Katibu Mkuu wa Chama cha Ada Tadea, John Shibuda amesema Rais
John Magufuli “ni katili kwa wahujumu wa ustawi na maendeleo ya Taifa na
rafiki kwa waadilifu”, na kuwataka Watanzania kumuunga mkono kwa
ukatili huo ambao amesema unabezwa na baadhi ya watu.
Shibuda, ambaye alikuwa mbunge wa Maswa Magharibi kwa tiketi ya
Chadema na CCM kwa vipindi tofauti, alisema hayo jana wakati akizungumza
na waandishi wa habari mjini Shinyanga.
Alisema wanaodai Rais Magufuli ni dikteta hawajui viwango vya
ubora wao katika kutoa hukumu hiyo na kuwataka kuchagua kupendezesha
waadilifu ili kwenda peponi au waovu waliojipanga kwenda jehanamu.
“Ndugu zangu ukweli haulogeki. Mahimizo ya Rais si udikteta,
bali ni dhamira ya kuibua msisimko wa uhuru na maendeleo na uhuru ni
kazi na asiyefanya kazi asinufaike na jasho la Watanzania,” alisema
Shibuda ambaye anasifika kwa uwezo wake wa kutumia vizuri lugha ya
Kiswahili.
Shibuda alisema kama Magufuli ni katili, basi dini zote ni
katili kwa kuwa zina amri za Mungu ambazo zinawakataza watu kufanya
mambo wanayoyapenda.
Alisema ndiyo maana viongozi wa dini nao wamekuwa wakisisitiza uadilifu, jambo ambalo Rais Magufuli analifanya.
“Napongeza ukatili wa Rais kukemea maovu,” alisema Shibuda.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekuja katika dunia ya
mabadiliko ya mila, jadi na utamaduni wa utendaji wa umma na kukomesha
uzembe katika uwajibikaji, ufisadi na kuleta msisimko unaoshangiliwa na
jamii na kuondoa zomeazomea dhidi ya Serikali.
Kiongozi huyo wa upinzani alisema ajenda ya vyama vya upinzani imenyauka na kuvitaka kuacha kutafuta mfereji wa kutorokea.
Badala yake, alivitaka vyama vya upinzani kujipanga upya ili viwe na mtazamo mpya wa utendaji wa shughuli za kisiasa.
Aliifananisha Serikali ya Awamu ya Tano na mabadiliko ya
tabianchi duniani, akisema Taifa limepata Rais mwenye utumishi changamfu
na kugusa hisia za jamii.
“Vyama vya upinzani viache siasa za mipasho na vijembe. Siasa
hizi hazitatui kero za umaskini, ujinga, uchumi wa kaya na wananchi,”
alisema Shibuda.
“Wanasayansi walianza na dawa ya panado zakutuliza maumivu,
lakini leo kuna dawa tatu na mseto kwa kuwa walishindana kugundua dawa
bora, basi na wapinzani wawe na vikosi kazi vya kubuni tiba mbadala ya
kutengua utumishi wa Rais Magufuli,” alisema Shibuda.
Alisema hakuna chama chochote cha kisiasa Tanzania ambacho kipo
kwa masilahi ya kukweza chama kingine, bali kila chama kipo kwa ajili ya
kugombania kushika hisia za jamii na kuwa na dola na wala chama
hakilazimishwi kufungamana na tafsiri ya chama kingine kwani kina sera
zake zaidi ya kufungamana siasa na itikadi ya chama chenyewe.
Alisema vyama vinaweza kuwa na ushirikiano wenye dhamira sahihi
ya kukuza masilahi ya jamii, ndiyo maana chama chake cha Ada Tadea
kinashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Shibuda aliwataka
wanasiasa kuwa na mawazo makini ya kunufaisha fikra za Watanzania.
0 comments:
Post a Comment