RAIS
Paul Kagame wa Rwanda atafanya ziara rasmi ya kitaifa nchini Julai mosi
mwaka huu ambayo pamoja na mambo mengine, atafungua Maonesho ya 40 ya
Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba siku hiyo
kutokana na mwaliko rasmi wa Rais John Magufuli.
Akitoa
taarifa rasmi ya serikali jana Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Dk Augustine Mahiga alisema
ziara hiyo ni mwendelezo wa uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili.
Alisema
Rais Magufuli amemualika Rais Kagame kuja nchini kutokana na ziara yake
aliyoifanya nchini Rwanda mapema Aprili mwaka huu ambayo pamoja na
mambo mengine, marais hao walikubaliana kushirikiana kwenye nyanja
mbalimbali.
“Rais
Magufuli amenituma kuwaambia umma kwamba amemwalika Rais Kagame kuja
nchini kwa ziara ya kitaifa ambapo atafungua Maonesho ya Sabasaba na pia
watasaini mkataba wa makubaliano kwenye mambo waliyoafikiana wakiwa
Rwanda,” alisema Balozi Mahiga.
Katika
ziara ya Rais Magufuli nchini Rwanda ambako yeye na Rais Kagame
walifungua Daraja la Rusumo lililo mpakani mwa nchi hizo, viongozi hao
waliafikiana kuendeleza ushirikiano katika sekta tofauti ikiwemo
biashara.
Hata
hivyo, marais hao waliwataka wataalamu wa nchi hizo mbili kukaa pamoja
na kujadiliana kwa kina mambo waliyozungumza ya ushirikiano, na ujio wa
Rais Kagame nchini una lengo pia la kuweka saini ya makubaliano baina
yake na Rais Magufuli kwenye Mkataba wa Makubaliano wa ushirikiano wa
mambo waliyoafikiana.
Aidha,
Balozi Mahiga alisema baada ya Rais Kagame kusaini mkataba huo na
mwenyeji wake na kufungua maonesho hayo, jioni ataungana na Rais
Magufuli kwenye dhifa itakayoandaliwa Ikulu.
Ziara
yake nchini Rwanda ilikuwa ya kwanza nje ya nchi kwa Rais Magufuli
tangu achaguliwe kuiongoza Tanzania na kuapishwa Novemba 5, mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment