MABINGWA wa England, Leicester City ni timu ya familia moja nchini Thailand.
Familia
hiyo inajulikana kwa jina la Srivaddhanaprabha, imeiongoza Leicester
City hadi kutwaa ubingwa. Leo kuna Watanzania wanataka kuingia na
kushangilia na kinachowavutia ni mafanikio, hakuna kingine.
Chelsea
kabla ya kumilikiwa na Roman Abramovich, huenda kulikuwa na Watanzania
wawili au watatu. Leo kuna maelfu kwa kuwa imefanya vizuri mfululizo.
Manchester
City pia, ilionekana kibonde na isiyo na mashabiki lakini leo hadi hapa
nyumbani ina mashabiki chini ya umiliki wa Mansour Bin Zayed Al Nahyan,
anayeimiliki kwa asilimia 87 na Serikali ya China asilimia 13. Hadi
serikali ya taifa la pili kwa uchumi duniani, linamiliki timu ya ligi
kuu.
Hakuna timu inayoshiriki Ligi Kuu England isiyo na mmiliki kwa maana ya kampuni au mtu.
Ujerumani,
wameweka asilimia 51 kwa wanachama na 49 kwa wamiliki wengine binafsi.
Nao wana mafanikio yao hata kama ni timu chache kama Bayern Munich na
Borussia Dortmund.
Hispania
hali kadhalika, timu kubwa zaidi za Real Madrid na Barcelona ni mali ya
wanachama lakini bado uendeshaji unaongozwa na bodi na anayechaguliwa
kuwa rais wa klabu sharti awe na uhakika kimaandishi angalau uwezo wa
kukopa benki kiasi kisichopungua euro milioni 50 (zaidi ya Sh bilioni
120), ili apate dhamana hiyo, lazima awe milionea. Jiulize, wanachama
vipi wanataka milionea awe kiongozi wao wa juu kabisa?
Wanajua
faida ya milionea kwa kuwa lazima atakuwa ni mfanyabiashara aliyepitia
mengi na anajua njia za kupita. Ndiyo maana hawakusema mwanachama yeyote
tu mwenye kadi.
Mwenyekiti
wa Yanga, Yusuf Manji ambaye kila mmoja wetu anajua ni bilionea,
ameamua kuwekeza Yanga ikiwa ni siku chache tu baada ya bilionea
mwingine, Mohamed Dewji ‘Mo’ kuamua kununua hisa asilimia 51 za Simba.
Kumekuwa
na mijadala mingi sana, hasa mitandaoni. Wengi wakiwananga wanachama wa
Yanga kwa uamuzi wao wa kupitisha Manji kuwekeza kwa miaka 10. Wengi
wao wanaonekana kuwa mashabiki zaidi kuliko hoja za msingi, mfano ni ule
ujumbe unaoelezwa kuwa wa Tundu Lissu anayeshangaa timu kukodishwa kama
roli, nafikiri hili suala ni ‘siriaz’, vema kuweka utani kando.
Wako
wanaotoa mfano wa Hispania, bila kueleza kilichofanyika hadi kufikia
hapo. Mashabiki wa Madrid dunia nzima ni zaidi ya milioni 40, lakini ina
wanachama 91,000 tu ambao hulipa ada hadi euro 123 (293,831) kila mmoja
kwa mwaka.
Yanga
ina mashabiki zaidi ya milioni 20 hapa nchini, wanachama wake hawafiki
hata 100,000. Wameamua kupitisha klabu yao kwa Manji awekeze kwa miaka
10 na faida ya asilimia 75 itakwenda kwake, 25 kwao. Kukiwa na hasara
yote inabaki kwake na umiliki wa majengo na viwanja unaendelea kubaki
kwa wao wanachama. Hapa hasara ni ipi?
Nani
anataka kusema Yanga ilijiendesha kwa faida na wanachama walifaidika
nayo, mwaka gani? Nani anayesema kumuacha Manji awekeze kwa miaka 10 ni
hasara kwao? Kivipi wakati wameimiliki kwa miaka 81 na karibu yote
imekuwa ni hasara na inafaidisha wajanja wachache hasa viongozi
waliokuwa na nia ya kushibisha matumbo yao tu!
Makampuni
makubwa yapo, wanahofia kuingia sababu ya migogoro na hofu ya
kuchafuliwa jina na wanaojiita wamiliki lakini kiuhalisia wanakuwa
hawachangii lolote kimaendeleo hasa linapofikia suala la kulipa fedha,
mfano ile ya ada.
Utaona
nimefafanua England, ni umiliki hadi asilimia mia wa makampuni au
familia. Ujerumani karibia nusu kwa nusu, Hispania ni asilimia mia
wanachama na mfumo wa bodi.
Lakini
Tanzania tayari tumefeli na mfumo wa wanachama, hakuna anayeweza
kupinga hili labda ni mgeni katika mpira. Hii ni uthibitisho tunatakiwa
kuhama na kujaribu mfumo mwingine.
Kupitisha
kwa Wanayanga Manji awekeze kwa miaka 10, hakuna dhambi kama wamefeli
kwa miaka rundo. Siku anairudisha timu yao, uhakika kutakuwa na
mabadiliko kwa maana ya miundombinu na ikiwezekana mfumo kifedha.
Neno
kukodisha, lisitumike vibaya na kuwakatisha tamaa wanachama wa Yanga
ingawa ni vizuri katika masuala ya uingiaji mikataba ndiyo wanapaswa
kujua mifumo na mipaka katika uwekezaji huo.
Miaka kumi, Manji amekwama wanachukua timu yao, nembo yao na kuendelea na hamsini zao. Lakini watakuwa wamejifunza jambo.
Kila
siku wapenda soka nchini wameigeuza TP Mazembe ya DR Congo kuwa mfano.
Wanajua ina mashabiki na wanachama lakini inamilikiwa na mfanyabiashara
Moise Katumbi. Dunia imebadilika na hakuna anayeweza kuyazuia mabadiko
hayo kwa mikono.
Kikubwa
ni kuangalia kabla ya kuingia kipi kifanyike. Tuache mihemko na
ushabiki maandazi kwenye masuala muhimu, badala yake tujadili hoja na
nini cha kufanya ili kuyavaa mabadiliko hayo. Tumekaa kwenye kisiwa peke
yetu, miaka nenda rudi ndiyo maana mafanikio kwetu ni bahati nasibu.
Kama
Leicester wangehofia kuiunga mkono timu ya familia, leo isingebeba
ubingwa na wote tumeona baada ya ubingwa walioingia mitaani na kukesha
wakisherehekea ni mashabiki na si familia ya Srivaddhanaprabha.
0 comments:
Post a Comment