Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini imemuandikia barua Katibu Mkuu wa
Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kufuatia mvutano wa
kusimamishwa uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa
Ibrahim Lipumba.
Hatua
hiyo imefikiwa baada ya Profesa Lipumba kumuandikia barua Msajili wa
vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi akilalamikia kusimamishwa
uanachama bila kufuata utaratibu huku akitaka kurejeshwa kwenye nafasi
yake ya uenyekiti.
Ofisi
hiyo imeutaka uongozi wa CUF kueleza kwa kina hatua ilizopitia hadi
kufikia uamuzi huo kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, na kwamba
iwasilishe barua hiyo kufikia kesho majira ya saa 9:30 alasiri.
Mkuu
wa kitengo cha Mawasiliano cha Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa,
Monica Laurent amesema kuwa ofisi hiyo ilipokea barua ya Profesa Lipumba
Agosti 29 mwaka huu ikiwa na malalamiko na kwamba wametaka uongozi wa
CUF kutolea majibu.
“Tumeitaka CUF kutoa majibu kuhusu malalamiko ya Profesa Lipumba, ndipo sisi tutakapotoa majibu,” amesema Monica.
Lipumba
ambaye alijiuzulu nafasi yake ya Uenyekiti mwaka jana akipinga uamuzi
wa chama chake kumuunga mkono Edward Lowassa kugombea urais, amerejea na
kudai kutengua barua yake ya kujiuzulu.
Baraza
Kuu la CUF lililoketi visiwani Zanzibar hivi karibuni lilimsimamisha
uanachama Profesa Lipumba pamoja na viongozi wengine 10 akiwemo Mbunge
wa Kaliua, Magdalena Sakaya aliyekuwa Naibu Katibu mkuu (Bara).
Hata hivyo, Profesa Lipumba amepinga uamuzi huo akieleza kuwa kikao cha baraza hilo kililiwa batili.
0 comments:
Post a Comment