SERIKALI
imeanza kuwashughulikia watumishi walionufaika na fedha za watumishi
hewa ambapo hadi sasa watumishi 839 wapo katika hatua mbalimbali
wakiwemo waliofikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) na wengine wanaendelea kuhojiwa polisi kwa ajili ya
kufikishwa mahakamani.
Sambamba
na hilo, serikali inatarajia kutoa ajira mpya 71,496 kwa mwaka huu wa
fedha baada ya kukamilisha uondoaji wa wafanyakazi hewa.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angella Kairuki
aliyasema hayo wakati akizungumzia utekelezaji wa mipango na mikakati ya
wizara yake katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachorushwa na Shirika
la Utangazaji Tanzania (TBC1). Kairuki alisema,
“Kwa
sasa tayari wapo watumishi wameshahojiwa na kuchukuliwa maelezo yao
polisi na upelelezi utakapokamilika watachukuliwa hatua mbalimbali za
kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani… Tunakamilisha ushahidi na
tutawatangazia tutakapokamilisha,” alisema.
Alisema
waligundua kwamba kuna maofisa utumishi na wahasibu ambao siyo
waaminifu, badala yake walikuwa wakielekeza fedha kwa ndugu zao na
miradi yao na wengine walishastaafu lakini bado majina yao yalikuwa
yakiendelea kupokea mishahara wakati walitakiwa kuondolewa kwenye mfumo.
Alisema
kwa kipindi cha Machi mosi hadi Agosti 20 mwaka huu, watumishi hewa
waliogundulika ni zaidi ya 16,127 na kuisababishia serikali hasara ya
mabilioni ya fedha. Kwa kipindi cha Agosti pekee watumishi hao hewa
wangelipwa mishahara wangeisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh
bilioni 16.
“Uhakiki
huu ni endelevu na tumegundua changamoto kubwa katika usimamizi wa
mishahara ni uadilifu kwa watu waliokasimiwa madaraka. Maofisa Utumishi,
Maofisa Utawala na Wahasibu wamepewa madaraka lakini wengi wao siyo
waaminifu, hivyo kwa sasa tumeweka uwajibikaji kwa waajiri,” alisema.
Aidha
alisema wanaufanyia mfumo wao maboresho zaidi ili uweze kuchakata
taarifa nyingi zaidi ambapo pia sekta ya mishahara imeshushwa katika
ngazi za chini zaidi hasa katika sekta za elimu na afya ambazo zimekutwa
na watumishi hewa wengi zaidi ili waweze kuwa na taarifa za mtumishi
mmoja mmoja.
Alisema
upo muongozo ambao fedha za serikali zinaporejeshwa zinapitia hazina na
kusisitiza kwamba wataendelea kuhakikisha wanasimamia fedha zote ambazo
zilichukuliwa serikalini kinyume na utaratibu na isivyo halali
zinarudishwa kwa mfumo sahihi.
Pia
alisema wameongeza kasi ili kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya kazi na
uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hivyo wanaanda mkataba wa utendaji
kazi kwa watumishi wa umma na ikiwezekana utaanza kutumika mwaka ujao wa
fedha.
Alisema
serikali imefanya maboresho makubwa katika mishahara na motisha kwa
ajili ya maslahi ya watumishi wa umma, sambamba na kuhimiza taasisi
mbalimbali kuweka vitendea kazi ili kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza
majukumu yao ipasavyo.
Akizungumzia
ajira hizo mpya Kairuki aliwatoa hofu watanzania waliokuwa wanatarajia
ajira serikalini na kusisitiza kwamba walichokuwa wanasubiri ni takwimu
halisi kwa taasisi ili kujua ni watumishi wangapi wameondolewa.
“Baada
ya kukamilisha mchakato huo, hatua nyingine zitaendelea… Hii ni neema
kwa waliomaliza vyuo, cha msingi wavute subira maana tutatoa ajira
71,496 kwa mwaka huu wa fedha na hatukuzifuta ajira.
"Nawashauri vijana wasijiingize kwenye makundi yasiyofaa wasubiri ajira zinakuja,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Kairuki alisema, wamepokea malalamiko zaidi ya 200
kutokana na ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa Utumishi wa
Umma ambayo inamnyima mtumishi kutotumia madaraka yake vibaya.
“Katika
malalamiko hayo 142 yanahusu sheria ya maadili. Sekretarieti ya Maadili
imefanya uchunguzi wa awali na malalamiko 12 yataanza kufikishwa Baraza
la Maadili na hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa ikiwemo kushushwa
vyeo au kuachishwa kazi,” alisema.
Pia
aliwaagiza maofisa utumishi kuwahudumia watumishi na kuwapa haki zao
ikiwemo kuwapandisha madaraja kwa wakati pale wanapostahili. Aidha
Kairuki alikemea tabia ya baadhi ya watu kughushi taarifa za utumishi wa
umma na kusisitiza kwamba jambo hilo ni kosa kubwa kwa yeyote
anayefanya hivyo.
“Mtu
yeyote ambaye anatoa nyaraka za serikali na siyo mlengwa au anayetoa
nyaraka ambayo imewekewa zuio kwa mujibu wa sheria ni kosa la jinai na
hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Tunawasisitiza
watumishi wa umma kuhakikisha wanazingatia sheria hizo na mwongozo wa
utoaji nyaraka na kumbukumbu za taarifa za serikali,” alisema.
0 comments:
Post a Comment