RAIS John Pombe Magufuli ameelezwa kuingizwa katika vita ambayo haina
sababu baada ya uamuzi wa vikao vya juu vya CCM vilivyokutana mkoani
Dodoma wiki iliyopita, Raia Mwema limeelezwa.
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), iliwavua uanachama baadhi ya
viongozi wa chama hicho, kuwaonya wengine na kuchukua hatua za kinidhamu
dhidi ya wale walioitwa wasaliti wa chama hicho.
Hata hivyo, baadhi ya waliokumbwa na hatua hizo wamedai kwamba Magufuli,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, ameingizwa katika vita ambayo hakuwa
na sababu nayo.
“ Unajua kwanini Rais Magufuli alipata nafasi ya kuwa mgombea urais wa
CCM mwaka juzi (2015)? Ni kwa sababu alikuwa na rekodi nzuri lakini pia
hakuwa na makundi.
“ Makundi yalimalizika baada ya uchaguzi ule wa ndani ya chama. Ndiyo
maana baadhi ya waliochukuliwa hatua walishiriki kwa hali na mali
kuhakikisha CCM inashinda kwenye uchaguzi ule.
“Watu hawakuwa na shida na Magufuli. Watu hawana mpango wa kumsaliti
Magufuli. Yale yalikuwa ni mambo ya uchaguzi na yalishapita. Huu sasa ni
mgogoro mwingine ambao haukuwa na sababu,” alisema mmoja wa wana CCM
aliyefukuzwa na NEC wiki iliyopita.
Katika historia yake ya takribani miaka 50, CCM imewahi kufukuza
wanachama wake kwa wingi walau mara mbili; ya kwanza ikiwa ni mwaka 1968
wakati TANU (mtangulizi wa CCM) ilipowafukuza viongozi walioonekana
kupingana na Azimio la Arusha na mwaka 1988 wakati ilipowafukuza akina
Maalim Seif Shariff Hamad.
Katika mara zote hizo mbili, mwisho wa hatua hiyo ilikuwa ni kutengeneza
kada ya wapinzani ambao ingawa bado hawajaitoa madarakani CCM, ndiyo
wapinzani wakuu wa chama hicho hadi sasa.
Viongozi wa CCM waliofukuzwa uanachama wa chama hicho ni wenyeviti wa
mikoa minne wa chama hicho ambao ni Jesca Msambatavangu wa Iringa,
Ramadhan Madabida wa Dar es Salaam, Erasto Kwilasa wa Shinyanga na
Christopher Sanya wa Mara. Mwingine aliyekumbwa na kadhia hiyo ni
aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Taifa, Sophia Simba.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kigoma, Josephine Genzabuke, alipewa onyo kali na kuvuliwa wadhifa wake huo.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa waliofukuzwa ni pamoja na Ali Sumaye wa
Wilaya ya Babati Mjini na Mathias Erasto Manga wa Wilaya ya Arumeru
huku Mjumbe wa Kamati Kuu, Emmanuel Nchimbi akipewa onyo kali na
kutakiwa kuomba radhi.
Kwa mujibu wa Katibu wa NEC (Itikadi na Uenezi), Humphrey Polepole, wote
waliochukuliwa hatua hizo walifanya usaliti dhidi ya chama hicho wakati
wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Inafahamika kwamba wote waliochukuliwa hatua walikuwa katika kambi ya
Edward Lowassa wakati akiwania kupitishwa na CCM kuwa mgombea wake wa
urais kwenye uchaguzi huo.
Karibu viongozi wote waliofukuzwa uanachama hawajazungumza hadharani na
vyombo vya habari lakini Raia Mwema limeambiwa takribani wote
wameshtushwa na hatua hiyo ingawa taarifa zilivuja walau wiki moja kabla
kuwa watavuliwa nyadhifa zao.
“Chukulia mfano wangu. Ni kweli nilimuunga mkono Lowassa wakati huo.
Lakini mara baada ya chama kutangaza kumkata, mimi nilipiga kampeni
Magufuli apitishwe. Na aliposhinda, nikapiga kampeni ili amshinde
Lowassa (akiwa mgombea wa upinzani nafasi ya urais).
“ Kwangu mimi, historia yangu na Lowassa iliisha baada ya yeye kuhamia
upinzani. Lakini kwa hatua hii, inaonekana sikufanya lolote na kwa kweli
nimesikitika sana,” alisema mmoja wa viongozi waliofukuzwa kwa masharti
ya kutotaka kutaja majina yake.
Ni kiongozi huyo ndiye aliyeliambia gazeti hili kwamba hakuna uamuzi wa
pamoja uliopangwa kufikiwa nao kwa sababu hakukuwa na mawasiliano kabla
na hawakujua kama hatua watakayochukuliwa ndiyo hii.
Raia Mwema limeambiwa kwamba wote waliofukuzwa na kuchukuliwa hatua
nyingine za kinidhamu walifanyiwa hivyo baada ya kuchunguzwa kwa
takribani miaka miwili na Kamati ya Maadili ya CCM inayoongozwa na
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.
Kwanini wamefukuzwa, kwanini wamepona?
Nchimbi, Sophia na Kimbisa walikuwa pamoja kwenye mkutano wa waandishi
wa habari uliofanyika kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kukata jina la
Lowassa miongoni mwa waliokuwa wakiwania urais kupitia chama hicho.
Hata hivyo, Sophia amefukuzwa kabisa wakati Nchimbi amepewa onyo na
kutakiwa kuomba radhi huku Kimbisa akiwa amesamehewa makosa yake.
Raia Mwema limeambiwa kwamba kamati hiyo ya Mangula ilibaini kuwa wakati
Nchimbi na Kimbisa walibadilika na kushiriki kikamilifu katika kampeni
za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Sophia hakufanya hivyo.
Gazeti limeambiwa kwamba si tu kwamba Sophia hakushiriki kikamilifu
kwenye kampeni hizo lakini kuna ushahidi wa yeye kuwa na mawasiliano
yanayotia shaka na vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa wakati huo.
“Ripoti ya Kamati ya Maadili iliweka bayana namna Sophia alivyokisaliti
chama wakati huo. Baada ya ukweli kuwekwa hadharani, wajumbe wa NEC
hawakuwa na namna zaidi ya kukubali afukuzwe uanachama.
“Hali ilikuwa hivyo kwa Msambatavangu wa Iringa. Kuna watu walitaka
kumtetea lakini zilionyeshwa picha za yeye kushiriki kwenye kikao cha
CCM siku moja na siku hiyo kushiriki kikao kingine cha Ukawa. Baada ya
hapo hakukuwa na msalia mtume,” gazeti hili limeelezwa na kiongozi mmoja
mwandamizi wa CCM.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Nchimbi alipewa kazi ya kuunganisha
vijana wa CCM na wale walio kwenye vyuo vikuu ili kusaka ushindi na
ilielezwa kazi yake ilikuwa nzuri. Kwa sababu hiyo, wajumbe wa NEC
waliomba kwamba Nchimbi asifukuzwe bali apewe onyo.
Kwa Kimbisa, gazeti hili limeelezwa kwamba kwanza aliwahi kuomba radhi
huko nyuma kutokana na tukio hilo la kupinga uamuzi wa Kamati Kuu,
lakini kilichomwokoa zaidi ni namna CCM ilivyoshinda vema katika mkoa wa
Dodoma ambako yeye ni Mwenyekiti wa Mkoa.
“Dar es Salaam kwa Madabida, CCM ilifanya vibaya sana . Ilipoteza
majimbo ya Kinondoni, Ubungo, Kawe na Kibamba. Na ilionekana yeye
hakufanya jitihada za maana kuokoa chama chake.
“ Lakini kwa Kimbisa kule Dodoma, CCM ilishinda majimbo yote. Wapinzani
hawakuambulia kitu. Kama Kimbisa angekuwa amecheza faulo kama za Dar,
CCM ingeshindwa na upinzani. Hapo ndipo alipookoka,” Raia Mwema
limeambiwa.
