Mwenyekiti wa Kampuni za Quality Group Limited (QGL), Yusuf Manji amesema bado anasubiria majibu kutoka kwa Rais John Magufuli juu ya sakata la kuendeleza ufukwe wa Coco, maarufu Coco Beach uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam baada ya kumwandikia barua Desemba mwaka jana.
Manji
alisema anatamani suala hilo limalizike kabla ya kuondoka rasmi katika
kampuni hiyo mwezi ujao, na kwamba tayari alishamwandikia barua kiongozi
huyo wa nchi juu ya usahihi wa mchakato wa zabuni wa kuendeleza eneo
hilo la ufukwe wa Bahari ya Hindi.
Mfanyabiashara
huyo anasema anashangazwa na baadhi ya viongozi wa Serikali
kurudiarudia suala hilo na kusababisha kuwa maarufu kuliko hata Benki
Kuu ya Tanzania (BoT).
Kwa
mujibu wa mfanyabiashara huyo, suala la Coco Beach ilikuwa ni sehemu ya
biashara na kwamba zabuni hiyo walishinda baada ya kutimiza masharti
yaliyokuwa yamependekezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni,
lakini cha kushangaza hali imekuwa tofauti.
Mfanyabiashara
huyo alifikia hatua hiyo kufuatia Rais John Magufuli kutangaza eneo
hilo liendelee kutumika na watu wa kawaida kwa kile alichosema kuwa kuna
mfanyabiashara ambaye anatumia fedha kuwahonga baadhi ya watumishi wa
halmashauri hiyo ili kumiliki eneo hilo.
Rais Magufuli ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa wafanyabiashara alisema;
“Inanifadhaisha sana kuona mfanyabiashara tajiri akihonga maofisa
kutumia vibaya fedha za umma kwa manufaa yake binafsi na wakazi kutoka
mazingira duni wakishindwa kutumia ufukwe huo kuogelea na kuburudika.”
Hata
hivyo, Manji alisema kuwa kampuni yake ilikuwa ikilihitaji eneo hilo
kuliendeleza kwa ajili ya biashara na kuhudumia wananchi hivyo iwapo
Rais ataridhia linyang’anywe licha ya kushinda zabuni na mahakamani,
hawatakuwa na hatua nyingine ya kufanya.
Alisema
Rais aliyasema yake na Mahakama ilishafanikisha ushindi wa awamu ya
kwanza na Serikali baadaye ilikata rufaa na kwamba mtu yoyote akitaka
kusoma kwa nini walishinda kesi ya awali, hukumu iliyotolewa inajieleza.
Manji
alieleza kuwa ingekuwa eneo lile linahitajika kwa matumizi binafsi hata
wangemwambia aliachie na achukue Jangwani angekubali, lakini kampuni
isingekubali kwa sababu eneo lile lilitafutwa kwa ajili ya biashara na
mbadala wowote huenda usiwavutie wanahisa.
“Coco
Beach siyo nyumbani kwangu na wala siyo sehemu ambayo lazima niwe nayo
au nisiwe nayo. Ni sehemu ambayo kampuni ilihitaji kwa ajili ya
uwekezaji,” alisema Manji.
“Wanahisa
walitaka kuwekeza lakini iwapo halitapatikana, hawajatufungia milango
ya kiuwekezaji kwa kuwa Coco Beach siyo sehemu moja tu duniani ya
kuwekeza.”
Tayari
QGL ilishaingia ubia na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) mwishoni
mwa mwaka jana kutekeleza mradi wa Dola 250 milioni za Marekani (Sh537.5
bilioni) kuendeleza eneo la Bwawani, kwa kuikarabati hoteli hiyo na
kujenga mji wa kisasa ambao utakuwa na huduma zote za kisasa katika
visiwa hivyo.
0 comments:
Post a Comment