Huku Yanga wenyewe wakisubiria Ligi Kuu Bara imalizike
ili wafanikishe usajili wa beki wa kulia wa Simba, Hassan Kessy, sasa
sakata hilo limekuwa kama filamu ya kusisimua baada ya Azam jana kumteka
na kumalizana naye kwa asilimia kubwa kuhusu usajili wake.
Beki huyo, hivi sasa ameziingiza kwenye vita kubwa Yanga
inayofundishwa na Mholanzi, Hans van Der Pluijm na Azam iliyo chini ya
Muingereza, Stewart Hall, zote zikimuwania.
Kessy ni mchezaji huru hivi sasa anayeruhusiwa kufanya
mazungumzo na klabu nyingine yoyote itakayomhitaji kwa ajili ya msimu
ujao kutokana na mkataba wake kumalizika mwezi huu mwishoni.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi
wa Azam, beki huyo Jumamosi iliyopita alipigiwa simu na viongozi wa timu
hiyo kwa ajili ya kwenda kukutana naye na lengo likiwa ni kufikia
makubaliano ya dau la fedha analolihitaji na mahitaji yake mengine
ikiwemo nyumba ya kuishi na usafiri.
Chanzo hicho kilisema, uongozi wa Azam umefikia
makubaliano hayo ya kumsajili kwa ajili ya kuongezea nguvu safu yao ya
ulinzi hasa pembeni, hiyo ni baada ya beki wao, Shomari Kapombe
kusumbuliwa na majeraha ambayo yamemsababishia kushindwa kumalizia mechi
za mwishoni za msimu huu.
Kiliongeza kuwa, beki huyo jana alitarajiwa kutua jijini
Dar es Salaam akitokea Morogoro alipokwenda kupumzika akitumikia adhabu
ya kutocheza mechi tano za ligi kuu baada ya uongozi wa Simba kumfungia
kwa kosa la kumchezea rafu mshambuliaji wa Toto Africans, Edward
Christopher na kupewa kadi nyekundu.
“Kessy leo (jana) anatarajiwa kukutana na viongozi wa
Azam kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kumsajili kwa ajili ya msimu
ujao, wameanza naye mazungumzo ya mapema kwa ajili ya kuiwahi Yanga
inayomhitaji.
“Viongozi walizipata taarifa za Yanga kumuwania Kessy
kwenye usajili wao katika msimu ujao, hivyo uongozi umeona ni vyema
ukaanza mchakato huo mapema wa kumsajili.
“Kessy atawasili Dar asubuhi (jana) akitokea Morogoro na
mara baada ya kumalizana naye, basi atarudi huko kwa ajili ya
mapumziko,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Kessy kuzungumzia hilo alisema: “Hizo
taarifa za mimi kupigiwa simu na viongozi wa Azam umezipata wapi? Naomba
nisilizungumzie hilo suala kwa kipindi hiki, tusubirie kwanza ligi
imalizike kwani kila kitu kitajulikana.
“Mimi hivi sasa bado mchezaji wa Simba hadi ligi kuu
itakapomalizika, na wao ndio wanaopaswa kunilipa mshahara hadi sasa,
hivyo nisingependa kuongea kitu chochote kwa hivi sasa,” alisema Kessy.
0 comments:
Post a Comment