JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC), imeiomba Jumuiya ya Ulaya (EU), iipe muda wa miezi mitatu kujua hatima ya wao kusaini Mkataba wa Kiuchumi na Jumuia hiyo (EPA).
Uamuzi
huo ulifikiwa jana Ikulu Dar es Salaam na viongozi wa Jumuiya hiyo
baada ya kikao cha 17 kilichodumu kwa takribani saa sita.
Akizungumza
baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa EAC, Rais John Magufuli alisema
kikao hicho kilikuwa na ajenda nne, ila ya EPA ilikuwa ngumu kulingana
na uzito wake.
Alitaja
ajenda hizo kuwa ni ripoti ya mgogoro wa Burundi, kuingizwa rasmi kwa
Sudan Kusini kwene Jumuiya, kupitishwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa EAC na
EPA.
Rais
Magufuli alisema viongozi wote kwa pamoja walikubaliana kupewa muda wa
miezi mitatu ili Sekretarieti ya EAC iangalie na kupitia masharti ya EPA
kabla ya kusaini ili kila mmoja afaidike.
Hata hivyo nchi ambazo zilishasaini makubaliano hayo kutoka Jumuiya hiyo ni Kenya.
Alisema
katika kikao hicho, walibaini mambo 10 ambayo yanapaswa kuangaliwa
kabla ya kufikia uamuzi kwa maslahi ya nchi na wananchi.
Mwenyekiti
alitaja mambo ya kuangaliwa kuwa ni kwa namna gani nchi za EAC
zitafaidika, njia gani itatumika kuzuia bidhaa za kilimo na kulinda
wakulima.
Maeneo
mengine ni usawa, makusanyo yatokanayo na bidhaa zitakazoingizwa,
Burundi itasainije huku ikiwa imewekewa vikwazo na EU, kujitoa kwa
Uingereza EU na athari zake, kukosekana kipengele cha kuruhusu nchi
zingine kujihusisha na nchi za EAC kibiashara, kukosekana ushuru wa
forodha na kipengele cha nchi kujitoa pale inapoona haijaridhika na
mkataba.
Rais Magufuli alisema mkataba huo ukisainiwa kwa wakati huu, nchi wanachama zinaweza kuingia kwenye mtego mbaya.
“Tumejadiliana
kwa muda mrefu ila mjadala mkubwa ulikuwa suala la EPA ambapo
tumekubaliana tupewe miezi mitatu ili tukutane Januari na kutoa uamuzi
wa pamoja,” alisema Magufuli.
Alisema Tanzania iko kwenye mkakati wa kujenga viwanda, hivyo ni lazima iwe makini katika kusaini mkataba huo.
Aidha, aliiomba EU kutoiadhibu Kenya kutokana na uamuzi huo kwani nia yao ni nzuri hivyo wapewe nafasi.
0 comments:
Post a Comment