Kwa ujumla, wenyeviti wote na wajumbe wa NEC waliovuliwa nyadhifa zao au
kuadhibiwa wanatoka katika maeneo ambako CCM hakikufanya vema.
Bashe, Malima na Msukuma
Mojawapo ya tukio lililokuwa sehemu ya mkutano huo ilikuwa ni kuwekwa
ndani kwa wabunge wawili wa CCM; Hussein Bashe na Joseph Rusheku
(Msukuma) pamoja na mjumbe wa NEC, Adam Malima.
Raia Mwema limeelezwa kwamba vyombo vya usalama vya CCM vilielezwa
kwamba wanachama hao watatu walikuwa na mipango ya kuvuruga vikao hivyo
na ndiyo sababu wakakamatwa.
Hata hivyo, kinyume cha taarifa za awali kwamba wanasiasa hao walikuwa
na kiasi kikubwa cha fedha walichotaka kukitumia kuvuruga vikao hivyo,
hakuna aliyekutwa na ushahidi wa kuthibitisha.
“ Ndiyo maana nakwambia, kuna watu wanataka kumharibia Magufuli.
Wanataka kumgombanisha na watu ambao wanamuunga mkono. Mambo ya Lowassa
yameisha. Tujenge CCM ya Magufuli, mmoja wa watu walio karibu na
viongozi hao aliliambia Raia Mwema juzi Jumatatu.
Akizungumzia matukio ya vikao hivyo, msemaji wa zamani wa CCM,
Christopher ole Sendeka, alisema hatua zilizochukuliwa na chama chake ni
sahihi, zimekuja kwa wakati.
“Uamuzi wa NEC ( Halmashauri Kuu) ni sehemu ya mabadiliko
yatakayokiwezesha Chama kuwa na wanachama waadilifu na si mara ya kwanza
kwa CCM kufukuza wanachama wake wa ngazi za juu ukiukwaji wa maadili na
utovu wa nidhamu.
“Hili la kufukuza, kutoa onyo kali kuvuliwa uongozi ni utaratibu wa
chama chochote cha siasa kwamba lazima tufike mahali mtakase safu ya
uongozi ili kupata uongozi utakaotoa matumaini kwa wanachama na
wananchi,” alisema.
Akizungumza kwa mifano, Sendeka alisema CCM kimewahi kufukuza wanachama
wake huko nyuma, mwaka 1988, ambapo kilimfukuza uanachama Maalim Seif
Sharif Hamad aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu pamoja na NEC pamoja na
wenzake saba wakiwemo mawaziri kwa kukiuka maadili ya chama na
kimeendelea kuwa imara hivyo hilo si jambo geni kwa CCM kufikia maamuzi
magumu.
Mazingira ya mabadiliko ndani ya Chama yanayopunguza wingi wa wa vikao
vya Chama huku muundo ukibaki uleule isipokuwa idadi ya wajumbe. Mfano
Kamati kuu itapungua kutoa 34 hadi 24, Halmashauri Kuu kutoka 388 hadi
163 huku Mkutano Mkuu ukipungua kutoka 2,380 hadi 1,706 tu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisisitiza kuwa
mabadiliko makubwa ndani ya chama hicho ni jambo la kawaida na kwamba
yalianza tangu muda mrefu na kwamba wapinzani wao walifikia hatua ya
kukopa sera yao wakidhani ni jambo jipya.
Alisema CCM ni chama kikubwa na kina misingi yake iliyojengwa madhubuti
katika kuwatumikia wananchi wanyonge na ndio maana bado inaaminika na
kupewa kura nyingi za urais, ubunge udiwani na serikali za mitaa.
“Mabadiliko haya ni ya kawaida kabisa, na tutazidi kuwa imara zaidi,
hakuna wa kuiyumbisha CCM. Chama hiki kitaendelea kubaki imara na
wananchi wanatuamini na wanatuelewa,” alisema.
Credit - Raia Mwema
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment