo tuleeteni, polisi
hazuiliwi kuwa na gari nzuri. Siku hizi kuna taasisi nyingi zinakopesha
anaweza kukopa,” alisisitiza.
Kashfa ya Lugumi
Akizungumzia
suala la kashfa ya mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd
inayomilikiwa na mfanyabiashara Said Lugumi, IGP Mangu alisema suala
hilo lilichukuliwa na Bunge na kufanyiwa uchunguzi hivyo, matokeo ya
uchunguzi hawezi kuyazungumzia.
Alisema
anachoweza kukizungumzia ni maelekezo ambayo jeshi hilo limepatiwa na
Bunge, ambayo ni kukamilisha yale ambayo hayajakamilishwa.
“Tunaendelea
kuchukua hatua za kukamilisha.Kuhusu uchunguzi kazi ilifanywa na Bunge
kwa anayetaka anaweza kuwasiliana na Bunge na kupatiwa matokeo kwa kuwa
naamini Bunge linawakilisha wananchi, taarifa zao ziko wazi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment