Thursday, 16 June 2016

#YALIYOJIRI>>>Sakala la Kumshitaki Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Laibua Mjadala Mzito.Fahamu zaidi hapa.

Kauli ya mwanahabari nguli nchini, Jenerali Ulimwengu kutaka Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ashtakiwe mahakamani kwa kuitia hasara Serikali imeibua mjadala mzito, huku wasomi wakisema ipo haja ya kubadili Katiba ili mkuu wa nchi aweze kushtakiwa baada ya kuondoka madarakani. 

Wasomi hao walisema ile kauli ya “hakuna aliye juu ya sheria” inapaswa kufuatwa na watu wote, wakitolea mfano Rais wa Brazil, Dilma Roussef aliyeng’olewa na Bunge baada ya kutuhumiwa kukiuka sheria za usimamizi wa akaunti ya bajeti ya nchi hiyo.
Kwa sasa nafasi yake inashikiliwa na aliyekuwa makamu wake, Michel Temer.

Hata hivyo, baadhi ya wasomi wamesema jukumu hilo la kumshtaki rais mstaafu inafaa liachwe mikononi mwa Bunge. 
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imempa kinga rais mstaafu ya kushtakiwa kwa jambo lolote alilofanya alipokuwa madarakani na imetoa mlolongo mrefu rais aliyeko madarakani kuondolewa. 

Juzi wakati akizungumza katika Tamasha la Nane la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Jenerali ambaye pia ni mwanasheria wa kujitegemea alisema Kikwete anapaswa kushtakiwa kwa kuisababishia hasara Serikali kutokana na kuruhusu mabilioni ya shilingi kutumika katika mchakato wa Katiba ambayo haikupatikana. 

Mbali na fedha zilizotumiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati wa kukusanya maoni, kununulia magari, kulipia pango la ofisi, nyingine zilitumika kurekebisha ukumbi wa Bunge uweze kubeba wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, na kulipa posho ya Sh300,000 kwa siku kwa wajumbe 620 kwa muda wa siku 130. 

“Itabidi (Kigoda cha Mwalimu) mumuite (Kikwete) mwaka ujao, aje aeleze fedha za wananchi zilizotumika katika mchakato ule zilikuwa na sababu gani,” alisema huku akishangiliwa na umati wa watu. 

Jenerali aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya za Hai na Ilala na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, alisema kama mawaziri wa zamani wamepandishwa kizimbani kwa kusababisha hasara, hata Kikwete anapaswa kupelekwa mahakamani kwa kusababisha hasara kwa Serikali na kuzima matumaini ya wananchi, jambo linaloweza kusababisha machafuko nchini. 

Ibara ya 46 sehemu ya (1) ya Katiba inasema wakati wote Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, itakuwa ni marufuku kumshitaki au kuendesha mashataka ya aina yoyote juu yake mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai.

Sehemu ya (3) inasema isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na masharti ya ibara ya 46A (10), itakuwa ni marufuku kumshtaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la kumdai mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo lolote alilofanya yeye kama Rais wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais kwa mujibu wa Katiba hii. 

Ibara ya 46A sehemu ya (1) inasema bila ya kujali masharti ya ibara ya 46 ya Katiba hii, Bunge linaweza kupitisha azimio la kumuondoa Rais madarakani endapo itatolewa hoja ya kumshtaki Rais na ikapitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii. 

Sehemu ya (2) imeweka masharti kwamba bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibara hii, hoja yoyote ya kumshtaki Rais haitatolewa isipokuwa tu kama inadaiwa kwamba Rais; (a) ametenda vitendo ambavyo kwa jumla vinaivunja Katiba au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma; (b) ametenda vitendo ambavyo vinakiuka maadili yanayohusu uandikishwaji wa vyama vya siasa yaliyotajwa katika ibara ya 20 (2) ya Katiba. 

Mbali ya Katiba ya sasa kumwekea kinga Rais mstaafu, Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba na Katiba Inayopendekezwa zilinakiri kipengele hicho kinachompa Rais mstaafu kinga ya kutoshtakiwa bila kubadili chochote. 
Maoni ya wasomi  Mhadhiri wa Shule ya Siasa ya Chuo Kikuu  Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse alisema ili kuondoa kile alichokiita ‘kusumbuliwa’, jukumu la kumshtaki Rais mstaafu au aliyepo madarakani linapaswa kuachwa mikononi mwa Bunge. 

“Katiba imeeleza wazi kwamba ataondolewa madarakani kwa azimio la Bunge. Binafsi nadhani utaratibu huo ndiyo mzuri hata kama atakuwa amemaliza muda wake, hoja ya kumshtaki ianzie bungeni,” alisema . 

Naye Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Innocent Shoo alisema, “Tukizingatia demokrasia za kisasa, rais akitoka madarakani hapaswi kuwa na kinga ya kushtakiwa. Hii inatakiwa iwezekane hata akiwa madarakani ili kuzingatia utawala wa sheria.” 

