Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amepiga
marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi na ametaka
mchanga wote ufanyiwe uyeyushaji hapa hapa nchini.
Rais
Magufuli ametoa katazo hilo leo wakati akiweka jiwe la msingi la
kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Kampuni ya Goodwill Tanzania
Ceramic Limited kilichopo katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Akizungumza
baada ya kutembelea kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru
Menejimenti ya kiwanda hicho kwa uwekezaji huo na ameelezea kufurahishwa
kwake na kutumika kwa teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea
vigae.
"Nchi
hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa
kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga
nje ya nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto
1,000, naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya
Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje
ya nchi" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kiwanda
hicho kikubwa Afrika Mashariki na Kati ambacho ujenzi wake umegharimu
Dola za Marekani Milioni 50 kwa awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa
kuzalisha mita za mraba 80,000 za vigae kwa siku, kitazalisha ajira za
moja kwa moja 1,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 2,000.
Akizungumza
kabla ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda hicho Katibu Mkuu wa Wizara
ya Viwanda, Biashara na uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru amesema pamoja na
kiwanda hicho, tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani jumla
ya viwanda 2,169 vinavyojumuisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa
vimesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na vipo katika hatua
mbalimbali za kukamilika.
Naye
Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amempongeza Mhe. Rais
Magufuli kwa kutilia mkazo juhudi za kukuza uchumi zilizowezesha
Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi kubwa
Barani Afrika na amebainisha kuwa China itaendelea kushirikiana na
Tanzania kuendeleza uwekezaji nchini Tanzania ikiwemo kujenga viwanda.
"Mhe.
Rais kwa mujibu wa takwimu za TIC mpaka mwisho wa Juni 2016 uwekezaji
wa moja kwa moja kutoka China umefikia Dola za Marekani Bilioni 6.6 na
umezalisha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 150,000 na zisizo za
moja kwa moja 450,000 na kiwanda hiki cha Goodwill Tanzania Ceramic
Limited kimejengwa na wawekezaji kutoka China, vipo viwanda vingine
vingi vinajengwa, Mbunge wa Mkuranga ameniambia kuwa kuna viwanda zaidi
ya 50 vya Wachina vinavyojengwa hapa Mkuranga, nimefurahi sana kuona
karibu kila sekta Watanzania wanafurahia ushirikiano wa Tanzania na
China" Amesema Balozi Dkt. Lu Youqing.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment