Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe
03 Oktoba, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa
Cuba Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa ambapo viongozi hao wamekubaliana
kuimarisha na kuongeza uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili
kwa manufaa ya wananchi wake.
Katika
Mazungumzo hayo Rais Magufuli amesema anatambua uhusiano na ushirikiano
mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Cuba na kwamba
Serikali yake imejipanga kuhakikisha uhusiano huu unaelekezwa katika
maeneo yenye manufaa ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Rais
Magufuli amemuomba Makamu huyo wa Rais wa Cuba kuwashawishi wawekezaji
wa kutoka nchini mwake kuja hapa nchini kujenga viwanda vya kutengeneza
dawa za binadamu ili kurahisisha upatikanaji wa dawa na kupunguza
gharama.
Pia,
Rais Magufuli amemuomba Makamu wa Rais wa Cuba Mhe. Salvador Antonio
Valdes Mesa kuwashawishi wafanyabiashara wa Cuba kuja kuwekeza katika
uzalishaji wa sukari na amewahakikishia kuwa wakiwa tayari Serikali ya
Tanzania ipo tayari kuwapa ardhi kwa ajili ya kuendesha uzalishaji huo.
"Mhe.
Salvador Antonio Valdes Mesa najua kuwa nchi yenu ina utaalamu wa
kutosha katika uzalishaji wa sukari, uzalishaji wa dawa za binadamu na
masuala mengine mengi yanayohusu matumizi ya teknolojia katika shughuli
mbalimbali za uzalishaji, nakuomba uwaambie wafanyabiashara wa Cuba kuwa
tunawakaribisha waje Tanzania kuwekeza na Serikali itawapa ushirikiano
wa kutosha" amesema Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Makamu wa Rais wa Cuba Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa
amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yake
katika kuinua uchumi wa Tanzania na amemhakikishia kuwa Cuba ipo tayari
kushirikiana na Tanzania kwa kutumia utaalamu na uzoefu wake.
Amesema
kwa kuanzia Cuba italeta wataalamu kwa ajili ya kuangalia namna
itakavyotekeleza ombi la kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za
binadamu na pia atazungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Cuba na
kuwashawishi kuja hapa nchini kuwekeza katika uzalishaji wa sukari.
"Mhe.
Rais Magufuli natambua kuwa uhusiano wetu na Tanzania na Afrika ni wa
kihistoria, sisi Cuba tumepiga hatua kubwa katika maendeleo ya uchumi na
teknolojia, nimekuja kukuhakikishia kuwa tutauendeleza uhusiano huu ili
ulete manufaa kwenu na kwa wananchi wa Cuba" amesema Mhe. Mesa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
0 comments:
Post a Comment