Mtandao wa Watetezi wa Waki za Binadamu (THRDC) kwa niaba ya wanachama
wake tunalani vikali maujai ya askari wa jeshi la polisi huku
tukisisitiza kwamba askari wa jeshi la polisi wanaofanya kazi katika
misingi na sheria ni watetezi wa haki za binadamu kama walivyo watetezi
wengine.
Kutokana na taarifa rasmi ya jeshi la polisi ni kwamba
mnamo tarehe 23/08/2016 saa moja usiku maeneo ya Mbagala Mbande kata ya
Mbande Temeke, majambazi ambao idadi yao haikuweza kufahamika wakiwa na
silaha za moto walivamia benki ya CRDB tawi la Mbande ambapo
waliwashambulia na kuwaua askari wanne wa Jeshi la Polisi waliokuwa
kazini na kuwajeruhi raia wawili waliokuwa jirani na eneo hilo.
Askari waliofariki katika tukio hilo ni E,5761 CPL Yahaya, F,4660 CPL
Hatibu, G9524 PC Tito na G.9996 PC Gastone na raia waliojeruhiwa ni Ally
Chiponda na Azizi Yahaya wote wakazi wa Mbande.
Katika tukio hilo,
majambazi hayo yalifanikiwa kupora silaha mbili za SMG na risasi sitini
(60) na hakuna pesa au mali za benki iliyoibiwa, ni dhahiri kwamba
walikuwa na kusudio la kujipatia silaha kwa ajili ya kufanya uhalifu na
si vinginevyo kama baadhi walivyotaka kupotosha.
Ikumbukwe kuwa
majambazi mara kadhaa mwaka jana katika maeneo mbalimbali chini, mfano
Kituo cha Stakishari Dar es Salaam na Kituo cha Polisi Ikwiriri ,
vilivyamiwa na majambazi kwa lengo la kuchukua silaha kwa ajili ya
uhalifu.
Aidha, Tunalipongoza Jeshi la Polisi kwa kuweza kuwafikia
majambazi hao huko Mkuranga bila kuumiza raia. Pia tunatoa pole kwa
familia za askari wote watano waliopoteza maisha wakiwa kazini.
Askari
anaekamilsha idadi ya askari waliouwawa kufika watano ni Askari Thomas
Njiku,Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Ujambazi alieuwa Vikindu wilayani
Mkuranga wakati akiongoza kikosi maalum cha kuwasaka watu waliosadikiwa
kuwa ni majambazi waliotekeleza tukio la kihalifu la Mbade,Mbagala.
Tunawasihi Watanzania kutoipokea dhana inayotaka kujengwa na wanasiasa
kuwa hatukemei matukio haya dhidi ya polisi.
Kumbukeni kuwa Mtandao wa
Watetezi umekuwa ukitoa matamko mbali mbali kukemea mauaji ya askari
wa jeshi la polisi, na tumekuwa mara kwa mara tukisisitiza kwamba askari
wa jeshi la polisi ni watetezi wa haki za binadamu, kwa kuwa jukumu lao
la kwanza ni kulinda mali za watu na usalama wa binadamu.
Mtandao
unatambua kuwa askari wa jeshi la polisi pia ni ndugu zetu, kaka zetu na
baba zetu hivyo madhila wanayokumbana nayo ni yetu sote.
Mfano,
katika repoti ya hali ya watetezi wa haki za binadamu kwa mwaka
jana(2015) , Mtandao uliweza kuwa na kipengele maalumu kilichozungumzia
haki za polisi na hali ya usalama kwa polisi wakiwa kama watetezi wa
haki za binadamu.
Katika ukarasa wa 18 wa repoti hiyo Mtandao uliweza
kurekodi matukio ya uvamizi na mauaji ya jeshi la polisi zaidi ya kumi
(10) na wengine watano (5) wakiachwa wamejeruhiwa. Kwa maana hii tukio
lilitokea Mbagala ni muendelezo wa matukio ya kiuhalifu yanayoendelea
nchini.
Kumekuwa na changamoto kutoka kwa Jamii kuwatambua askari
wa jeshi la polisi kama watetezi wa haki za binadamu, na hii ni kutokana
na ukweli kwamba baadhi ya askari wamekuwa wakitumia vibaya madaraka
yao kukandamiza haki za wananchi.
Hali ilivyo sasa inaweza kuharibu
dhana nzima ya polisi kuwa ni walinzi wa raia na mali zao, kwani vitendo
wanavyofanya polisi dhidi ya raia hasa wafuasi wa vyama vya siasa na
viongozi wao ni sababu kubwa ya kuharibu uhusiano mzuri kati ya polisi
na raia.
Mtandao unatambua kwamba jeshi la polisi ni mamlaka muhimu
sana katika kustawisha amani na ulinzi wa nchi kama litakuwa huru, bila
kuingiliwa na wanasiasa na kuegemea upande wowote.
Mtandao unapenda
kuona kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa weledi na kwa mujibu
wa sharia na katiba ya nchi. Aidha, Mtandao unaona pamoja na migongano
mbali mbali ya kazi za polisi na za wanasiasa ( hasa nafasi za wakuu
wa mikoa na wilaya), ni vyema polisi wakaangalia misingi ya kimataifa
ya haki za binadamu ili kuhakikisha usawa mbele ya jamii ili kurudisha
mahusiano mazuri baina ya polisi na jamii wanayoitumikia.
Sambamba
na hayo, Mtandao pia umesikikitishwa na kauli ya Mkuu wa mkoa wa Dar Es
Salaam Mhe Paul Makonda aliyotoa tarehe 25 agosti 2016 wakati wa kuaga
miili ya askari wanne waliouwawa huko Mbande Mkoani Dar es Salaam.
Mtandao unakemea matamshi ya aina hiyo kutoka kwa kiongozi yoyote Yule,
kwakuwa matamshi kama haya yanakwenda kinyume na misingi ya utawala
bora na haki za binadamu na yanaweza kuwa sehemu ya kupoteza amani ya
Taifa. Kitendo cha kukejeli haki za binadamu na kuamuru askari polisi
wapige tu bila kujali taratibu za kisheria kinakwenda kinyume na misingi
ya utawala bora.
Tunapenda viongozi wa serikali watambue kwamba
kazi ya kulinda na kutetea haki za binadamu ni ya kikatiba na ndiyo
maana kupitia Katiba yetu tuna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
iliyoundwa kwa lengo la kuhakikisha viongozi wanaheshimu misingi ya
utawala bora na haki za binadamu. Watetezi wa haki za binadamu
wanatambulika kote duniani na wanalindwa kisheria mfano, kimataifa tuna
Tamko la watetezi wa haki za binadamu la mwaka 1998.
Madhara ya Uhusiano Mbaya kati ya Polisi na Raia
Ili Jeshi la Polisi liweze kufanya kazi yake vizuri ya kupambana na
uhalifu hawana budi kuhakikisha wanakuwa karibu na wananchi. Madhara ya
kutokuwa na mahusiano mazuri kati ya Jeshi la Polisi na raia ni makubwa.
• Mojawapo ya madhara ni pamoja na kukua kwa makosa ya jinai na polisi kukosa taarifa za waalifu toka maoneo mbalimbali.
• Hali ya makosa ya jinai Tanzania imezidi kukua katika kiwango
kikubwa. Kukua kwa makosa ya jinai ni zao la kutokuwa na mahisiano
mazuri kati ya raia na polisi.
Wito wetu;
• Mtandao unatoa pole
kwa Jeshi la Polisi pamoja na familia za askari hao na tunatoa wito kwa
askari wengine wa jeshi la polisi kuendelea na kazi zao kwa weledi huku
wakiboresha mahusiano mazuri na wananchi.
• Tunaishauri serikali kuliongezea nguvu Jeshi la polisi na kuboresh utalaamu katika kufanya kazi zao
• Tunawasihi askari wa Jeshi la wananchi kuheshimu mipaka ya kazi zao
na kuheshimu haki za binadamu na katiba ya nchi katika kutekeleza kazi
zao za kila siku
• Tunaishauri serkali kuwe na mabadiliko katika
mfumo wa jeshi la polisi kuanzia kwenye mfumo wa kisheria ambao utatoa
wajibu na uwajibikaji na kuheshimu haki za binadamu
• Tunaomba umma
kutoa taarifa kwa jeshi la polisi na vyombo vya usalama hasa pale
wanapohisi kuna tukio linalo ashiria uvunjaji wa amani na usalama.
•
Tunaiomba serikali yetu kuipa kipaumbele jeshi la polisi katika
kuboresha vitendea kazi vyao,nyumba za kuishi na mishahara bora ili
kukidhi hali ya maisha ya sasa.
• Tunawaomba wadau wengine wa Haki
za Binadamu pamoja na mashirika mengine ya maendeleo kukemea vikali
tukio hilo. Tunashauri viongozi wa siasa waache kuingilia kazi za polisi
ili kuepuka migogoro
PICHANI JUU :Wakili wa THRDC akiwaonyesha
waandishi wa habari(hawapo pichani) repoti ambayo ilitolewa na THRDC juu
ya hali ya Watetezi wa Haki za Binadamu kwa mwaka jana(2015) ,ambayo
ina kipengele maalumu kilichozungumzia haki za polisi na hali ya usalama
kwa polisi wakiwa kama watetezi wa haki za binadamu katika ukarasa wa
18 wa repoti hiyo, http://thrdc.or.tz/download/situation-report-2015/
Imetolewa na Onesmo Olengurumwa
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
Imewasilishwa na Bennedict Ishabakaki
Wakili wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
30/08/2016
0 comments:
Post a Comment