WANANCHI
wametakiwa kutumia tafiti zilizopo ili kuboresha kilimo kuwa cha kisasa
na chenye tija ili kiweze kuwakwamua na umaskini.
Ushauri
huo ulitolewa na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa baada ya
kutembelea mabanda kwenye uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Mwalimu J. K.
Nyerere mjini Morogoro juzi.
Lowassa
alieleza kuvutiwa na mafanikio makubwa na ubunifu kwenye sekta ya
kilimo, mifugo na uvuvi na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza zaidi
katika maonyesho hayo siku za usoni kwa kujifunza.
Aidha,
Lowassa aliwashauri vijana kutumia maonyesho kama hayo kuwasilisha
tafiti walizozifanya katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, ili
Watanzania wengi waweze kuzitumia kwa manufaa ikiwamo kujifunza na
kubadilisha utendaji wa mazoea na kuwa wa kisasa kwa faida yao na taifa.
Lowassa
alisema maendeleo duniani yanafikiwa kutokana na tafiti na kushauri
kama Watanzania watatumia vyema matokeo ya tafiti zinazoendelea kufanywa
na wataalamu, wataweza kufika mbali.
Katika
ziara hiyo Lowassa alivutiwa na banda la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
ambamo alipongeza shughuli za uzalishaji wa kisasa wa mazao mbalimbali
ikiwamo mboga.
JKT
ilikuwa ikionyesha kilimo cha kutumia nyumba ya kijani (green house),
ufugaji wa kisasa wa mbuzi wa maziwa, kuku, uvuvi na teknolojia nyingine
zinazohusu sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Maonyesho
hayo ambayo kitaifa yalikuwa mkoani Lindi, yalifikia kilele jana kwa
kuhutubiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
0 comments:
Post a Comment