Katika ufafanuzi wake, Shoo alisema kuwa kutokuwajibika na utamaduni wa kutokujali ni utambulisho wa viongozi wengi barani Afrika huku akinukuu kauli ya Rais wa Marekani, Barack Obama, kwamba “Afrika inatakiwa kuwa na taasisi imara siyo mwanaume mwenye nguvu.” 

Shoo alisema nchi nyingi barani Afrika hazina chaguzi huru, haziheshimu haki za binadamu na uhuru wa watu na taasisi mbalimbali, mambo aliyodai kuwa yanafaa kumfanya Rais kushtakiwa. 

“Umeona kilichotokea Brazil? Ule ni mfano hai kuwa rais anaposhindwa kufuata sheria na taratibu ashtakiwe tena ashtakiwe hata akiwa madarakani,” alisisitiza. 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Profesa Damian Gabagambi alisema, “Anapaswa kushtakiwa anapomaliza utawala wake na hasa kama wakati akiwa rais alikuwa akifanya mambo ya kulihujumu taifa.” 

Profesa Gabagambi ambaye alikuwa mmoja wa wataalamu walioandaa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), alisema kushtakiwa siyo kufungwa kwa kuwa mtuhumiwa atakwenda mahakamani na kujitetea. 

“Hii itasaidia viongozi wakati wa utawala wao kuheshimu utawala bora na kufuata sheria na Katiba ili kukwepa kushtakiwa, mara wamalizapo kipindi chao cha kuongoza,” alisema. 

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch alisema Katiba inampa Rais kinga ya maisha, jambo ambalo si sahihi huku akieleza kuwa wazo la Kikwete la kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya lilikuwa zuri ila liliharibiwa na wanasiasa. 

“Kinga aliyonayo rais ndiyo inayompa kiburi na ndiyo sababu akiwa madarakani akishauriwa hataki, ila akimaliza muda wake anajuta kwa uamuzi aliouchukua,” alisema Olouch huku akisisitiza kuwa hayo ni maoni yake binafsi si ya CWT. 

Akitolea mfano wa kilichomkumba Rais wa Brazil, Oluoch ambaye alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, alisema hata kama nchi nyingine nazo zina kinga kwa marais wao, si lazima Tanzania kubaki na kinga hiyo kwa kuwa kila nchi ina utamaduni na ustaarabu wake. 

“Rais wa Tanzania yupo juu ya sheria. Mfano Benjamin (MkapaRais wa Awamu ya Tatu) amesema anajutia uamuzi wake wa ubinafsishaji na kutowekeza katika elimu. Hayo ni baadhi tu ya makosa wanayoyafanya viongozi wetu,” alisema Oluoch. 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala alisema kuondoa kinga ya Rais baada ya utawala wake ni hatari kwa usalama na demokrasia ya nchi. 

Alisema kwa kuwa kila kiongozi hufanya maamuzi ya kisiasa ambayo wakati mwingine hayatimii, kuondolewa kwa kinga hiyo kunaweza kukaleta matatizo ya kisiasa kwa siku za mbele.

 “Kuna mtu atakuja kung’ang’ania ikulu endapo atatambua kuwa yupo kwenye hatari ya kufikishwa mahakamani,” alisema Profesa Mukandala na akashauri zianzishwe taasisi makini na imara zitakazokuwa zinamshauri Rais juu ya maamuzi mbalimbali anayoyafanya akiwa madarakani. 

Alisema hakuna haja ya kuwafikisha mahakamani viongozi wa ngazi hiyo, kama makosa yao yalitokana na mtazamo wa kisiasa na kukumbusha kuwa hata Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere alishindwa kutekeleza mkakati wa kuanzisha Vijiji vya Ujamaa kama ulivyoratibiwa sawa na ilivyotokea kwenye Katiba Mpya kipindi cha Rais Kikwete. 

Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, kimeunga mkono kauli ya Jenerali kuhusu Kikwete kushtakiwa kuhusiana na mchakato wa Katiba ambayo haikupatikana. 
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani alisema CUF inaunga mkono kwa asilimia 100 kauli hiyo, kwa sababu sehemu kubwa ya matatizo yaliyojitokeza na yanayojitokeza Zanzibar yamesababishwa na kutopatikana kwa Katiba Mpya. 

“CUF tungekuwa na uwezo hata leo tungetaka ashtakiwe haraka iwezekanavyo. Kwa sababu Kikwete ni mmoja wa watu aliyevuruga uchaguzi Oktoba 25, mwaka jana,” alisema Bimani. 

Lakini Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vua Ali Vuai alisema maoni ya Jenerali si sahihi na si ya kiungwana kwa kuwa yana lengo la kuleta uchochezi kwa wananchi dhidi ya Kikwete. 

“Huu ni upotoshaji kwa wananchi, kwa sababu Kikwete amefanya mambo makubwa nchini. Sioni sababu ya kusema fedha nyingi zimetumika wakati mchakato huu bado unaendelea, ukisubiri kupiga kura za maoni.

0 comments:

Post a Comment