Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo, Bungeni Mjini Dodoma amewataka wabunge
wa upinzani ambao wamesusia vikao vya Bunge tangu Mei 30 kuingia Bungeni
na kuacha kususia vikao vya Bunge kwani hakuna tija kwa Taifa.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akitoa hutuba ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la kumi na moja.
“Kitendo
cha baadhi ya waheshimiwa wabunge kususia vikao vya Bunge hakitoi picha
nzuri kwa wananchi waliotuchagua kuwasilisha matatizo yao katika Bunge
hili, hivyo natoa rai kwa waheshimiwa wabunge hao kutafakari upya uamuzi
wao na niwasihi kwa busara zao waingie ili kwa pamoja na kwa
ushirikiano tuweze kutoa ushauri kwa Serikali,” alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha
Mhe. Majaliwa alitoa ufafanuzi juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 ambayo imetoa haki na kinga kwa waheshimiwa
wabunge ili kujadili na kuhoji utendaji wa Serikali kwa uhuru bila
mashaka yoyote ya kuweza kushitakiwa wanapotimiza wajibu wao wakiwa
Bungeni.
Aliendelea
kwa kusema kuwa kinga ya aina hiyo haijatolewa kwa mwananchi yeyote
yule Nchini ila kwa Wabunge, hivyo basi hakuna mbunge aliyefungwa mdomo
labda aamue kujifunga mdomo yeye mwenyewe.
Mhe.
Majaliwa amesema kuwa Bunge linaongozwa na Katiba, Sheria na Kanuni za
Kudumu za Bunge, hivyo ni vyema zikafuatwa kuondoa manung’uniko yasiyo
ya lazima na endapo kuna utata katika jambo lolote ndani ya Bunge zipo
taratibu zilizowekwa na kanuni za kufuata ili kupata ufumbuzi na si kwa
kususa kuingia Bungeni kwani hakuna tija kwa Taifa.
Wabunge wa upinzani wamesusia vikao vya Bunge tangu Mei 30, 2016 mpaka leo Juni 30 ambapo Bunge limehitimishwa.
Aidha
wabunge hao wamekuwa wakiingia Bungeni kila asubuhi na jioni kisha
kutoka mara tu Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson anapomaliza kusoma Dua
maalum la kuliombea Bunge na Taifa.
0 comments:
Post a Comment