Kama
wewe unadhani huna fedha, basi kuna wengine ambao wamezichimbia
ardhini, tena kwa mamilioni. Benki ya chini ya ardhi iliyosheheni
mamilioni ya fedha, zilizoswekwa ndani ya mifuko myeusi ya plastiki na
kufukiwa mchangani, imechimbuliwa na matrekta ya kutengeneza barabara
jijini Arusha huku noti nyekundu zikitawanywa kila kona na kufanyika
kuwa 'Sadakalawe - Amina,' kwa kila mpita njia ambaye angeweza
kujitwalia fungu.
Ilikuwa ni mshikemshike katika eneo la Mianzini mjini Arusha , ambako kuna mradi mkubwa wa upanuzi wa barabara ya kutoka Mianzini Mataa hadi Ilkiding'a unaoendelea.
Watu
walipigana vikumbo katika harakati za kujineemesha na fedha zilizokuwa
zimetapakaa eneo hilo. Ikiwa imesheheni noti tupu, tena nyekundu na
mpya, kufumuliwa kwa akaunti hiyo ya benki ya chini ya ardhi pamoja na
kuwa neema kwa wapita njia na wakazi wa eneo hilo, kuligeuka pia kuwa
kilio kwa mmiliki wa hazina hiyo, Christopher Akoonay maarufu kama
'Mmbulu' ambaye sasa amejipatia jina jingine la 'Mabulungutu.'
Akonaay
ni mkulima, lakini hasa akijishughulisha na ufugaji wa ng'ombe wa
maziwa. Yeye hudamka asubuhi kukamua mifugo hao na kisha kusambaza
bidhaa hiyo ya maziwa katika maeneo mengi ya jiji katika kuwauzia wakazi
wa Arusha.
Na
katika siku ya tukio, Akonaay alikuwa yuko kwenye shughuli zake za
kuwapelekea maziwa wateja wake, ndipo watengeneza barabara walipofika
eneo hilo la Mianzini na tingatinga zao na kuanza kuichimba njia hiyo ya
kutoka Mianzini hadi Ilkiding'a katika kata ya Ilboru, inayotenganisha
Jiji la Arusha na wilaya ya Arumeru.
Ikiwa
imejengwa kwa fito na matope, nyumba ya 'Mmbulu' ilikuwa miongoni mwa
zile zilizobomolewa na ni baada ya wamiliki wake, kugoma kuzibomoa
wenyewe ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
“Shauri letu tulilipeleka mahakamani kudai fidia kabla ya mradi wa barabara haujapita hapa,” alisema
Akonaay na kuongeza kuwa mara baada ya kesi yao kutupiliwa mbali na
chombo hicho cha sheria, wajenzi hawakusubiri hata saa moja ipite, bali
walikwenda moja kwa moja eneo hilo na kuanza kazi.
Baadhi
ya wakazi wa Mianzini, wakizungumzia suala hilo kwa masharti ya
kutotajwa majina, walisema ni ajabu kwa Mzee Akonaay kuwa na kiasi
kikubwa cha fedha na kuzifukia ardhini huku mwenyewe akiishi kwenye
nyumba duni ya matope.
Lakini
Akonaay ambaye kwa sasa anaitwa 'Mabulungutu,' anasema kuwa alikosa
imani na benki maana wakati akifanya kazi serikalini miaka ya 1980,
alifungua akaunti na akawa anaweka fedha zake zote benki.
Baada
ya kustaafu mwaka 1994 na kuamua kushughulika na ufugaji,
hakuzifuatilia tena fedha zake benki hadi mwaka 2000, ambako alipokwenda
kuangalia fedha zake aliambiwa kuwa kwa sababu akaunti yake haikuguswa
kwa zaidi ya miaka 10, alitakiwa aende Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
kujieleza. Hata hivyo, aliona huo ni usumbufu na kuamua kuanza kuweka
fedha zake nyumbani.
Lakini
hii pia ilimtokea puani baada ya mmoja wa ndugu zake kuzikwapua zote
mara baada ya kuzifuma katika vitita vyenye thamani ya Sh milioni 20 na
zaidi. Sasa Akonaay akaja na mkakati mpya wa kuhifadhi fedha kwa
kuchimba shimo katikati ya chumba chake cha kulala, kilichokuwa upande
wa barabara ya Mianzini na kuanza kuweka hazina yake humo.
0 comments:
Post a Comment