Wednesday 21 June 2017

Meya Ubungo Aendelea Kusota Selo, Wengine Wawili Wapata Dhamana.

Wakati viongozi wawili kati ya watatu wa Chadema waliokuwa wakishikiliwa polisi wakipata dhamana, mmoja anaendelea kushikiliwa kutokana na agizo la mkuu wa wilaya.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo amesema Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob ataendelea kuwa rumande hadi agizo la saa 48 lililotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori litakapokamilika.

Jacob alichukuliwa na polisi juzi saa sita mchana akiwa makao makuu ya manispaa hiyo, Kibamba, akiwa katika msafara uliokuwa unaelekea kukagua miradi ya maendeleo akiwa na viongozi wenzake wa Chadema, akiwamo mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Ingawa polisi hawakusema sababu ya kumhitaji, Kilewo aliliambia gazeti hili kuwa chombo hicho cha dola kiliamua kumweka rumande meya kwa kosa la kutumia ukumbi wa halmashauri kwa shughuli za chama bila mkurugenzi kuwa na taarifa.

Kilewo alidai kosa jingine ni hatua yake ya kutaka kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo akiwa na viongozi wa chama chake ambao si madiwani.

Baada ya Jacob, ambaye ni diwani wa Ubungo kuwekwa rumande, taarifa zilisambaa zikieleza kuwa mkuu wa wilaya ameagiza akamatwe pamoja na viongozi wengine.

Mkuu huyo wa wilaya hakutaka kufafanua alipoulizwa kuhusu suala hilo. “Waliokamatwa mmeshawaona, watakaokamatwa mtajua. Hakuna siri hapa. Naomba niishie hapa kwa sababu nipo katika kikao,” alisema.

Wakili wa meya huyo, Frederick Kihwelo alisema mteja wake yupo katika hali nzuri na kwamba wanasubiri busara za mkuu wa wilaya za kumwachia au kumalizika kwa saa 48 alizozitoa.

Katika hatua nyingine, mkoani Iringa polisi wamemwachia kwa dhamana makamu mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick ole Sosopi baada ya kumshikilia kwa siku moja.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, John Kauga alisema jana kuwa hatua hiyo imefikiwa wakati utaratibu wa kuandaa jalada kwa ajili ya kuliwasilisha Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali ukiendelea.

Sosopi, ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la vijana Jimbo la Isimani, alikamatwa juzi kwa tuhuma za kufanya mkutano bila kibali katika kata mbalimbali za jimbo hilo.

Pia Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Hai, Helga Mchomvu jana aliachiwa kwa dhamana baada ya kushikiliwa kituo cha polisi Bomang’ombe kwa mahojiano.

Mwenyekiti huyo juzi aliendesha kikao cha baraza chini ya ulinzi wa polis.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah alisema nguvu ya polisi iliyotumika kumfikisha kituoni haikupaswa, bali ilifikiwa kutokana na yeye kukaidi amri ya jeshi hilo.

Imeandikwa na Bakari Kiango, Dar; Geofrey Nyang’oro, Iringa na Fina Lyimo, Hai. 


Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment