Polisi jana walipiga kambi kwa saa saba kwenye geti la nyumba ya Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, wakitaka kumkamata bila ya mafanikio.
Polisi hao walikuwa kama wageni wa askofu huyo wakisubiri wafunguliwe geti, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:10 jioni walipoamua kuondoka wakitumia gari aina ya Toyota Landcruser lenye namba za kiraia, ambalo kwa muda wote huo lilikuwa limeegeshwa pembeni mwa geti hilo.
Hii
ni mara ya pili katika kipindi cha takriban miezi 16, kwa askari wa
jeshi hilo kwenda nyumbani kwa askofu huyo na kushinda mbele ya nyumba
yake kwa saa kadhaa, kabla ya kuondoka bila ya kumtia nguvuni.
Tukio
hilo pia linatokea wakati kukiwa kumesambaa mkanda unaotoa sauti ya
Askofu Gwajima, ikizungumzia kitendo chake cha kuamua kumuunga mkono
Rais John Magufuli na kumshutumu Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne,
Jakaya Kikwete ikiitaka afikishwe mahakamani kwa yote yaliyofanyika
wakati wa utawala wake ambayo Rais wa sasa anayashughulikia.
Jana,
mbele na nyuma ya gari hilo kulikuwa na askari waliokuwa wamevalia
kiraia, kila mmoja akionekana kama anafanya shughuli tofauti, lakini
wote wakionekana kuwa na lengo moja; kusubiri kufunguliwa lango la
nyumba ya Askofu Gwajima.
Mbele
ya nyumba walikuwapo askari watatu na raia wawili, mmoja mwanamke na
mwingine mwanamume ambao baadaye ilibainika kuwa walikuwa wamezuiwa na
askari hao baada ya kuonekana wakitokea mlango wa nyuma wa nyumba hiyo.
Mwandishi
alishuhudia mwanamke huyo akiitwa na askari aliyekuwa ndani ya gari na
kuonywa kuepuka kutumika, kisha akarudishiwa simu yake ambayo walikuwa
wakiishikilia.
Raia
hao walisema, walifika kwenye nyumba hiyo kwa ajili ya kufanya tathmini
ya matengenezo na baada ya kumaliza walipokuwa wanatoka wakakutana na
askari hao na kukamatwa.
Askari
hao wasikika wakisemezana kuwa kuna taarifa zinasambazwa kwenye simu
kuwa nyumba ya kiongozi huyo wa kiroho, ambaye aliibuka kuwa maarufu
mwishoni mwa mchakato wa Katiba Mpya, imezingirwa, wakati hakukuwa na
kitu kama hicho.
Pia, askari hao walisikika wakieleza kushangazwa na kitendo cha wenyeji kutowafungulia geti hilo ili waingine.
“Mtu kama huna tatizo; ni raia mwema. Una sababu gani ya kukataa kufungua mlango? Afungue akutane na sisi wageni wake,” alisema mmoja wa askari hao wakati wakiongea baina yao.
“Tumekuja bila silaha, tunataka kuzungumza naye, hataki kufungua mlango, anataka nini sasa?” alihoji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alipoulizwa alisema hajatuma askari yeyote nyumbani kwa Gwajima.
“Wapigie makamanda wengine kwa sababu si kila anayeishi Kinondoni amefanya kosa Kinondoni,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema wanamuhitaji askofu huyo.
“Kama uko na Gwajima mwambie tunamuhitaji.” Alipoulizwa wanamuhitaji kwa sababu gani, Kamanda Sirro alisema: “Tumepata
clip (mkanda) inayosemekama ni ya kwake. Tunamtaka athibitishe kama
hayo maneno ni ya kwake. Na kama ni yeye ameyasema, anaelewa nini kuhusu
kile alichokizungumza kwa sababu hayo maneno ni ya kichochezi. Tupo
kwenye uchunguzi .”
Askofu Gwajima si mgeni wa matukio kama hayo dhidi ya mamlaka.
Mwaka
2012 aliingia kwenye mzozo na Jeshi la Polisi baada ya kijana mmoja
kudai amejisalimisha kanisani kwake kutubu, baada ya kushiriki kwenye
tukio la kumteka kiongozi wa madaktari, Dk Steven Ulimboka.
Hata
hivyo, Askofu Gwajima aliekeza kuwa kijana huyo hakuwahi kufika kwenye
kanisa hilo, wala kukutana naye na kwamba taarifa hizo zililenga
kuchafua kanisa lake.
Mwaka
2015, Askofu Gwajima aliingia kwenye mgogoro mwingine na Jeshi la
Polisi baada ya mkanda wa sauti ya mahubiri kanisani kwake kutoa maneno
yaliyoonekana kukashifu msimamo wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa
Katoliki Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo dhidi ya tamko la
maaskofu wa Jukwaa la Wakristo la kuwataka waumini wao wasipige kura ya
maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Katika
sakata hilo, Askofu Gwajima alifunguliwa shtaka la kutoa lugha ya
matusi dhidi ya Kardinali Pengo, na kushindwa kuhifadhi silaha na risasi
wakati akiwa hospitalini.
Kabla
ya kufunguliwa mashtaka hayo, askari walizingira nyumba yake kwa
takriban saa saba, lakini hawakufanikiwa na siku iliyofuata kiongozi
huyo alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam.
Akiwa
huko aliugua na baadaye kulazwa. Polisi walitangaza kukamata watu 15
wakiwatuhumu kuwa walikuwa na mpango wa kumtorosha na kukamata silaha
hiyo pamoja na risasi walizodai walizikuta kwenye gari.
0 comments:
Post a Comment