Hatimaye
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye amekuwa
akitafutwa na Jeshi la Polisi kwa siku kadhaa alikamatwa jana katika
Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) alipowasili akitokea Japan.
Baada
ya Askofu Gwajima kukamatwa na Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa JNIA
alipelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya mahojiano
akidaiwa alitoa maneno ya uchochezi mwezi uliopita.
Akizungumzia
kukamatwa kwake, Kamanda wa Polisi Uwanja wa JNIA, Martin Otieno
alisema askofu huyo aliwasili saa 2.45 asubuhi akitokea Japan kwa
kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.
Otieno
alisema mara baada ya kukamatwa alipelekwa katika Kituo Kikuu cha
Polisi kwa ajili ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam.
“Ni
kweli tulimkamata Askofu Gwajima hapa uwanja wa ndege wa JNIA baada ya
kuwasili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya na tulipomuhoji alidai
kuwa alikuwa nchini Japan,” alisema Otieno.
Mwanasheria
wake Peter Kibatala alisema Gwajima alifika Kituo Kikuu cha Polisi saa
4.45 asubuhi kwa mahojiano mafupi na aliruhusiwa kuondoka baada ya
kujidhamini yeye mwenyewe.
“Askofu
Gwajima amehojiwa leo (jana) na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu na
amejidhamini yeye mwenyewe, ameruhusiwa kuondoka hivyo tunasubiri
chochote kitakachoendelea,” alisema Kibatala bila kueleza mahojiano yalivyokuwa.
Askofu
Gwajima alikuwa anatafutwa na polisi tangu mwezi uliopita baada ya
kusambazwa mkanda kwenye mitandao ya kijamii unaodhaniwa una sauti yake
akipendekeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete kufikishwa mahakamani kwa yote
yaliyofanyika wakati wa utawala wake ambayo sasa Rais John Magufuli
anayashughulikia kwa mtindo wa kutumbua majipu.
Katika
mkanda huo, sauti hiyo inadai kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wametuma
watu mikoani kupiga kampeni ya kutaka Rais Magufuli asipewe uongozi wa
chama hicho kwa sasa kama ilivyo utaratibu wa chama hicho na kwamba hilo
likifanyika basi Rais abadili katiba ili mstaafu huyo aweze kufikishwa
kortini.
Tangu
ulipotolewa mkanda huo, makachero wa polisi wamekuwa wakipiga kambi
nyumbani kwa Askofu Gwajima kwa lengo la kumkamata lakini hawakumpata.
Baadaye ilikuja kufahamika kwamba askofu huyo alikuwa amekwenda nje ya nchi lakini haikujulikana ni nchi gani.
Hata
hivyo, baada ya kutafutwa na polisi, Gwajima kupitia wakili wake
Kibatala alisema atakaporejea nchini atakwenda moja kwa moja polisi kwa
ajili ya mahojiano.
Kamanda
wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amekuwa akisisitiza
kwamba jeshi litaendelea kumtafuta askofu huyo kwa kushirikiana na
polisi wa kimataifa, Interpol.
0 comments:
Post a Comment