Serikali jana imewasilisha bungeni muswada wa sheria ya huduma za habari mwaka 2016, huku ikitaja marekebisho saba katika muswada huo.
Marekebisho
hayo ni pamoja na kuainisha haki na wajibu wa wanahabari, kuainisha
haki ya chombo cha habari kukata rufaa, uwakilishi wa wanahabari katika
bodi ya ithibati, Jaji Mkuu kuweka utaratibu wa kusikilizwa haraka kesi
za kashfa.
Mengine
ni kuviondolea vyombo vya habari adhabu kwa baadhi ya makosa ya
mwandishi, vyombo vya dola kukamata mitambo na vifaa vya wanahabari na
mitambo kutohusika moja kwa moja kwa kosa la gazeti.
Akiwasilisha bungeni muswada huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema
marekebisho hayo yamefanyika baada ya mashauriano na wadau wa habari
wakiwamo wananchi, wanataaluma ya habari, wanasheria na kamati nyingine
za bunge.
Alisema
katika eneo la kuainisha haki na wajibu wa wanahabari, muswada wa awali
kwa kiasi kikubwa uliainisha zaidi wajibu wa wanahabari lakini kwa
kuzingatia mikataba ya kimataifa ambayo nchi imesaini na kuridhia na
matakwa ya katiba.
Nnauye alisema
kwa sasa eneo hilo limerekebishwa katika kifungu cha saba kwa kuainisha
pia haki za wanahabari kama vile uhuru wa kukusanya, kuhariri na
kuchapisha au kutangaza habari.
Alisema
kuhusu kuainisha haki ya chombo cha habari katika kukata rufaa, katika
kifungu cha 10 kuhusu utoaji wa leseni za vyombo vya habari , muswada wa
awali haukuwa umeweka haki ya kukata rufaa kwa atakayekataliwa kupewa
leseni na Mkurugenzi wa Idara ya Habari.
Alibainisha
kuwa chombo husika kinaweza kukata rufaa kwa waziri wa habari na pia
mwishowe kisiporidhika na uamuzi wa waziri sasa kinaweza kupinga suala
hilo mahakamani.
Kuhusu
uwakilishi wa wanahabari katika bodi ya ithibati, Nnauye amesema eneo
hilo limeboreshwa ni uwakilishi wa vyombo vya habari katika bodi hiyo,
na kwa mujibu wa mapendekezo ya awali, bodi hiyo itakayokuwa na wajumbe
saba sasa itakuwa na wanahabari wanne akiwemo mwenyekiti.
Alisema
suala la Jaji Mkuu kuweka utaratibu kusikilizwa haraka kesi za kashfa,
moja ya malalamiko makubwa ya wadau katika utoaji wa haki zinapokuja
kesi za habari hasa za masuala hayo ni kuchukua muda mrefu kwa kesi
hizo.
Katika maboresho ya kipengele hicho, alisema
hivi sasa jaji huyo kwa kuzingatia tathmini ya uwezo wa Mahakama na
rasilimali zilizopo na kama ilivyowekwa kwa kesi nyingine kama za
uchaguzi atatunga kanuni zitakazoweka muda wa kumalizika kwa kesi za
aina hiyo.
Kadhalika, Nnauye alisema
kuhusu vyombo vya dola kukamata mitambo na vifaa vya wanahabari,
maboresho yamefanywa kwa kulenga kumuondoa mkurugenzi wa idara ya habari
kuwa na mamlaka ya kukamata mitambo hiyo.
0 comments:
Post a Comment