NA HAMZA TEMBA - WMU
Waziri
wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe ametangaza mabadiliko
makubwa katika biashara ya mkaa nchini na kusema kuwa kuanzia mwezi
Julai mwaka huu hakuna mkaa wowote utakaosafirishwa kutoka wilaya moja
kwenda nyingine ili kunusuru misitu inayoteketea kwa kasi hapa nchini.
Amesema
hayo jana wakati akifungua mkutano wa 24 wa baraza la wafanyakazi wa
Wizara ya Maliasili na Utalii uliofanyika katika ukumbi wa LAPF mjini
Dodoma na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali kutoka kwenye Idara, Vitengo
na Taasisi mbalimbali zilizopo chini ya Wizara hiyo.
“Kuanzia
mwezi Julai hakuna ruhusa ya kutoa vibali vya kuhamisha mkaa kutoka
wilaya moja kwenda wilaya nyingine, mkaa utachomwa, utauzwa ndani ya
wilaya kwa ajili ya matumizi ya watanzania wanaohitaji nishati ya mkaa,
lakini biashara ya mkaa ya kutoa Dodoma kwenda Dar es Salaam mpaka
Zanzibar marufuku.
“Wamekata
misitu yetu yote, mito yetu imekauka, tunashindwa kupata maji ya
umwagiliaji kwasababu watu wengi huko nje wanataka mkaa wetu, Tanzania
jamani sio shamba la bibi, wale wote watakaotoa mkaa kutoka eneo moja
hadi jingine kinyume na sheria hii watashuulikiwa kwa utaratibu wa
uhujumu uchumi”, alisema Maghembe.
Alisema
kuwa kwa upande wa miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro na
Tanga vitaanzishwa viwanda maalumu vya kuzalisha mkaa ambao utauzwa kwa
vibali maalumu katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Amesema mkaa huo
hautakuwa na athari nyingi za kimazingira kwa sababu utazingatia
taratibu za uzalishaji endelevu.
Wakati
huo huo, Waziri Maghembe amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma
za Misitu Tanzania kumuhamisha kituo cha kazi Mkuu wa Kikosi cha
Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu wa Wakala hiyo, Arjason Mloge
kutoka Makao Makuu ya Taasisi hiyo kwenda chuo cha Viwanda vya Misitu
(FITI) kilichopo mkoani Kilimanjaro na badala yake atafutwe mtu mwingine
muaminifu.
Alisema
uamuzi huo ni kufuatia udhaifu uliojitokeza katika usafirishaji wa
rasilimali za misitu ndani na nje ya nchi ikiwemo usafirishaji kwa
kutumia nakala za vibali ambazo sio halisi, yaani “Photocopies”.
“Agizo hili litekelezwe mara moja kabla ya saa sita mchana wa leo na niwe nimepewa nakala ya barua hiyo ya uhamisho” alisema.
Kufuatia
uamuzi huo amepiga marufuku kuanzia sasa usafirishaji wa mazao ya
misitu ndani na nje ya nchi kwa kutumia nakala zisizo halisi
(Photocopies). Ameongeza kuwa katika kuunga mkono Sera ya Uchumi wa
Viwanda ya Serikali ya awamu ya tano hakuna gogo litakalosafirishwa
kwenda nje ya nchi.
“Wawekezaji
wanahimizwa kujenga viwanda vya kuchakata magogo hayo hapa nchini ili
kutoa ajira kwa Watanzania pamoja na kutoa faida halisi inayotokana na
rasilimali hizo kwenye uchumi wa taifa”, alisema.
Akizungumzia
changamoto ya mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini amesema Sheria ya
Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 sehemu ya 21 (1) hairuhusiwi
kabisha kuchunga mifugo katika Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba,
Mapori Tengefu na Hifadhi za Misitu. Aliwataka watumishi wa Maliasili
kusimamia Sheria hiyo pamoja na kutoa wito kwa wananchi kuifuata
kikamilifu.
Katika
hatua nyingine, Waziri Maghembe aliwataka majangili wote nchini
kuachana na biashara hiyo haramu ambayo hailipi kwa sasa na badala yake
wachukue matrekta wakalime.
“Mtu
ambaye alikuwa anaishi kwa kutegemea ujangili sasa atafute trekta
akalime, kwa sababu akifanya ujangili tukamkamata tu, na tukimkamata
atakaa kwenye hoteli ya mkuu wa magereza (magereza) kwa zaidi ya miaka
25”.
Aidha,
Waziri Maghembe alitoa pongezi kwa watumishi wote wa Wizara ya
Maliasili kwa kazi nzuri wanayofanya ya kupambana na ujangili nchini
pamoja na ulinzi wa maliasili za taifa (Misitu, Wanyamapori na Mambo ya
Kale) ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 20.5 kwenye pato la taifa.
Amesema matokeo chanya ya kupambana na ujangili yameanza kuonekana japo
ujangili bado upo.
Kwa
upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Aloyce Nzuki
alimueleza Waziri Maghembe kuwa maelekezo yote aliyoyatoa yamepokelewa
kwa ajili ya kuyafanyiwa kazi, huku Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori, Prof. Alexandre Songorwa akimueleza Waziri huyo kuwa
watalinda na kusimamia Malisili za Taifa na kwamba katu hawapo tayari
kuandikwa kwenye vitabu kuwa walishiriki katika kutoweka kwa maliasili
hizo.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment