HATIMAYE Prof. Ibrahim Lipumba, aliyekuwa Mwenyekti wa Chama cha Wananchi (CUF) ametangaza kurejea kwenye nafasi yake ya uenyekiti-taifa wa chama hicho.
Amesema,
anarejea kwenye nafasi hiyo baada ya muda wa kutosha alioutumia
kutafakari siasa za nchini na namna demokrasia inavyokanyagwa na
watawala wa nchi hii.
“Nimemwandikia Katibu Mkuu (Maalim Seif Sharif Hamad) kutengua barua yangu niliyoandika 5 Agosti mwaka jana,” amesema Prof. Lipumba.
Prof.
Lipumba alijiuzulu nafasi yake mwaka jana kwa madai ya kutoridhishwa na
uamuzi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kumridhia Edward Lowassa kupeperusha bendera ya umoja huo kwenye
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 kupitia Chadema.
Hata
hivyo amesema, analazimika kurejea kwenye nafasi ya uenyekiti wa chama
hicho taifa kutokana na kuguswa na matatizo ya demokrasia nchini.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam amesema kuwa,
amemuandikia barua Maalim Seif ili atengue uamuzi wake wa awali wa
kuachia nafasi hiyo.
Katiba
ya mwaka 1992 Toleo 2013 Ibara ya 117 inaeleza kwamba, barua ya
kujiuzulu inapaswa kujadiliwa na Mkutano Mkuu kujadili jambo ambalo
mpaka sasa halijafanyika.
Prof.
Lipumba aliteuliwa kutwaa nafasi hiyo na Mkutano Mkuu mwaka 1999. Ibara
hiyo inaipa mamlaka mkutano huo kukubali ama kukataa kujiuzulu kwake na
kwamba, kauli yake ya leo kuwa Maalim Seif atengue barua yake inatokana
na kutokwenda kwenye ngazi hiyo (Mkutano Mkuu) nyingine ya uamuzi.
Prof.
Lipumba amesema kuwa, dhuluma iliyofanyika katika visiwa vya Zanzibar
ya kuporwa kwa haki ya wananchi, imemsukuma kurejea kwenye mapambano ya
haki nchini.
Amesema, demokrasia ya Tanzania ina matatizo akitaja miongoni mwayo ni Bunge kuendesha kwa itikadi ya chama.
Pia amesema kuwa, uongozi wa Rais John Magufuli unaonekana kuwa wa kasi isiyojali Demokrasia.
Akizungumzia
Zanzibar amesema, chama chao na watanzania wapenda haki hawatambui
utawala wa Dk. Ali Mohammed Shein visiwani humo kwa kuwa hakupatikana
kwa njia halali ya kidemokrasia.
Amesema kuwa, Rais Magufuli asipozingatia misingi ya demokrasia nchi haitakuwa na uwajibikaji.
0 comments:
Post a Comment