Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amefunguka juu ya uamuzi wa chama chake cha Mapinduzi (CCM) kuwafukuza baadhi ya wanachama waliobainika kukiuka misingi ya sheria na kanuni za chama hicho.
Amesema chama hicho hakina budi kuwaeleza wananchi kwa undani kuhusu hatua hiyo ili kuondoa sintofahamu.
Ridhiwani ambaye ni mtoto wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema ingawa CCM imefanya hivyo kwa lengo la kujiimarisha, isipopeleka mrejesho kwa wanachama wake anaweza kutokea mtu akapika taarifa zinazoweza kuwa tofauti na ukweli.
“Lazima chama kiangalie namna ya kuendelea kusimama kwa kuwa waliofukuzwa walikuwa na watu, na walichaguliwa. Kwa mfano (aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoani Dar es Salaam, Ramadhan) Madabida alichaguliwa na watu, hivyo ni lazima waelezwe kilichotokea,” alisema Ridhiwani.
Akielezea wasiwasi huo, Ridhiwani alionya kuwa kuna watu ni mafundi wa kupika taarifa kwa maslahi yao na wanaweza kwenda kwa wananchi kuwaambia uongo kuhusu hatua hiyo.
“Akishuka mtu mpaka chini akawaambia watu wamemwonea au hawakufanya haki, wanaweza kuamini. Sasa, badala ya kujenga chama mtajikuta mnaanza kutumia nguvu kujenga umoja wenu,” alisema.
Pamoja na angalizo hilo, mbunge huyo wa Chalinze alisema haoni kama kuna mwanachama aliyeonewa kwa kufukuzwa au kuonywa kwa kuwa makosa yao ni mazito.
“Sidhani kama kuna aliyeonewa na adhabu waliyopewa ilistahili kutokana na makosa yao tuliyoelezwa,” alifafanua.
Katika sakata hilo, mjumbe mmoja wa Kamati Kuu, Sophia Simba alivuliwa uanachama pamoja na wenyeviti wanne wa mikoa ya Iringa, Shinyanga, Mara na Dar es Salaam, wenyeviti wa wilaya na kuwaonya viongozi wengine kutokana na makosa ya usaliti na kukihujumu chama.
Habari zaidi Soma Gazeti la Mwananchi
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment