MFANYABIASHARA
Alex Msama amemuomba radhi Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison
Mwakyembe kufuatia habari mbili zilizochapishwa katika Gazeti la Dira ya
Mtanzania analolimiliki.
Akizungumza
leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msama alisema
amejiridhisha kuwa habari hiyo iliyobeba kichwa cha habari ‘Utapeli wa
Mwakyembe wamwagwa hadharani’ haikufuata misingi ya uandishi wa habari.
Habari
nyingine ambayo imeonekana kumchafua Dk Mwakyembe ni ile ya Mwakyembe
atuhumiwa kutapeli bilioni 2 ambazo zimemuumiza kiongozi huyo.
Alisema
yeye kama mmiliki wa gazeti hilo amesikitishwa na habari hiyo na kwamba
hatua ya kwanza anayoichukua ni kumuomba radhi Waziri Mwakyembe.
Msama alisema sambamba na kuomba radhi atamfikishia barua Mwakyembe ya kumtaka radhi kwa tukio hilo.
“Nimesikitishwa
na habari hii kwa kuwa haikuzingatia misingi ya uandishi wa habari,
ilihukumu na kuonyesha kuwa lengo lake lilikuwa kumharibia jina Waziri
Mwakyembe, ninachukua nafasi hii kumuomba radhi nikiwa mmiliki wa gazeti
hilo,” alisema Msama.
Aidha
Msama alisema hatua nyingine anayochukua ni kumsimamisha kazi mhariri
wa gazeti hilo, Mussa Mkama kwa kuwa alishindwa kufanya kazi yake kwa
umakini ya kuhakikisha habari anazozipitisha zinafuata misingi ya
uandishi wa habari na weledi.
Alisema
Mkama alipaswa kuhakikisha anafuata weledi lakini alishindwa kufanya
hivyo kwa hiyo anamsimamisha kazi na kwamba hatua nyingine kali za
kinidhamu zitafuata.
“Mimi
ni mfanyabiashara sijui mambo ya uandishi, nilimuajiri nikiamini
atasimamia yale aliyofundishwa chuoni, kwa kuwa ameshindwa inabidi akae
pembeni kwanza,” alisisitiza Msama.
Ameahidi kuwa katika Gazeti la Dira ya Mtanzania litakalotoka Juni 27, kwa ukubwa uleule atamuomba radhi Waziri Mwakyembe.
Hivi
karibuni Waziri Mwakyembe aliitisha mkutano wa waandishi wa habari
mjini Dodoma akilalamikia kuwa habari mbili za gazeti hilo
iliyochapishwa na Gazeti la Dira ya Mtanzania la Juni 20 na la Juni 23
mwaka huu zililenga kumchafua na kuahidi kuwa atalishtaki kupitia habari
hizo mbili.
0 comments:
Post a Comment