Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha akizungumza na waandishi wa habari LEO kuhusu hospitali hiyo kuanza kuboresha huduma ya chakula kwa wagonjwa (special diet) wanaolazwa MNH kuanzia Julai Mosi, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Uuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Agness Mtawa akifafanua jambo LEO katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu hospitali hiyo kuanza kuboresha huduma ya chakula kwa wagonjwa. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma, Aminiel Aligaesha akiwa kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa MNH, Aligaesha akifafanua jambo kwenye mkutano na waandishi wa habari LEO jijini Dar es Salaam.
Yawaondolea usumbufu ndugu wa wagonjwa kupeleka chakula mara tatu kwa siku.
· Ndugu watapata muda wa kuendelea na shughuli za uzalishaji
Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) imeboresha huduma za chakula kwa wagonjwa wote
watakaolazwa kuanzia Julai Mosi, mwaka huu ili kuwaondolea ndugu wa
wagonjwa usumbufu na gharama za usafiri wakati wa wanapokwenda kuwaona
ndugu zao waliolazwa mara tatu kwa siku katika hospitali hiyo.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar Es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano ya Umma, Hospitali ya Taifa Muhimbili Bw. Aminiel Aligaesha
amesema hospitali imeingia ubia na mzabuni ili kutoa huduma hiyo kwa
wagonjwa wote wanaolazwa.
Kwanini Hospitali imechukua hatua hii
Bw. Aligaesha amesema Hospitali inataka kujikita katika majukumu yake ya msingi ambayo ni kushauri, kuchunguza na kutibu.
“Aidha
Hospitali inataka kuwaondelea adha ndugu wa wagonjwa ambao wamekuwa
wakiingia gharama kubwa hususani usafiri wa kuja Hospitalini mara tatu
kwa siku, ambapo kwa kukadiria gharama ya usafiri wa ndugu mmoja wa
mgonjwa ni kati ya shilingi 6,000/= na 10,000/= kwa siku, kulingana na
mahali anapotokea bila kujumuisha gharama za kuandaa chakula cha mgonjwa
ambacho mara nyingi ni chakula maalumu. Na kama mgonjwa akilazwa zaidi
ya siku tano hadi 10 ndugu mmoja wa mgonjwa gharama atalipia fedha
nyingi kwenye usafiri” amesema Bw. Aligaesha
Ameongeza
kuwa adha ya pili wanayopata ndugu ni usumbufu ambapo inabidi kuacha
shughuli nyingine za uzalishaji ili kuja kuleta chakula mara tatu kwa
siku, hivyo kuingiliana na shughuli zao za kiuchumi na kimandeleo na
kushindwa kuzalisha. Hivyo jukumu hili linachukuliwa na Hospitali
kuwaondolea adha hii.
“Pia
kuna baadhi ya ndugu wamekuwa wakishindwa kuwaletea chakula wagonjwa wao
hivyo hospitali ililazimika kuwapatia chakula ambacho kilikuwa kwa
ajili ya wagonjwa wanaotoka mikoani wasio na ndugu hapa Dar Es Salaam”
amesisitiza Bw. Aligaesha.
Amesema
kumekuwepo na ongezeko la msongamano wa watu ndani ya Hospitali toka
asubuhi saa 12 mpaka saa 12 jioni, suala linaloingiliana na utoaji
huduma hasa saa za mchana kwani muda wa saa 6.00 hadi saa 8.00 mchana
ulikuwa unaingiliana na majukumu ya kiutendaji ambapo majopo mbalimbali
ya watalaamu yamekuwa yakiendelea na raundi za wagonjwa waliolazwa. Hii
wakati mwingine imesababisha mgonjwa kutokupata huduma stahiki kutokana
na muingiliano huu.
·
“Vile
vile msongamano huu ni changamoto kwa ajili ya masuala ya kiusalama
ambapo kati ya watu wanaoingia Hospitali kwa kigezo cha kuja kuona
wagonjwa kuna wanaoingia kwa lengo la kufanya uhalifu ikiwemo wizi wa
mali za Hospitali, magari pamoja na vifaa vya magari” alisisitiza.
Amesema
kwa kufanya hivyo, Hospitali itapunguza baadhi ya gharama za uagizaji
wa vyakula kwa wazabuni, kulinda upotevu na baadhi ya vyakula kuharibika
wakati mwingine kwani utunzaji wa vyakula una mahitaji makubwa.
Bw.
Aligaesha amesema Hospitali inakusudia kutoa chakula chenye ubora na
viwango vinavyotakiwa kwa wagonjwa ikiwemo kutoa chakula maalumu
(special diet) kwa wagonjwa wenye uhitaji huo.
Utaratibu wa chakula cha mzabuni kwa wagonjwa
Kuhusu
utaratibu huo Bw. Aligaesha amesema Mzabuni ndiye atakayepika chakula
kwa wagonjwa wote waliolazwa na atatayarisha, atakipeleka na kukikabidhi
katika wodi husika ambapo jukumu la kumpa mgonjwa kifungua kinywa,
chakula cha mchana na jioni linabaki wa Hospitali.
Amesema wagonjwa watapatiwa milo mitatu kwa siku yaani asubuhi, mchana
na jioni kazi itakayofanywa na muuguzi wa zamu ambaye atahakikisha
wagonjwa wote wamepata chakula kufuatana na mahitaji (diet list)
iliyowasilishwa jikoni kutokana na mahitaji yao ya kiafya.
Muda wa kuona wagonjwa
Kutokana
na uamuzi huu, utaratibu wa ndugu kuleta chakula kwa wagonjwa
waliolazwa wakati wa mchana umefutwa na hivyo mchana hatutakuwa na
nafasi ya ndugu kuja kutembelea wagonjwa. Muda wa kutembelea wagonjwa
utakuwa asubuhi saa 12 hadi saa moja kamili na saa 10:00 jioni hadi saa
12:00jioni ndipo ndugu wataruhusiwa kuingia ndani kuwaona ndugu zao
waliolazwa. Katika muda huo ndugu ataruhusiwa kuja na chakula chochote
anachofikiri atamuongezea mgonjwa wake kama matunda n.k
Uchangiaji huduma ya chakula
Bw.
Aligaesha amesema mgonjwa aliyelazwa atachangia kiasi cha shilingi
50,000 atakapolazwa ambapo kati ya hizo, shilingi elfu 10,000 itakuwa ni
gharama ya kumuona daktari (Consultation), shilingi elfu 10,000 ikiwa
ni gharama ya kulazwa na bei ya chakula itakuwa shilingi elfu 30,000
sawa na shilingi elfu 6,000 kwa siku. Wastani wa mgonjwa kukaa wodini ni
siku tano. Gharama hizo zinahusika kwa muda wote atakaokuwa amelazwa.
Kwa
sasa Hospitali inatoa chakula kwa wagonjwa 650 ambao wamepata rufaa
kutoka hospitali za nje ya mkoa wa Dar es Salaam kwa gharama wastani wa
shilingi 1.8 bilioni kwa mwaka, sawa na shilingi 150 milioni kwa mwezi
kwa vyakula pamoja na gharama nyingine kama vile za nishati. Takribani
wagonjwa kati ya 600 na 700 ambao rufaa zao ni kutoka Hospitali za Dar
es Salaam walikuwa hawapati chakula kutoka Hospitalini, na ilibidi ndugu
zao wawaletee chakula. Hata hivyo, Hospitali ilikuwa inawapatia chakula
tu kama ndugu zao wakishindwa kufanya hivyo.
Hitimisho.
“Uongozi
wa Hospitali unaamini kwamba mabadiliko haya hayatamuongezea mgonjwa
gharama, bali yatampunguzia gharama pamoja na ile adha kama
ilivyoainishwa hapo juu. Aidha, uongozi unaamini kwamba uamuzi huu
unaendana na azma nzima ya kuboresha utoaji huduma katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili na kuboresha mazingira ya Hospitali. Tunaomba
ushirikiano wenu katika kutekeleza jukumu hili ili kusudi wagonjwa
waweze kuhudumiwa vizuri zaidi” amesisitiza Bw. Aligaesha.
0 comments:
Post a Comment