WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo macho,
haijalala na haijashindwa kuongoza nchi bali imejipanga kuliongoza
Taifa kwa mafanikio makubwa.
"Serikali
haijashindwa kuongoza nchi. Nataka niwahakikishie waheshimiwa Wabunge
na wananchi wote kwamba tutaongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa na
kazi hiyo imeanza kwa marekebisho makubwa kwa maeneo ambayo tunadhani
yatafanya Taifa hili liweze kupata mafanikio makubwa,” amesema.
Ametoa
kauli hiyo leo (Alhamisi, Septemba 8, 2016) Bungeni mjini Dodoma wakati
akijibu swali lililoulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na
Mbunge wa Hai, Bw. Freeman Mbowe, ambaye alitaka kufahamu Serikali ina
mkakati gani wa kunusuru mdororo wa uchumi uliopo nchini.
Bw.
Mbowe alidai kwamba hali ya uchumi imeshuka na kwa mujibu wa taarifa za
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) uagizaji wa bidhaa kutoka nje umepungua,
uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na sekta ya ujenzi imesimama hali
inayoashiria kudorora kwa uchumi.
Kuhusu
suala la kupungua kwa mizigo katika bandari na vituo vya forodha,
Waziri Mkuu amesema usafirishaji wa mizigo kwa njia ya bahari umeshuka
duniani kote kwa sababu ya kushuka kwa hali ya uchumi kutokana na
kuporomoka kwa bei ya mafuta na gesi.
Hata
hivyo Waziri Mkuu amesema tayari wafanyabiashara wa Rwanda na Jamhuri
ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wameihakikishia Serikali kwamba mizigo yao
yote itakuwa inapitia Bandari ya Dar es Salaam hasa kwa mkakati wa
pamoja wa ujenzi wa reli ya standard gauge inayoanzia Dar es
Salaam-Tabora - Isaka.
Wakati
huo huo Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha inaendelea kuimarisha
amani na ulinzi kwenye maeneo yote nchini na kwamba vyombo vya dola
viko macho. “Watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu yakiwemo
mauaji watakamatwa popote walipo na kuchukuliwa hatua za kisheria,;
amesema.
Amesema
hatua hiyo inatokana na matukio ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni
ambapo raia wasiokuwa na hatia na askari waliuawa katika maeneo ya
Vikindu mkoani Pwani, Tanga na Mwanza. Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati
akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani
Katika
swali lake, Bw. Ngonyani alitaka kujua ya Serikali kuhusu kukomesha
mauaji hayo, yanayotokea kwa watu wasio na hatia pamoja na askari,
ambapo Waziri Mkuu, alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa wananchi na
familia, ambazo ndugu zao walipoteza maisha katika mauaji hayo.
Pia
ametoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha wanawafichua watu ambao
wanawatilia shaka na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili waweze
kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua
Habari na Ofisi ya Waziri Mkuu
0 comments:
Post a Comment