Kama
unakumbuka katika zile mechi mbili za Yanga na Medeama ya Ghana?
Kulikuwa na beki aliyeshiba, mwenye mwili mkubwa na mrefu kwelikweli
akicheza beki ya kati ambaye muda wote Amissi Tambwe alipata shida, basi
kwa taarifa yako tu, jamaa tayari ametua rasmi Azam FC na kuanza kazi.
Beki
huyo anaitwa Daniel Amoah ambaye katika mchezo wa awali wa Kombe la
Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Yanga
alisababisha Tambwe kutolewa uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na Juma
Mahadhi wakati timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1. Yanga ilifungwa
mabao 3-1 katika mchezo wa marudiano nchini Ghana.
Amoah
alitua nchini juzi akitokea kwao Ghana, Medeama walimuomba akawasaidie
kwenye mechi za mwisho za makundi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya TP
Mazembe na MO Bejaia. Hata hivyo, timu hiyo imeshindwa kufuzu nusu
fainali baada ya kufanya vibaya mechi ya mwisho.
Makamu
Mwenyekiti wa Azam, Idrissa Nassor ‘Father’ ameliambiaChampioni
Jumamosi: “Tunashukuru Amoah amefika. Alitua nchini usiku wa kuamkia
jana (juzi) na leo (jana) alikuwa sehemu ya kikosi kilichoanza mazoezi
baada ya mapumziko mafupi.”
Mbali
na Tambwe, Laudit Mavugo wa Simba ambaye anaaminika kwa kusumbua ngome
za ulinzi, atakuwa kwenye orodha ya kukumbana na gharika hilo la Mghana
akicheza sambamba na Pascal Wawa wa Ivory Coast.
Kikosi hicho kinatarajia kuendelea na mazoezi leo na kundi la wachezaji wasiofikia 15 ambao hawakuitwa kwenye timu za taifa.
SOURCE: CHAMPIONI.
0 comments:
Post a Comment