Saturday, 18 June 2016

#YALIYOJIRI>>>Mke Wa Rais Mama Janeth Magufuli Akabidhi Vyakula Vya Futari Kwa Vituo Vinne Vya Kulea Watoto Yatima Jijini Dar Es Salaam.Fahamu zaidi hapa.

MKE wa Rais Mama Janeth Magufuli amekabidhi chakula kwa ajili ya futari wakati huu wa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa vituo vinne vya kulea watoto yatima na wale waishio katika mazingira magumu Jijini Dar es salaam.

Vyakula hivyo vimekabidhiwa leo tarehe 18 Juni, 2016 katika ofisi ya Mke wa Rais Ikulu Jijini Dar es salaam vimejumuisha Mchele kilogramu 500, Sukari kilogram 500 na Tende kilogramu 28.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi vyakula hivyo, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli aliyeongozana na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewatakia heri Waislamu wote katika mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuwasihi waendelee kuliombea Taifa amani na utulivu.

“Tunawatakia mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, katika kipindi hiki tunawaomba mzidi kuiombea nchi yetu amani, viongozi wetu wa nchi na watanzania wote kwa ujumla, nchi ikiwa na amani ndio mambo mengi mazuri yanaweza kufanyika”

Kwa niaba ya vituo vilivyopatiwa vyakula hivyo, Mwenyekiti wa Kituo cha Charambe Islamic Center Dkt. Haruni Kondo amemshukuru Mke wa Rais kwa kutoa vyakula hivyo na ameeleza kuwa kitendo hicho kinaonesha mshikamano na ushirikiano walionao watanzania wote bila kujali tofauti ya dini, kabila wala maeneo wanayotoka.

“Kwa hiyo ndugu zangu mna imani ya kikristo lakini mnatambua waislamu ni ndugu zenu, wote tunajenga nyumba moja, mshikamano ndio tunu tuliyoachiwa na Baba yetu wa Taifa, leo mmeguswa kuona wenzenu tunafanya ibada na nyinyi mmeingia kwenye ibada, sasa ibada ya kutoa ni ibada kubwa sana, sio nchi nyingi katika Afrika zinafanya kitendo hiki, watu hawaelewi, ni nchi chache sana ambazo imani moja inaunga mkono imani nyingine, lakini sisi waislamu tunalitambua hili hata toka kipindi ambacho mtume wetu SWA anapigana kusimika dini hii kwa waumini alipata nusura kwa wakristo”

Vituo vilivyokabidhiwa vyakula hivyo ni Charambe Islamic Center, Tasofe Lqadiria, Nur Twarigatu Lqadiria na Zawiyatul Lqadiria.

0 comments:

Post a Comment