Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) imekamata akaunti za Kampuni ya Sahara Media Group kwa kushindwa kulipa deni la Sh4 bilioni kama kodi iliyopaswa kulipwa na kampuni hiyo.
Taarifa zilizosambaa kupitia mitandao ya kijamii zimeeleza kuwa
akaunti zote za kampuni hiyo zimefungiwa mpaka pale watakapolipa deni
hilo, lakini kampuni hiyo imetoa ufafanuzi.
Ujumbe huo uliongeza kuwa kampuni hiyo imefikishwa mahakamani na
benki moja hapa nchini kwa madai ya kutaka kulipwa Sh600 milioni, baada
ya kuingia makubaliano ya kulipa wafanyakazi wake mishahara pamoja na
mikopo lakini mpaka sasa imeshindwa kurejesha fedha hizo.
Hata hivyo, akizungumzia suala hilo mwenyekiti mtendaji wa kampuni
ya Sahara, Anthony Diallo alikiri mamlaka hiyo kufungia akaunti ya
kampuni yake.
Diallo ambaye ndiye mmiliki wa kampuni hiyo alisema ni akaunti moja
tu iliyofungiwa na kwamba anaamini baada ya kukutana na kufanya
mazungumzo na mamlaka hiyo watafikia muafaka ili biashara ziendelee kama
kawaida.
“Tutalimaliza hakuna kitakachoenda mrama,” alisisitiza
Diallo ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo
nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri wa Maji,
Maendeleo ya Mifugo katika Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu Jakaya
Kikwete.
Amesema deni la TRA linatokana na kodi iliyopatikana baada ya ukaguzi wa vitabu kwa miaka mitatu.
“Ni ukaguzi wa kawaida hufanyika kama taratibu. Sasa kwa sababu
ya kuhamisha matangazo yetu kutoka analojia kwenda digitali ilibidi
tukope benki, ujenzi na kumaliza mradi imechukua miaka mitatu. Wakati
wote tumekuwa tukilipa riba benki na zinazobaki toka mauzo ya matangazo
tunalipa mishahara, umeme na malipo ya kodi za kawaida,”alisema.
“Ni kawaida ila wamefanya hatua za kutuaibisha tu. Kampuni yetu
ya ving’amuzi ni ya Kitanzania na mapato yote yanaingia nchini wakati
kampuni nyingine kubwa zote ni za kigeni kutoka China, Afrika Kusini,
Mauritius na Kenya! Ukweli sisi tunahitaji kusaidia nchi kiuchumi na
kutuharibia ni hasara kwa nchi.”
0 comments:
Post a Comment