KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema kuwa kadi sita za
njano ambazo wachezaji wake wamepata katika mechi ya juzi dhidi ya
Mouloudia Bejaia (Mo Bejaia) ya Algeria, zitawaweka kwenye mazingira
magumu ya mechi zinazofuata za mashindano hayo ya Kombe la Shirikisho
Afrika.
Katika mechi hiyo ya kwanza ya Kundi A, Yanga ililala bao
1-0 wakati TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ikipata
ushindi mnono wa magoli 3-1 dhidi ya Medeama ya Ghana na kuongoza kwenye
kundi hilo.
Wachezaji wa Yanga waliopata kadi katika mechi hiyo ni
Mwinyi Haji ambaye ameonyeshwa kadi nyekundu na hivyo kukosa mchezo
unaofuata wakati walioonyeshwa kadi za njano ni pamoja na Donald Ngoma,
Simon Msuva, Haruna Niyonzima na Amissi Tambwe.
Pluijm alisikitika pia kupoteza mechi hiyo licha ya kuwaandaa vizuri wachezaji wake na kuwapa mbinu mbalimbali za kuwakabili Waarabu hao wa Algeria.
Mdachi huyo pia aliwalaumu waamuzi waliochezesha mechi hiyo kutoka Morocco kwa kuwapendelea zaidi wenyeji.
Naye Kocha Msaidizi Juma Mwambusi alisema kuwa wachezaji hawakuwa waangalifu katika dakika za mwanzo za mchezo huo na kuwafanya wenyeji watawale mchezo huo.
Kocha huyo wa zamani wa Mbeya City alisema kuwa kikosi hicho kilizinduka katika kipindi cha pili na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara lakini hayakuzaa matunda.
“Kipindi cha pili tuliamka lakini hatukufanikiwa kupata goli, kwa sababu mashambulizi yetu yalikuwa yanavurugwa na mwamuzi, kikubwa imepita na tunajipanga kuangalia mchezo unaofuata,” alisema Mwambusi.
Kikosi cha wawakilishi hao pekee wa Tanzania kwenye mashindano ya Yanga kiliondoka Algeria jana jioni na kurejea Uturuki kuendelea na mazoezi na kinatarajia kuwasili nchini Jumatatu.
0 comments:
Post a Comment