Na Beatrice Lyimo- MAELEZO.
Serikali
imetoa kauli kuhusu hali ya chakula nchini na kusema kuna chakula cha
kutosha pamoja na ziada ya asilimia 123. Ziada hiyo ya chakula inatokana
na uzalishaji wa msimu wa mazao mwaka 2015/2016 ambao unapelekea
upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba
jana mjini Dodoma alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu hali ya
chakula nchini.
“Takwimu
zinaonesha upatikanaji na mahitaji ya chakula nchini ni wa kuridhisha
kwa kiwango cha utoshelevu wa ziada kwa asilimia 123” Dkt. Tizeba.
Katika
kufafanua hali hiyo, Dkt. Tizeba alisema kuwa kulingana na takwimu
zilizopo hali ya upatikanaji na mahitaji ya chakula nchini inautoshelevu
wa ziada kwa asilimia 123 ambapo nafaka ni asilimia 113 na mazao yasio
ya nafaka ni asilimia 140 ambapo viwango vya ziada kwa mazao yote ya
chakula ni tani 3,013,515.
Dkt.
Tizeba aliongeza kuwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA)
inauwezo wa kuhifadhi jumla ya tani 246,000 ambapo kufikia Septemba 6,
ilikuwa na akiba ya tani 67,506.920 za chakula kinachojumuisha mahindi,
mpunga na mtama.
Pia
alisema kuwa Serikali inaendelea na mpango wake wa kuiongezea NFRA
uwezo wa kuhifadhi chakula katika kanda sita baada ya kupata mkopo wa
dola za Kimarekani million 55 kutoka Serikali ya Poland ambazo
zitatumika kujenga vihenge vyenye uwezo wa kihifadhi tani 190,00 na
maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 60,000.
Kuhusu
muda wa Serikali wa kutoa vibali vya kuuza chakula nje ya nchi, Dkt
Tizeba alisema kuwa lengo ni kutoa nafasi kwa Serikali kukamilisha
taarifa ya tathimini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa
mwaka 2015/2016 na hali ya upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017.
Mbali
na hayo, Dkt Tizeba alisema kuwa katika kuboresha hali ya usalama wa
chakula nchini, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
inapitia upya mfumo wa utoaji wa vibali vya kusafirisha chakula nje ya
nchi ili kuwezesha ufuatiliaji wa karibu kuliko ilivyo sasa.
Aidha,
Dkt. Tizeba alisema kuwa utoaji wa vibali vya kusafirisha mazao nje
umejitokeza baada ya kuona chakula kinasafirishwa nje bila kufuata
utaratibu maalumu ambapo wafanyabiashara wa nchi jirani walijihusisha
kununua vyakula vikiwa bado mashambani kabla ya kuvunwa.
Aidha,
alitoa wito kwa wananchi kuhifadhi chakula cha kutosha kwa matumizi
katika kaya ambapo ameitaka sekta binafsi kuendelea kushiriki katika
kutoa masoko ya kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye uhaba.
Kuhusu
hali ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayoikabili dunia ikiwamo
upungufu wa mvua , Dkt Tizeba alisema kuwa Serikali itaendelea na
juhudi za kuhimiza na kupanua kilimo cha umwagiliaji mashambani kwa
kuimarisha miundombinu iliyopo na uvunaji wa maji ya mvua ili kuongeza
uzalishaji wa mazao wenye tija.
Hata
hivyo, Serikali inaendelea kuhamasisha na kuelimisha wafanya biashara
kuuza unga nje ya nchi badala ya mahindi au mchele badala ya mpunga ili
kuendana na Sera ya kuendeleza Viwanda nchini na kuongeza thamani ya
mazao ya kilimo.
0 comments:
Post a Comment