Saturday 23 April 2016

#YALIYOJIRI>>>>Mkurugenzi Mkuu wa Zamani wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Naibu wake wana Kesi ya kujibu.Fahamu zaidi hapa.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) Ephraimu Mgawe (Kulia) na Makamu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Hamadi Koshuma
 *****
 
Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Ephraim Mgawe na aliyekuwa Naibu wake, Hamad Koshuma wana kesi ya kujibu ya matumizi mabaya ya madaraka, imefahamika.

Mgawe na mwenzake wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kutoa zabuni kwa kampuni ya China ya Communication Construction Company Limited kwa ajili ya ujenzi wa magati katika Bandari ya Dar es Salaam.

Jana mahakama hiyo katika uamuzi wake baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka, iliwaona washtakiwa hao kuwa wana kesi ya kujibu kwa mashtaka yanayaowakabili, hivyo watapanda kizimbani kujitetea, Mei 16 mwaka huu.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkazi Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo, alisema kwamba ameridhika kuwa upande wa mashtaka umeweza kujenga kesi dhidi ya washtakiwa hao na kuwa wana kesi ya kujibu.

“Baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka pamoja na vielelezo, nimeridhika kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu, hivyo wanatakiwa kutoa utetezi wao,” alisema hakimu Mkeha.

Baada uamuzi huo, Mgawe aliieleza mahakama kuwa anatarajia kuita mashahidi tisa kumtetea mahakamani hapo, huku Koshuma akisema kuwa yeye atajitetea mwenyewe na kwamba hatakuwa na shahidi mwingine.

Mgawe na Koshuma wanadaiwa kula njama na kutoa zabuni tata kwa kampuni hiyo kwa ajili ya kujenga maghati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa gharama ya Dola 600 milioni (Sh1.3 trilioni) kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mkataba wa kibiashara na kampuni hiyo bila zabuni shindanishi kinyume cha sheria hiyo ya manunuzi ya umma.

Hata hivyo, wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwaita mahakamani jumla ya mashahidi watano kujenga kesi yao, akiwamo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa mamlaka hiyo, Kokutulage Kazaura.

Kwa upande mwingine, Mahakama hiyo imeshindwa kutoa uamuzi wa uhalali wa shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya na wenzake wawili.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mshindi wa Mashindano ya Urembo (Miss Tanzania), mwaka 1996, Shose Sinare na Sioi Solomon ambao walikuwa wafanyakazi waandamizi wa Benki ya Stanbic tawi la Tanzania.

Washtakiwa hao watatu wanadaiwa kutakatisha fedha dola 6 milioni (1.2 bilioni) wakati Serikali ilipokopa Dola 550 milioni (takriban Sh1.2 trilioni) kati ya mwaka 2012 na 2013 kutoka katika Benki ya Standard ya Uingereza ambayo ni kampuni mama ya Stanbic.

Washtakiwa hao kupitia kwa mawakili wao walihoji uhalali wa shtaka hilo na kuiomba mahakama ilifute pamoja na mambo mengine wakidai kuwa halijakidhi vigezo vya kisheria kuitwa shtaka la utakatishaji fedha.

Maombi yao hayo yalitarajiwa kutolewa uamuzi jana na Hakimu Mkazi Emilius Mchauru, anayesikiliza kesi hiyo, lakini uamuzi huo ulikwama na badala yake ulipigwa kalenda hadi Aprili 27, mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment