WATU
watakaogundulika kuwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wataanza kupewa na
kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa (ARVs) bila kusubiri kinga
zao za mwili kupungua kama ilivyozoeleka.
Wakati
utaratibu huo mpya ukitarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu, kwa upande
wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi kupitia kwa
Mwenyekiti wake, Constantine Kanyasu, imeshauri serikali kuangalia namna
ya kuruhusu dawa ziingizwe na kuuzwa madukani kwa bei nafuu kwa ajili
ya watu ambao hawako chini ya mpango wa serikali.
Hayo
yalielezwa jana mjini Dodoma kwenye kikao cha kamati hiyo ya Bunge
ambayo ilipokea taarifa iliyofikiwa katika utafiti wa upatikanaji wa
chanjo ya Ukimwi.
Katibu
Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk
Mpoki Ulusubisya aliieleza kamati juu ya mabadiliko katika tiba na
kusema mtu yeyote anayepima na kugundulika kuwa ana Virusi Vya Ukimwi,
ataanza kupatiwa ARVs mara moja.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hii, Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi,
Dk Angela Ramadhani, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) yaliyotolewa mwaka jana baada
ya tafiti kubainisha kuwa zipo faida za kuwahi kupata dawa husika.
Dk
Ramadhani alisema maagizo hayo ya WHO yanatokana na tafiti
zilizofanyika katika nchi mbalimbali na kubainisha kuwa kutumia ARVs
kabla ya kinga ya mwili kushuka, kuna faida kutokana na kuonesha kuwa
kunakuwa na usalama zaidi.
Kwa
mujibu wa Dk Ramadhani, baada ya mwongozo kutolewa mwaka jana, Aprili
mwaka huu, shirika hilo liliita nchi wanachama na kusambaza taarifa hizo
kwa ajili ya kuziwezesha kujipanga kiutekelezaji.
“WHO wakishatoa mwongozo, huita wataalamu na kuwaeleza ili nchi zijiendae. Kwa mfano, kama zina uwezo wa kutoa dawa hizo,”
alisema Dk Ramadhani na kusema pia hapa nchini, wameanza wiki hii
kupitia miongozo ya zamani kabla ya utaratibu huo mpya kuanza Oktoba
mwaka huu.
Wakati
huo huo, wakati wa kikao na Kamati ya Bunge baada ya wizara kuonesha
kuwa uwezo wa serikali wa kutoa dawa hizo unaishia kwa watu milioni 1.3
licha ya kuwa na watu 2.4 wenye VVU, Mwenyekiti wa Kamati, Kanyasu
alishauri suala hilo liangaliwe kwa umakini.
“Kama
uwezo wa serikali unaishia kwa watu milioni 1.3, ni kwa nini serikali
isijikite hawa wanaopata free (bure) halafu hawa private (binafsi)
wakaruhusiwa kuingiza dawa zikauzwa kwenye maduka kwa bei nafuu ili mtu
akishajiona ana Ukimwi aende akanunue ili kuziba pengo hilo la watu
milioni 2.4,” alihoji Kanyasu wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Katika
kikao hicho cha kamati na watendaji kutoka wizara, taarifa
zilibainishwa kwamba wafadhili wamepunguza na wanaendelea kupunguza
bajeti katika masuala ya Ukimwi.
Kuhusu
chanjo, ilielezwa na Katibu Mkuu kwamba, shughuli zote zilizopangwa
awali kuhusu chanjo zilisitishwa Juni, 2015 baada ya fedha kutoka kwa
wafadhili kwisha jambo ambalo serikali imechagizwa kutoa fedha uendelee.
Ilisisitizwa
kwamba Tanzania inapaswa ijikite kwenye chanjo ikizingatiwa kwamba
haiwezi kutegemea tafiti za mataifa mengine kutokana na wadudu
kutofautiana.
Wakati
huo huo, kamati ilielezwa changamoto zilizopo kwenye utafiti juu ya
suala la Ukimwi kwamba Watanzania wengi wanaogopa kuwekewa vimelea vya
kupambana na Ukimwi wakidhani wakipandikiziwa watakuwa wameambukizwa.
Katibu Mkuu alisema hali hiyo inasababisha watafiti kupata shida ya
kupata watu wa kufanyia utafiti.
Awali,
katika taarifa yake kuhusu utafiti wa chanjo ya Ukimwi, Katibu Mkuu
alisema wizara yake kupitia Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili na Taasisi ya
Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Kituo cha Mbeya
zilifanya utafiti mwaka 2014.
Alisema
kati ya Februari 2007 na Februari 2008, watu 162 miongoni mwa 177
walifanyiwa uchunguzi na chanjo kuonesha usalama mzuri na hakukuwa na
madhara makubwa yanayohusiana moja kwa moja na chanjo.
Aidha,
asilimia 100 ya washiriki waliopata chanjo halisi waliweza kutengeneza
kinga zinazohusisha seli za kinga ya mwili na protini zilizoko kwenye
damu dhidi ya VVU. Kutokana na mafanikio ya awamu ya kwanza, mradi wa
awamu ya pili ulifanyika Tanzania na Msumbiji.
0 comments:
Post a Comment