Tuesday 28 February 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa afungua mkutano wa watendaji Wakuu wa Mashirika ya umma,Ikulu.Fahamu zaidi hapa.

Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa  mapema leo 28 Februari 2017, ameongoza mkutano wa siku moja wa watendaji wakuu na wenyeviti wa bodi za mashirika ya umma, unaojadili nafasi za mashirika ya Umma katika utekelezaji wa Mpango wa Pili ya Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21), Unaofanyika Ikulu Jijini Dar e Salaam.

Mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina,Waziri Majaliwa amewapongeza wakuu hao ambapo amewataka kuhakikisha wanaongeza juhudi na maarifa katika mashirika yao ili kusonga mbele.

Akisoma hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wakuu hao kuongeza ubunifu zaidi ili kuongeza maarifa katika mashirika yao hii ni pamoja na kujiendesha kwa faida ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kujiendesha.

Majaliwa amelipongeza Shirika la Nyumba NHC ambalo kwa miaka ya nyuma lilikuwa likiendeshwa kwa hasara, hata hivyo baada ya kuongeza ubunifu na kuingia kijana mzawa, wameweza kupiga hatua na sasa wamekuwa wa mfano wa kuigwa huku pia akipongeza baadhi ya mifuko ya Maendeleo ya Jamii pamoja na mabenki mengine kwa ikiongozwa na benki kuu, kutokana na kuwa na menejimenti nzuri, ubunifu na kutumia wataalamu waliobobea  katika fani zao, wameweza kufanya mambo makubwa.

“Kumekuwa na dhana potofu kwamba Mashirika ya Umma hayatakiwi kufanya biashara,  na kwamba yakifanya biashara lazima yapate hasara inaendelea kubaki kuwa ni dhana potofu. Ipo mifano mbalimbali” ameeleza Majaliwa huku akitolea mifano ya nchi zilizofanikiwa kwa mashirika ya Umma  kufanya vizuri  mfano

Mashirika kama Petrobras la Brazil, Statoil la Norway, CNOOC la China ambayo ni makubwa na yameweza kuwekeza nje  ya mipaka ya nchi zao.

Majaliwa amesema mpaka sasa Serikali imeweza kuwa na Mashirika ya umma 264 ambapo kati ya Mashirika hayo, Mashirika 65 ni Mashirika ya Kibiashara, Mashirika 187 ni mashirika ya  huduma wakati mashirika 12 ni udhibiti. Kati ya Mashirika 65 ya kibiashara, Mashirika 8 yanaendeshwa kwa ruzuku ya Serikali, wakati Mashirika 57 hayategemei ruzuku ya Serikali.

Awali akifungua mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja amesema malengo ya mkutano ni kukusanya maoni ya viongozi kuhusu nafasi ya mashirika ya umma katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, kuzungumzia changamoto tarajiwa katika utekelezaji wa majukumu haya na kutoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo.

“Mashirika ya Umma yana nafasi na uwezo mkubwa wa kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano, 2016/17–2020/21 wenye kaulimbiu ‘Maendeleo ya Viwanda kwa Mabadiliko ya Kiuchumi na Maendeleo ya Watu’,” amesema Profesa Semboja.

Profesa Semboja aliongeza, “Katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais John Magufuli, mkutano huu umewezakutanisha viongozi kutoka serikalini na mashirika ya umma kwa lengo la kubadilishana maarifa na uzoefu wa jinsi mashirika haya yatakavyoiwezesha Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa maendeleo endelevu.”

Mkutano huo unajadili namna ya kuboresha mifumo ya kiutendaji ndani ya mashirika na uhusiano miongoni mwa mashirika na taasisi za serikali, kufungamanisha mipango ya mashirika ya umma na Mpango wa Pili wa Maendeleo, kutathmini kiwango na aina ya rasilimali zinazohitajika kuwezesha utekelezaji wa mipango na; kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mipango.

Jumla ya washiriki 100,  kutoka wizara, mashirika ya umma na mamlaka za udhibiti takribani 52 nchini.


Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment