WACHEZAJI wa zamani wa Yanga na Simba
wameitaka Yanga kutobweteka katika mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho
Afrika dhidi ya TP Mazembe na badala yake watulie na kutumia vyema
uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti ,
wachezaji hao walisema Yanga ilionesha kandanda nzuri katika mchezo
dhidi ya Mo Bejaia isipokuwa safu ya ushambuliaji haikucheza kwa
utulivu.
Miongoni mwa wachezaji hao ni Mwanamtwa
Kihwelu na Moses Mkandawile waliosema kuwa Yanga inaweza kupata matokeo
mazuri iwapo kama hawatabweteka, na ikiwa watapambana kwa ushirikiano.
Kihwelu alisema: “TP Mazembe sio timu
nyepesi kwani ina uzoefu wa mashindano hayo, na tayari wana pointi tatu
na kuhimiza Yanga kutulia kwenye uwanja wa nyumbani kutengeneza nafasi
zenye kuzaa matunda.”
Alisema kinachohitajika ni mabingwa hao
wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuzidisha mara mbili kiwango chao ili kuwa na
uhakika wa kuibuka na ushindi. Kihwelu alipendekeza kuwa iwapo Juma
Abdul na mchezaji mpya Obrey Chirwa watakuwepo kuna uwezekano wa kupata
ushindi mzuri.
Kwa upande wake, Mkandawile aliwahimiza
Yanga kucheza wakijua kuwa wako kwenye uwanja wa nyumbani. Alisema ni
muhimu kuzingatia nidhamu kwa ajili ya kuepukana na kadi nyingi
zisizokuwa na tija .
Golikipa huyo wa zamani wa Simba
alisema sehemu inayohitaji kufanyiwa kazi ni safu ya ulinzi na
ushambuliaji, kwani wanahitaji kucheza kwa utulivu mkubwa. Yanga
wanatarajiwa kushuka dimbani Juni 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam katika mchezo wa pili hatua ya makundi. Kwa sasa
wanaendelea kujifua na mazoezi katika kambi yao iliyoko nje ya nchi
Uturuki na kesho wanatarajiwa kurudi.
0 comments:
Post a Comment