Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameendelea na
kasi yake ya kutumbua majipu ambapo jana alishusha nyundo kwa majipu
mapya 7 yanayotafuna uchumi wa nchi kwa kuiibia Serikali kwa mbinu
mbalimbali kupitia miamala ya fedha.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 50 ya Benki Kuu
ya Tanzania (BOT), Rais Magufuli alisema kuwa Serikali yake haiwezi
kuyavumilia makampuni ya Madini yanayofanya kazi nchini kwa kuendelea
kuieleza Serikali kuwa yanapata hasara miaka yote huku yakiendelea na
shughuli zake za uchimbaji madini.
Rais Magufuli alisisitiza kuwa kama Makampuni hayo yanasema yanapata hasara kila mwaka ni bora yaondoke nchini.
“Hivyo ni visingizio tu, ni bora tubaki na madini yetu miaka 1,000 watachimba watakaokuja sisi tukiwa tumeoza,” alisema.
“Wanadai wanapata hasara wakati wana akaunti sehemu nyingine,” aliongeza Rais Magufuli.
Rais
Magufuli pia alieleza kuwa tayari amebaini kuwepo kwa malipo ya zaidi
ya shilingi bilioni 7 yasiyo ya halali (hewa) kwa wastaafu 2,800 kupitia
Benki ya NMB. Katika hilo alieza kuwa tayari ameshatoa maagizo watu hao
warejeshe fedha hizo.
Pia,
Rais Magufuli amelikamua jipu udanganyifu kwenye miamala ya simu.
Alisema amebaini kuwa makampuni ya simu yamefanya miamala yenye thamani
ya shilingi trilioni 5.5 ambayo haikukatwa kodi, mwezi Machi mwaka huu.
Aliwataka TCRA kushirikiana na BOT kuhakikisha wanalishughulikia suala hilo na kurejesha fedha za serikali kupitia kodi.
Rais
Magufuli pia aliyanyooshea kidole maduka ya kubadilishia fedha za
kigeni akiitaka BOT kuyasimamia kwa ukaribu ili yasiwe kichochoro cha
kupitishia fedha za dawa za kulevya ama fedha ambazo zinavushwa
kinyamela.
Kadhalika,
Rais Magufuli aliwataka BOT kuhakikisha kile walichomueleza kuwa
wamewezesha kushuka kwa mfumuko wa bei kwa kutoka asilimia hadi asilimia
5.2 kionekane kwa uhalisia ka wananchi na sio kuishia kwenye maandishi.
“Je, [kushuka huko]kumefika kwa wananchi au kumeishia kwenye makaratasi tu? Je, bidhaa za miaka ya 90 na sasa ni sawa?” Rais Magufuli anakaririwa.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli amemuagiza Gavana wa BOT, Profesa Benno
Ndulu kuifuta Benki ya Twiga Bancorp kwakuwa imekuwa ikijiendesha
kihasara huku ikivunja sheria.
Alimtaka Gavana Ndulu kuzichukulia hatua Benki zote zenya muelekeo huo hata kama ni za Serikali.
“Unakwenda
Benki unakuta kuna negative (hasi) bilioni 18, mimi nasema katika
utawala wangu sitabembeleza Benki isiyofanya vizuri hata kama ni ya
Serikali. Kuna Benki moja inapambwa na CCM lakini….” Rais Magufuli alisikika japo hakuitaja Benki hiyo.
Rais
Magufuli pia aliitaka BOT kuhakikisha Benki zinaweza kutoa mikopo yenye
riba nafuu ili kunusurua taasisi na wananchi wanaokopa katika benki
hizo.
Naye
Gavana Ndulu alimhakikishia Rais Magufuli kuwa wanaunga mkono juhudi
zake na kumkabidhi mfano wa hundi ya shilingi bilioni 4 ambayo watatoa
kwa serikali kuchangia madawati katika shule za msingi na sekondari
nchini. Gavana ndulu alisema kuwa fedha hizo zimepatikana kutokana na
kubana matumizi.
0 comments:
Post a Comment