Siku
tatu baada ya Rais John Magufuli kueleza bayana kwamba suala la Katiba
Mpya si kipaumbele chake kwa sasa akitaka aachwe ili ainyooshe nchi
kwanza, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema kiongozi huyo
hawezi kunyoosha nchi bila kuwa na Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya
wananchi.
Wakati
Lissu akisema hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji
mstaafu Damiani Lubuva amesema atatolea ufafanuzi suala hilo siku za
karibuni.
Lubuva
na Lissu walieleza hayo walipotakiwa kuzungumzia kauli ya Rais Magufuli
kwamba kipaumbele chake ni kuchapa kazi ili kuinyoosha nchi na mengine
yafuate ikiwamo Katiba Mpya.
Magufuli
alitoa kauli hiyo Novemba nne, alipozungumza na Wahariri wa vyombo
mbalimbali vya habari siku moja kabla ya kutimiza mwaka mmoja tangu
aingie madarakani.
Lakini,
Lissu alisema nchi haiwezi kunyooka bila kunyoosha kwanza Katiba
inayoiongoza ambapo alipendekeza uwepo wa Katiba Mpya badala ya
kuifanyia marekebisho iliyopo sasa.
“Tulishaondoka
kwenye mjadala wa kuziba viraka kwenye Katiba, tumeshakubaliana kwamba
tunahitaji mabadiliko ya Katiba yote si sehemu tu. Rais asidhani mtu
akikalia kiti hicho basi neno lake ni sheria ya nchi. Haiwezekani,” alisema.
Alisema mchakato wa Katiba Mpya hautakiwi kuendelea ulipoishia kwa maelezo kuwa ikiwa hivyo nchi haiwezi kufika popote.
“Katiba
Inayopendekezwa ni kama imepakwa rangi ya Katiba ya sasa. Inaonekana
mpya lakini misingi yake ni ya Katiba ya sasa…, kama Rais Magufuli
anataka kunyoosha nchi, anapaswa kuirejea Rasimu ya Jaji Warioba.
Tuanzie hapo, zaidi ya hivyo atajidanganya na kuwadanganya Watanzania,” alisema.
Lissu
ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema nchi haiwezi kuongozwa
kwa matamko ya kiongozi mkuu pekee bila kuangalia matatizo ya kisheria.
“Anafikiri
akiamua yeye kama Rais unafuata utekelezaji? Kuna matatizo mengine ya
kikatiba…, hayawezi kubadilika bila kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba.
Kuna mambo ili yanyooke ni lazima uwe na Katiba nzuri.
Usipoyashughulikia hayo mengine yote hayatawezekana,” alisema Lissu.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ,Jaji Lubuva alipoulizwa kuhusu
mchakato wa Katiba Mpya na kauli ya Rais Magufuli alisema suala hilo
linahitaji kukaa na kulizungumza vizuri.
“Naomba
upokee kuwa nimekuelewa ila kwa sasa ninachoweza kusema nitatoa
ufafanuzi mzuri kuhusu suala hilo kwani ni jukumu la ofisi yangu,” alisema.
Alisema
ni kweli baada ya Katiba Inayopendekezwa kupigiwa kura na Bunge hatua
iliyokuwa inafuata ilikuwa ni kuitisha Kura ya Maoni, lakini
ilishindikana kutokana na kuingiliana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Kabla
ya Rais Magufuli kutoa kauli yake kuhusu Katiba Mpya, siku za karibuni
NEC iliwahi kueleza kwamba ipo katika hatua mbalimbali za kuhakikisha
mchakato huo unafanyika kwa mujibu wa sheria.
Katika
kauli yake ya Novemba nne, Rais Magufuli alisema wakati anaomba kura
hakuweza kuzungumzia Katiba hivyo kwa sasa kilichopo mbele yake ni
kunyoosha nchi kwanza na Katiba mpya itakuja baadaye.
0 comments:
Post a Comment