MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imetoa amri ya kukamatwa Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na kuamuru wadhamini wake kufika
mahakamani hapo kujieleza kwanini wasilipe fungu la dhamana kutokana na
mshtakiwa huyo kushindwa kufika kusikiliza kesi yake bila ruhusa.
Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka ya uchochezi kupitia gazeti la Mawio.
Amri
hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya upande
wa Jamhuri kudai kuwa kesi hiyo ilipangwa jana kutajwa lakini mshtakiwa
wa nne Lissu hakuwepo mahakamani.
Hata
hivyo, alijitokeza mdhamini wake mmoja kati ya wawili Robart Katula
kudai kuwa mshtakiwa huyo anaendesha kesi ya uchaguzi Mahakama Kuu
Tanzania, Kanda ya Mwanza.
Hakimu alihoji kwa nini mshtakiwa amesafiri na kuacha kuhudhuria kesi yake bila kuomba kibali cha mahakama yake.
"Mshtakiwa
Lissu anafanya dharau kila wakati inapopangwa kesi yake mahakamani
anashindwa kuhudhuria bila kutoa sababu ama kuomba ruhusa ya mahakama...
kama asingekuwa nje kwa dhamana angefanyaje? angetumia busara kuomba
ruhusa" alihoji na kuongeza kuwa.
"Wadhamini
wa mshtakiwa wapelekewe wito wa mahakama waje kujieleza kwanini
wasilipe fungu la dhamana kama walivyoahidi kwenye hati ya dhamana ya
maneno ya Sh. milioni 10 kila mmoja" alisema Hakimu Simba.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Patrick Mwita aliomba mahakama hiyo kutoa hati ya kukamatwa mshtakiwa.
Hakimu
Simba alikubali ombi la Jamhuri na kutoa amri ya kukamatwa mshtakiwa na
wito kwa wadhamini kufika mahakamani Novemba 21, mwaka huu kujieleza
kwa nini wasilipe fungu la dhamana dhidi ya mshtakiwa kwa kushindwa
kuhudhuria kesi yake.
Mbali
na Lissu, washtakiwa wengine ni, Wahariri wa gazeti la Mawio, Simon
Mkina na Jabir Idrisa na mchapaji wa magazeti, Ismail Mehboob.
Katika
kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, mwaka huu,
Dar es Salaam, Lisu na wenzake walikula njama ya kuchapisha chapisho la
uchochezi katika gazeti la Mawio lenye kichwa cha habari kisemacho,
‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Pia
Lissu na wenzake walidaiwa Januari 14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa
nia ya kuleta chuki na uchochezi kati ya wananchi na mamlaka halali ya
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, walichapisha chapisho hilo lenye
uchochezi.
Aidha,
Lissu alidaiwa siku hiyo kinyume cha sheria na bila ya mamlaka
waliwatishia na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia
kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.
Washtakiwa walikana mashtaka hayo kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana.
0 comments:
Post a Comment